Jumamosi, 9 Julai 2016

Nguvu ya MAZIWA MTINDI kwa Wanawake na Wazee!


Maziwa ya mtindi hunywewa na hata kuwa mboga na chakula kwa watu wengi, lakini sasa kwa wanawake ni muhimu sana kunywa kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa wa fangasi.

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umeeleza kuwa asilimia 70 hadi 90 ya wanawake nchini wanashambuliwa na aina mbalimbali za fangasi.

Wameeleza kuwa fangasi hizo zinatokana na sababu mbalimbali ambazo wanawake wanakumbana nazo katika maisha ya kila siku, ikiwemo ujauzito, matumizi ya kondomu kwa muda mrefu, kuchangia tendo la ndoa na mwanamume zaidi ya mmoja, nguo, maji, matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari na mazingira.

Utafiti huo umebaini sababu zinazochangia wanawake wengi kushambuliwa na vijidudu vya fangasi ikiwemo wanawake wenyewe kushindwa kujihifadhi vizuri. Aliongeza kuwa katika utafiti huo, walibaini pia kuwa wanawake wamekuwa wakishambuliwa na aina zaidi ya nne za fangasi.

Sababu nyingine alisema ni kutodhibiti matumizi ya sukari, ambapo fangasi huelemea kuta za seli na kuzalisha vimeng’ enya ambavyo hufyonza virutubisho na kuingia katika damu.

Fangasi baadaye huanza kujipenyeza kwenye damu, mapafu, moyo na hatimaye kushambulia figo ambapo huleta magonjwa nyemelezi na njia pekee ya kutibu ni kutumia mtindi mara kwa mara na kutumia dawa ambazo pia zinahitaji ushauri kwa daktari.

Utafiti huu ni muhimu kwa wanawake wote kuchukua hatua katika kupambana na fangasi ambao wakianza huwezi kujua kama wana maradhi kiasi hicho, lakini kila mmoja ahakikishe anatumia mtindi ambao ni chakula na dawa.

kila mwanamke ajikinge na kujitibu, ikiwa ni pamoja na kuona wataalamu wa afya kila unapoona dalili zozote za kuwa na fangasi. Lakini pia kuzingatia usafi wakati wote na namna ya kujihifadhi kama inavyoonekana kwenye utafiti huo, lakini kubwa zaidi ni kuhamasishana kunywa mtindi kwa ajili ya tiba hiyo.

FAIDA NYINGINE YA MAZIWA MTINDI :

Mtindi unaorodheshwa kuwa miongoni mwa vyakula bora kutokana na kuwa na virutubisho vingi vya aina mbalimbali ambavyo vina faida nyingi katika mwili wa binadamu.

Vikitajwa kwa uchache virutubisho hivyo, imethibitika kuwa mtindi ni chanzo kizuri cha ‘Calcium’, ‘Phosphorus’, ‘Riboflavin (vitamin B2), ‘Iodine’, ‘vitamin B12’, ‘Pantothenic acid (vitamin B5) ‘Zinc’, ‘Potassium’ na ‘Molybdenum’. Mbali ya virutubisho hivyo, ndani ya mtindi kuna ‘bakteria hai’ ambao ni muhimu kiafya katika mwili.

HUREFUSHA MAISHA:


Utafiti unaonesha kuwa unywaji wa mtindi mara kwa mara, hasa katika kundi la wazee, uwezo wa mwili wa kupambana na magonjwa mbalimbali umeonesha kuongezeka na kufanya mfumo wa kinga ya mwili kuwa imara zaidi.

Katika utafiti mmoja, walichaguliwa wazee 162 ambao walipewa utaratibu wa kunywa mtindi na maziwa zaidi ya mara 3 kwa wiki na kufuatiliwa maendeleo yao kwa muda wa miaka mitano. Baadaye utafiti huo ulionesha kuwa idadi ya vifo vya wazee hao ilipungua kwa asilimia 38 ukilinganisha na kundi la wazee wasiotumia au waliotumia mtindi kiasi kidogo sana.

KINGA KWA KINA MAMA:
Aidha, mtindi umeonesha kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza ukeni (vaginal infections). 

Katika utafiti mmoja uliohusisha wanawake wenye magonjwa ya kuambukiza sehemu za siri, baada ya kutumia mtindi kiasi cha paketi moja kila siku kwa muda wa miezi sita, maambukizi waliyokuwanayo wanawake hao kabla yalitoweka.

KINGA YA MWILI:
Utafiti uliofanywa kwa wanyama, wakiwemo panya na kuchapishwa kwenye jarida moja la masuala ya virutubisho nchini Marekani (Journal Of Nutrition), umeonesha kuwa unywaji wa mtindi kila siku, huamsha na kuupa nguvu mfumo wa kinga ya mwili kupambana na magonjwa kadhaa ya maambukizi, ikiwemo saratani ya utumbo.

MUHIMU KUZINGATIA:
Jambo muhimu la kuzingatia ni unywaji wa mtindi halisi uliotengenezwa kutokana na maziwa halisi ya ng’ombe, siyo mtindi uliotengenezwa kutokana na maziwa ya unga. Siri kubwa iliyomo kwenye mtindi ni ule uchachu unaotokana na ‘bakteria hai’ wanaopatikana baada ya maziwa kuganda na kuchachuka.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni