Ijumaa, 12 Februari 2016

Je umeshawahi sikia kua bundi analeta uchuro? Na kwamba akilia juu ya paa la nyumba kama kuna mgonjwa atakufa? huu ndio ukweli

Bundi
Bundi ni aina ya ndege anayehusianishwa sana na masuala ya ushirikina. Tumesimuliwa tangu utotoni, kuwa bundi akilia kwenye paa ya nyumba, basi ni uchuro.

Kama kuna mgonjwa ndani, atakufa. Wengi wetu tumekua tukiamini hivyo. Hakuna ukweli katika hilo,

Nitafafanua kwanini bundi kulia kwenye paa si uchuro bali ni hali ya kawaida, kisayansi bundi ana tabia ya kutulia mchana na kuhangaika kutafuta chakula chake wakati wa usiku. Kama ilivyo kwa popo, bundi anaona zaidi usiku. Anapenda kukamata panya. Bundi anapenda pia kula viumbe vilivyokufa na kuoza, huvutwa na harufu ya uoza.

Nyumba zetu nyingi zina panya darini, na bundi akikuta usiku kuna nyumba ina mwanga wa taa, basi hutokea akatua kwenye paa ya nyumba hiyo na kuangaza kuona vivuli vya panya, hilo linafafanua kisayansi  kwa nini bundi atue kwenye paa la nyumba

Inakuwaje basi mgonjwa anapofariki dunia usiku ambapo bundi ametua kwenye paa na kulia? Hapa hakuna cha uchuro. Ni hali ile ile niliyoilezea hapo juu. Kinachoongezeka hapa ni harufu ya mgonjwa.

Ni kawaida na jadi yetu kwa wanandugu kupangiana zamu ya kukesha na mgonjwa aliye kitandani mahututi. Anayekesha huacha taa ikiwaka. Hutokea, kwa sababu mbali mbali, mgonjwa akiachwa bila kuoga. Mgonjwa hutoa harufu. Mazingira hayo, kama ni ya kijijini au mahali palipo na msitu wenye bundi, humvutia bundi kutua kwenye paa ya nyumba alimo mgonjwa.

Bundi huyo atakaa juu ya paa akisikilizia panya na hata kuvutwa na harufu. Atachoka kusubiri, atalia na kujirukia zake akiacha nyuma kilio kikubwa. Kila aliyesikia sauti ya bundi huyo atashtuka na hata kuanzisha kilio.

Kisaikolojia mgonjwa naye atakata tamaa ya kuishi, yawezekana kabisa, kabla ya kupambazuka, mgonjwa atakata roho. Ni hapo ataanza kutafutwa mchawi, maana bundi haji bure kwenye paa ya mgonjwa,

Tuache kutafuta majibu mepesi kwa maswali magumu. Imekuwa kama hulka yetu. Moja ya jibu jepesi kwa matatizo yetu ni ' kurogwa'.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni