Jumamosi, 12 Desemba 2015

Kilimo cha Kisasa Kimebadili Ulimwengu



UNAPATAJE chakula chako? Je, unakinunua au unakikuza mwenyewe? Si zamani sana wanadamu wengi walikuwa wakulima wanaokuza mazao kwa ajili tu ya kujilisha wenyewe. Lakini sasa katika nchi fulani zilizoendelea kiviwanda, ni mtu 1 kati ya watu 50 anayekuza vyakula vyake mwenyewe. Mabadiliko hayo yalianzaje?
Maendeleo katika ukulima yalianza polepole kisha yakapamba moto. Kila hatua ya maendeleo ilileta mabadiliko makubwa kwa familia nyingi, na bado yanaendelea ulimwenguni pote. Kuchunguza jinsi maendeleo katika kilimo yalivyoathiri watu kutakusaidia kuelewa ulimwengu wa sasa.
Mabadiliko Makubwa Yaanza
Kwa kushangaza, katika karne ya 12 mbinu ya kutumia farasi waliofungwa ukanda shingoni huko Ulaya ilikuwa hatua moja muhimu iliyofanya watu waache kukuza mazao kwa ajili tu ya kujilisha wenyewe. Iliwezesha farasi kufanya kazi bila kujinyonga. Farasi waliofungwa wangeweza kuvuta kwa nguvu, kasi, na kwa muda mrefu zaidi kuliko fahali waliokuwa wakitumiwa hapo awali. Kwa kutumia nguvu hizo za farasi, wakulima wangeweza kukuza chakula kingi. Wangeweza kutumia plau za chuma kulima mashamba ambayo hayangeweza kulimwa hapo awali. Hatua nyingine muhimu ilikuwa kukuza mazao kama vile maharagwe, njegere, klova, na alfalfa ambayo yangeweza kurutubisha ardhi kwa nitrojeni. Udongo wenye rutuba ulizalisha mazao mengi zaidi.
Maendeleo hayo ya mapema yalitosha kuwasaidia wakulima kuzalisha chakula cha ziada ili wakauze. Hilo lilisababisha miji kukua ambako watu wangeweza kukunua chakula chao na kufanya kazi viwandani na kufanya biashara. Baadhi ya matajiri waliokuwa wakitokeza bidhaa viwandani, wafanyabiashara, na wakulima walikuja kuwa wabuni wa mashini za kwanza za kulima.
Katika mwaka wa 1700 hivi, Jethro Tull, mkulima Mwingereza, alivumbua mashini ya kupanda mbegu iliyokokotwa na farasi ambayo ilichukua mahali pa kupanda mbegu kwa mikono, mbinu iliyopoteza mbegu nyingi. Mnamo 1831, huko Marekani, Cyrus McCormick, alivumbua mashini ya kuvuna iliyokokotwa na farasi. Mashini hiyo ingeweza kuvuna nafaka mara tano zaidi ya mtu moja akitumia mundu. Pia wakati huohuo, wafanyabiashara walianza kuleta mbolea Ulaya kutoka pwani ya Milima ya Andes huko Amerika Kusini. Kutumiwa kwa mashini na mbolea kulitokeza mazao mengi shambani. Lakini hilo liliwaathirije watu?
Maendeleo katika mbinu za ukulima yalisababisha mvuvumko wa kiviwanda kwa kufanya miji iwe na vyakula vingi vya bei rahisi. Mvuvumko huo ulitukia kwanza huko Uingereza katika mwaka wa 1750-1850 hivi. Maelfu ya familia zilihamia miji yenye viwanda ili watu wakafanye kazi katika migodi ya makaa ya mawe, viwanda vya kufua vyuma, vya kutengeneza meli, na vya nguo. Hali ziliwalazimisha kufanya hivyo. Wakulima wadogo hawangeweza kugharimia mbinu hizo mpya za ukulima kwa hiyo walipokea malipo madogo kwa chakula walichokuza na hivyo hawangeweza kulipa kodi ya nyumba. Walilazimika kuacha mashamba yao na kuishi katika mitaa ya mabanda yaliyosongamana na yenye magonjwa mengi. Badala ya familia kulima pamoja, wanaume walilazimika kufanya kazi mbali na nyumbani. Hata watoto walifanya kazi kwa saa nyingi viwandani. Punde si punde, mataifa mengine yaliathiriwa pia na mabadiliko hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni