Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo SAIKOLOJIA NA MAISHA. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo SAIKOLOJIA NA MAISHA. Onyesha machapisho yote

Jumatano, 6 Aprili 2016

Mambo 9 muhimu ya kufahamu kuhusu Ukatili kwa watoto, mzazi/mlezi utawezaje kumfahamu mtoto aliefanyiwa/anaefanyiwa ukatili



mtoto akiendelea akifanya kazi ya kupasua kokoto 
 
Mambo 9 muhimu ya kufahamu kuhusu Ukatili kwa watoto

Tatizo la Ukatili dhidi ya watoto, linaongezeka siku hadi siku, na kuleta athari mbalimbali za kimwili, kiakili, (kisaikologia) na kiafya kwa watoto. Watoto wanaumizwa, kubakwa, kunajisiwa, kutelekezwa, kusafirishwa kibiashara na kufanyishwa kazi za hatari zinazoathiri afya zao. Matendo haya ya kikatili hayakubaliki kabisa. 

Yafuatayo ni mambo 9 muhimu ya kufahamu kuhusu ukatili kwa watoto:

1.    Aina za ukatili 
Ukatili dhidi ya watoto upo wa aina nyingi. Ukatili wa Kijinsia, ni vitendo au maneno yanayoweza kusababisha madhara kwa mtu au kundi la watu kutokana na maumbile yao. (Mf: kuguswa bila ridhaa, jaribio la kubaka/kubaka, kulazimisha kufanya ngono n.k). Ukatili wa Kimwili ni kama kupigwa, kusukumwa, au kutishiwa kuuwawa kwa silaha. (Mf: kuonyeshwa kwamba hutakiwi, vipigo vya mara kwa mara) na Ukatili wa Kiakili/Kisaikolojia, kutelekezwa, kubaguliwa, kutishwa. (Mf: kuitwa majina mabaya, kunyimwa huduma za msingi, kufanyishwa kazi ngumu n.k)
 dada wa kazi akimfanyia ukatili mtoto

2.    Wahusika wa Ukatili dhidi ya watoto 
Utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto Tanzania ulifanyika mwaka 2009 na uliongozwa na Kikosi Kazi kinachojumuisha Sekta mbalimbali za Serikali, Asasi za Kiraia na Wadau wa Maendeleo. Katika utafiti huo ilionekana kuwa ndugu  wa karibu kama mjomba, baba, walezi na walimu ndio wanaosababisha ukatili dhidi ya watoto.  Kwa kuona hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wakaona umuhimu wa kuanzisha mpango wa kuelimisha jamii kuzuia ukatili dhidi ya watoto.

3.    Nini kifanyike kupunguza ukatili kwa watoto
Wananchi wote kwa ujumla wana jukumu la kuhakikisha kwamba wanawalinda watoto. Wazazi / walezi wanapaswa kujua watoto wao walipo na wanachokifanya kila wakati na kuhakikisha usalama wa mahali watoto wanapopenda kutembea mara kwa mara. Watoto wapewe moyo kuripoti vitendo mbalimbali vya ukatili.
watoto wakicheza katika mazingira hatarishi, hivyo ni jukumu la mzazi kujua usalama wa eneo ambalo mtoto/watoto hucheza
  
4.    Umuhimu wa kituo cha huduma ya simu kwa mtoto - namba 116
Kituo cha huduma ya simu kwa mtoto ni muhimu katika mifumo ya ulinzi wa mtoto nchini. Ni sehemu pekee ambayo mtoto au Mzazi/Mlezi anaweza kupiga simu na kutoa taarifa za ukatili kwa siri na kupata huduma ya ushauri nasaha na rufaa kwa msaada zaidi kwa mujibu wa tatizo lolote linalohusu ukatili dhidi ya watoto. PIGA SIMU BURE kwenda namba 116 kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto. 

5.    Uchumi na Familia
Familia zikiwa na hali ngumu ya kiuchumi husababisha ugomvi kati ya wanafamilia na hii huweza kupelekea kutelekezwa kwa watoto au kuwatenga watoto na familia, jambo ambalo litaongeza hatari ya ukatili na unyanyasaji wa watoto. Vilevile ugumu wa maisha ni kisababishi cha watoto wanaofanya kazi katika umri mdogo, kuchuuza /kufanya biashara ya watoto, mimba zisizotarajiwa na ndoa za utotoni. Hivyo basi ni muhimu wazazi/walezi kujishughulisha na kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa wanachama wa vikundi  ili waweze kuzalisha mapato ya kusaidia mahitaji ya familia.
Mtoto huyo akiwa katika kazi ya kupasua kokoto kazi ambayo inahitaji nguvu tofauti na uwezo wa mtoto 

6.    Madhara ya adhabu kwa watoto

Kuna madhara mengi sana ambayo yanaweza kuwapata watoto kutokana na kupewa adhabu mbalimbali. Adhabu huleta hasira na chuki ambayo haisaidii kuleta mabadiliko ya tabia. Kadri adhabu inapokuwa kali zaidi ndivyo inavyopelekea mtoto kuwa na matatizo ya kutojithamini, kuwa mhalifu, kupata magonjwa ya akili na kuwa na tabia ya ukatili. Adhabu mara nyingi haitoi mchango chanya kwa maendeleo ya mtoto

7.    Ishara ambazo huonyeshwa na watoto waliofanyiwa ukatili
Ni muhimu kwa wazazi/ walezi kutambua ishara mbalimbali zinazoonyeshwa na mtoto aliyefanyiwa ukatili. Ishara hizo ni kama vile mtoto kutojiamini hata kama anafanya kitu sahihi anakua na hofu kwa sababu tu anahisi anaweza kupigwa. Mtoto kukataa kwenda sehemu ambazo amezoea mf. shule, ukifuatilia kwa ukaribu utakuta kuna mtu anamfanyia ukatili huko au njiani.

8.    Wasikilize kwa makini
Ni muhimu kujijengea mazingira ya kumsikiliza mtoto kwa makini. Unapofanya hivyo ni muhimu ajue kuwa unamsikiliza, aidha kwa kutumia ishara bila maneno; kama vile kuashiria kwa kichwa. Mtazame mara kwa mara kwa mtazamo wa kirafiki.  Unaweza pia kurudia aliyokwambia kwa maneno mengine.
Mama akiwa karibu na watoto wake, hali ambayo huwafanya watoto kua huru na wenye furaha daima

 
Baba akiwa karibu na watoto wake, hali ambayo huwafanya watoto kua huru na wenye furaha daima
9.    Umuhimu wa vyombo vya habari kupambana na ukatili

Kwa mujibu wa mwongozo wa vyombo vya habari wa kuandika habari za watoto uliochapishwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), “Watoto wanahitaji uangalizi maalum wa kuwajali na kuwalinda. Wakati wa kuandika habari za watoto, vyombo vya habari vinapaswa kujenga taswira sahihi kwa watoto ili kuwaepusha katika hatari ya kuadhibiwa au kunyanyapaliwa. Watoto ni binadamu wanaohitaji kutambuliwa, kupewa hadhi, utu, heshima na zaidi ya yote kulindwa. Kutokana na ukweli huo, uelewa, umakini na weledi wa uandishi wa habari zinazowahusu wao kwa kuzingatia hali yao na mahitaji yao ni muhimu. Kimsingi vyombo vya habari vinatakiwa kuboresha uandikaji wa habari za watoto na wakati huo huo kulinda usalama wao kimwili na kihisia/jaziba.






 
 muandishi Emmanuel Lengwa wa gazeti la nipashe na ITV, alieripoti habari ya ukatili  dhidi ya Bahati Kaminyonge na wazazi wake, mtoto Bahati alifungiwa ndani kwa miaka 10 huko Mbozi Mkoani Mbeya,


Jumanne, 29 Machi 2016

Eric Shigongo atoa siri ya vijana wanaotoka kijijini kwenda mjini kufanikiwa zaidi kuliko wale wanaojiita wazawa wa mjini (born here here)

KWA NINI VIJANA WA MJINI HAWAFANIKIWI?.


Inawezekana na wewe umekuwa ukijiuliza swali hili lililokuwa likinitatiza kila siku kwamba kwa nini vijana wengi wanaoishi mjini huwa hawafanikiwi kama wale wanaotoka vijijini na kuja mjini?

Hili ni jambo linalowatesa watu wengi, wengine wamekuwa wakilalamika kwamba kwa nini fulani ametoka kijijini, kaja mjini kafanikiwa na wakati wao ni maborn town lakini bado wamepigika kitaa.

Nimefanya uchunguzi, nimezungumza na vijana wengi na nimefanikiwa kupata baadhi ya majibu ambayo leo hii ningependa kuzungumza nawe, labda tushauriane mawili-matatu, kama kuna hatua za kuchukua, basi uchukue ili na wewe ufike pale unapotakiwa kufika.

Kumbuka kwamba mimi pia nilizaliwa kijijini, nikakulia huko, nikaondoka na kuja Dar es Salaam ambapo sikuwa na ndugu, mvua zilikuwa zangu na jua lilikuwa langu. Sikuwa na pa kwenda, katika kituo cha mabasi ya mkoani (KISUTU) hapo zamani ndipo nilipokuwa nikilala. Niliumwa sana na mbu, lakini katika hayo yote, sikujuta, maumivu niliyosikia nilijipa moyo kwamba kuna siku yangekoma, kweli,

leo unapozungumza watu waliyoyabadilisha maisha yao kutoka kijijini na kuja mjini, basi mtoto wa mkulima, mimi pia nitakuwepo kwenye orodha hiyo. Hebu ngoja nikwambie kwa nini vijana wengi wa mjini hawafanikiwi kirahisi.

Hizi ndio sababu

KUJISHTUKIA Mjini kuna ajira nyingi kuliko vijijini ambapo ajira yao ni moja tu, kulima. Vijana wengi waliozaliwa mjini huwa hawafanikiwi kirahisi kwa kuwa wanajishtukia. Leo unaweza ukamwambia kijana wa mjini auze sabuni kwa kutembeza, lakini anaogopa, anamuonea aibu mtu fulani atamuona, lakini biashara hiyohiyo, mtu kutoka kijijini anafanikiwa na mwisho wa siku anaachwa kijana wa mjini akilalamika.

Unapoamua kutafuta maisha, usiogope kuchekwa, usiogope kudharaulika. Najua wengi hawataki kubezwa wanapofanya biashara za kutembeza pipi au nyingine, lakini kumbukeni kwamba hata matajiri wakubwa mnaowaona katika Tanzania hii, wameanzia hukohuko, kwenye biashara ndogo, zikakua na kuanzisha kubwa. STAREHE Hii nayo ni sababu mojawapo.

Vijana wengi wa mjini, baada ya kupata fedha kidogo, wanachokifikiria ni starehe tu. Kijana wa mjini yupo radhi atumie hata elfu hamsini kwa usiku mmoja tu na wakati kiasi anachoingiza ni kidogo. Kabla ya kufanya matumizi makubwa, hebu jiulize, je kuna umuhimu wa kufanya hivyo? Kama unataka kwenda sehemu kula bata kwa hamsini hiyo, hebu jiulize, je usipokwenda siku hiyo, utakufa? Je usipotumia kiasi hicho cha fedha maisha yatakwisha? Je utachekwa? Kama jibu lako ni hapa, basi achana nalo, acha fedha zako ziwe akiba na zikusaidie hapo baadaye.

Unapoanza starehe, kunywa pombe kupindukia, huwezi kufanikiwa, kila siku utakuwa mtu wa kulalamika. Nafurahi kumuona kijana akiendesha gari, lakini wakati anaendesha gari, nafurahi zaidi kumuona akiwa na biashara inayomuingizia kipato kikubwa. Huwa sifurahii kumuona kijana akiendesha gari, huku mafuta akitumia mshahara wake. Mtu kama huyu kufanikiwa ni vigumu, acha mshahara ufanye mambo mengine, gari ni gharama, wakati mwingine linaharibika, linahitaji vifaa vya gharama, je mshahara ndiyo utakaotumika tu? Na kama ndiyo, je fedha za matumizi na kufanyia mambo mengine zitatoka wapi?

KUJISAHAU Ndiyo! Wengine wanajisahau. Kama leo mtu akafanya kitu kikamuingizia laki moja, basi kesho hawezi kufanya kitu kama hicho, atakwambia mpaka fedha hizo ziishe kwanza. Hivi umekwishajiuliza kwa nini makonda wengi wa daladala hawafanikiwi? Wengi wanapata fedha nyingi, kwa siku konda anaweza kupata hata shilingi elfu thelathini mpaka hamsini, kweli mtu wa namna hiyo hawezi kufanikiwa? Kuna mtu anafanya kazi kwa mshahara wa laki mbili, na anafanikiwa, kwa nini mtu kama konda hafanikiwi? Nimewahi kukutana na makonda wengi, kauli zao ni kwamba wanapata fedha kila siku, leo akipata elfu hamsini, kesho inaingia nyingine sasa kwa nini niiweke hii ya leo? Ukisikiliza sababu zao unaweza kuona zina mashiko lakini hazina mashiko yoyote.

Mchukulie mtu kama Mengi au matajiri wengine, wanaingiza kiasi gani? Mbona wanajua kuweka akiba na huwasikii wakisema leo imeingia hii, nitumie yote kwa kuwa kesho itaingia nyingine?

Ni lazima fedha tunazozipata tuziweke matumizi sahihi na tusijisahau kwa kujipa moyo kwamba kesho itaingia nyingine. Kama tukipambana, tukiingiza fedha na kufanyia vitu vya msingi, tusiporidhika, tusipojisahau basi hii Tanzania itakuwa na mabilionea wengi sana na kila kijana atakuwa na maisha mazuri.

KUKOSA UBUNIFU Kuna wengine wanapata fedha lakini wanapofungua biashara, wanakosa ubunifu. Kabla ya kufungua biashara fulani ni lazima uangalie je ukiifungua biashara hiyo sehemu fulani, utapata wateja? Je biashara hiyo inahitajika mahali hapo? Huwezi kufungua baa sehemu yenye vijiwe vya wahuni, watu wataogopa kuja kwa kuwa wanaogopa kukabwa! Huwezi kufungua duka sehemu isiyokuwa na nyumba zaidi ya kumi, unapoamua kufungua biashara, ni lazima uangalie sehemu na kisha ufanye ubunifu. Hapo ndipo ambapo vijana wengi wamekuwa wakifeli, wengine wana

UBUNIFU Kuna wengine wanapata fedha lakini wanapofungua biashara, wanakosa ubunifu. Kabla ya kufungua biashara fulani ni lazima uangalie je ukiifungua biashara hiyo sehemu fulani, utapata wateja? Je biashara hiyo inahitajika mahali hapo? Huwezi kufungua baa sehemu yenye vijiwe vya wahuni, watu wataogopa kuja kwa kuwa wanaogopa kukabwa! Huwezi kufungua duka sehemu isiyokuwa na nyumba zaidi ya kumi, unapoamua kufungua biashara, ni lazima uangalie sehemu na kisha ufanye ubunifu. Hapo ndipo ambapo vijana wengi wamekuwa wakifeli, wengine wanaamua kuanzisha biashara ya mandazi sehemu ambayo kuna wauzaji wengi wa mandazi, je unapotaka kuanzisha biashara hiyo sehemu kama hiyo, unaweza kufanya ubunifu? Kama unaweza, fanya ila kama hauwezi, achana nayo.

Jirani anauza mandazi, na wewe hapa unaanzisha biashara ya mandazi, unahisi utaweza kupata wateja? Ni lazima ufanye ubunifu, yaani kama mtu anauza mandazi, angalia udhaifu wake, kama mandazi yake ni ya kawaida, yako yaweke hiriki, yako yafanye yawe makubwa, huo ndiyo ubunifu. Kama unataka kuanzisha biashara ya chipsi, angalia udhaifu wa mwenzako. Yeye anauza chipsi bila mishikaki, wewe weka na mishikaki, kama anauza chipsi bila samaki, wewe weka na samaki. 

Siyo yeye hana samaki, na wewe huna, yeye hata soseji, na wewe huna, yeye hana mishikaki, na wewe huna, ni lazima ufanye ubunifu. Sasa vijana wengi wa mjini wamekosa vitu hivyo na mbaya zaidi wengi wao hawataki kushaurika. Hili linawakosti sana na ndiyo maana wengi huanzisha biashara na kuanguka chini. Kwa leo acha niishie hapa, natumaini vijana wa mjini mtafanyia kazi yale machache niliyoshauri.


Asanteni. SHIGONGO

Ijumaa, 18 Machi 2016

Hisia 4 zitakazo weza kukwamisha malengo yako, furaha iliyopitiliza yatajwa pia



kisaikolojia inaelezwa kuwa, wakati mwingine hisia ni adui kwa sababu huweza kukudumbukiza kwenye anasa na hatimaye kujikuta unakwama kwenye kutimiza malengo yako. Hebu tuangalie 4 kihisia ambazo zimewafanya wengi washindwe kufikia malengo yao.

Ulishawahi kukaa na kujiuliza ni jinsi gani hisia zako zinaweza kukusukuma ukafanya jambo ambalo hukulitegemea? Huenda hujajiuliza lakini nikwambie tu kuwa hisia ni adui mkubwa wa maendeleo ya binadamu hasa kama utashindwa kuzizuia zisiathiri maisha yako.

HISIA 4 ZINAZOWEZA KUKWAMISHA MALENGO YAKO 

Furaha iliyopitiliza
Hali hii inapokutokea hujiona ni mtu unayeweza kufanya lolote lakini pia unaweza kujikuta unashindwa kufikia malengo mazuri uliyojipangia.

Mfano: Unadhani ni kwa nini kwenye mabaa na kasino wanatumia muziki mkubwa na kunakuwa na kelele nyingi? Hii yote ni ili kukufanya upate hisia ya furaha inayoweza kukusukuma kutumia mshahara wote hapo baa.

Hii ni kwa sababu kwa wakati huo una furaha kupitiliza kutokana na mazingira hayo, unajikuta unasahau malengo yako na hata shida za nyumbani.
mtu anapoenda sehemu za starehe katika vivyaji  anaanza kwa kujinunulia yeye na watu alioongozana nao, furaha ikizidi anaanza kugawa pombe kila meza akiamini ana hela nyingi kumbe zile pesa ni kwa ajili ya matumizi yaliyomfanya achukue mkopo.


Wasiwasi
Hii ni hisia nyingine mbaya ambayo inaweza kukusababishia ukaharibu mali zako na hata maisha kwa ujumla.
Wasiwasi katika maisha ya binadamu wakati mwingine husaidia lakini wakati mwingine huharibu mambo kabisa.


Unaweza kuwa unataka kufanya mabadiliko labda ya ofisi yako kwa kutumia fedha nyingi lakini usifanye lolote tu pale hali ya wasiwasi itakapokuingia kwani unahisi huenda ukiitumia fedha haitarudi. Huyu ni adui mkubwa na hakika huwezi kufikia malengo yako kama utakuwa ni mtu mwenye wasiwasi kila wakati.


Utakuta mtu anataka kufungua duka lakini anashindwa kwa kuhofia kuwa atakosa wateja na hela alizoziandaa kufungulia duka zikaenda bure, ‘huyu wasiwasi’ bado atakuwa ni adui kwa sababu haukupi nafasi ya kufanya jambo .


Huzuni
ukiwa na huzuni mara nyingi uwezo wa kufikiria na kupanga malengo huwa ni mdogo sana.
Hivi hujawahi kuona ukiwa na huzuni unatamani kulala tu au kwenda baa kukutana na watu, ingawa wengine huwa hawapendi hata kukutana na watu?


Hasira na kuhisi kuonewa
Hisia hizi ni hatari zaidi ya zote kwani kama usipokuwa mwangalifu unaweza kujikuta unafanya jambo ambalo si zuri kabisa, ukajihatarishia maisha yako na hata ya familia yako kwa ujumla.


Unaambiwa ukiwa na hasira usimtumie ujumbe wa sms mtu aliye kuudhi au usiongee mbele za watu maana unaweza kujikuta unadharaulika kwa maneno utakayo yatoa.
Ndiyo maana unashauriwa kutuliza hisia zako kwanza kabla ya kufanya jambo lolote linaloyahusu maisha. Kamwe usiruhusu hisia zikatawala maisha yako.



Kibinadamu huwezi kuishi bila kupatwa na hisia hizo lakini kikubwa cha kufanya ni kuhakikisha unazituliza ili zisije zikakuletea madhara, 


Ukihisi una furaha nyingi kaa mbali na pesa zako, ukiwa na huzuni jaribu kuwa karibu na watu wanaoweza kuipoteza kama siyo kuipunguza hali hiyo, ukiwa na wasiwasi pia washirikishe watu waliowahi kupitia mambo hayo watakushauri pia, lakini ukiwa na hasira fanya kila uwezalo kuzipunguza ikiwa ni pamoja na kunywa maji mengi.