Alhamisi, 7 Januari 2016

Wang’ang’ania mzoga wa simba wakidai kua viungo vyake ni tiba ya kijadi pia ni zindiko



WATU wawili, baba na mwanawe wamekufa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa na simba mkoani Katavi. Tukio hilo lilijiri Januari 3, mwaka huu, ambapo mkazi wa kijiji cha Sitalike wilayani Nsimbo Wilaya ya Mlele, John Jeremiah (45) na mwanawe mwenye umri wa miaka mitano, walipouawa na simba baada ya kuwavamia wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Anjelo alisema kuwa kutokana na mlango wa nyumba waliyokuwa wakiishi kutokuwa imara, simba huyo aliuparamia, akausukuma na kuingia ndani.

Inadaiwa kuwa simba huyo baada ya kumjeruhi vibaya na kumsababishia kifo Jeremiah alimvamia mtoto wake na kula kiwiliwili chake ambapo alibakiza kichwa kisha akaondoka na kutokomea porini. Kijiji cha Sitalike kinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo wilayani Mlele.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Anjelo alitoa taarifa kwa askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambapo walianza kumsaka simba huyo wakishirikiana na wananchi na kufanikiwa kumuua simba huyo.

Inaelezwa kuwa baada ya kumuua simba huyo, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walitaka wapewe mzoga wa mnyama huyo kwa ajili ya kitoweo huku wengine wakidai viungo vyake ni tiba za kijadi na mazindiko, lakini askari hao wa wanyama pori walikataa na kuondoka na mzoga wa mnyama huyo kwa madai kuwa wanenda kuuteketeza kwa moto.

Wakati huo huo, watu wawili wameuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo na kukatwakatwa mapanga katika tukio lililotokea katika vijiji vya Bindi na Mwamkulu mkoani Katavi. Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Katavi, Focus Malengo alisema kwamba Januari 02 mwaka huu, saa saba usiku mtu aliyefahamika kwa jina la Chalya Kishosha (60), mkazi wa Kijiji cha Ibindi alikutwa akiwa ameuawa kikatili kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.

Alisema watu hao walimvamia akiwa amelala chumbani kwake. Tukio jingine lilitokea siku hiyo hiyo katika Kitongoji cha Center John katika Kijiji cha Mwamkulu Wilaya ya Mpanda ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Tiho Robart (40) alikutwa akiwa ameuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo.

Kaimu Kamanda Malengo alisema marehemu pia alivamiwa na wauaji hao wakati akiwa amelala ndani ya nyumba yake. Alisema kuwa chanzo cha mauaji katika matukio hayo mawili hakijajulikana na kwamba jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vya Mwamkulu na Ibindi wanaendelea kufanya msako ili kubaini waliohusika na mauaji ya watu hao na kuwafukuisha kwenye mkondo wa sheria.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni