Ijumaa, 11 Machi 2016

Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (T) Ltd (BCEG) ya China imekabidhi ramani za viwanja vya soka kwa uongozi wa klabu ya Yanga, ujenzi kuanza rasmi November mwaka huu, zitazame ramani hizo hapa





 

Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (T) Ltd (BCEG) ya China imekabidhi ramani za viwanja vya soka kwa uongozi wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam Tanzania iweze kuchagua mojawapo tayari kwa ujenzi utakaoanza Novemba mwaka huu makao makuu mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizoko jirani na Uwanja wa Taifa, Meneja Msaidizi wa BCEG, David Zhang Chengwei, alisema ni jukumu la Yanga sasa kuamua aina ya uwanja inaouhitaji, kulingana na uwezo wao wa kipesa, ingawa vyote ni vya kisasa.

Chengwei alibainisha kuwa bajeti ya Yanga katika mchakato wa uwanja ndio itakayoamua aina ya uwanja kulingana na gharama za ujenzi, huku akiongeza kuwa hata kukamilika kwake kutategemea na utayari wa fungu la ujenzi huo, ingawa sio chini ya miaka miwili.

“Gharama za ujenzi wa uwanja namba moja ‘A’ ni dola milioni 50, pamoja na ofisi, ukumbi wa mikutano, maduka, maegesho na sehemu ya mazoezi (gym). “Uwanja ‘B’ gharama zake ni dola milioni 40, huku ule ‘C’ ni dola milioni 30, ingawa vyote vina mahitaji muhimu niliyotangulia kuyataja,” alisema Chengwei.

Kwa mujibu wa ramani hizo, Uwanja A ambao ni wa kufunikwa juu, utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 50,000, kama ulivyo Uwanja B utakaochukua watazamaji 40,000, wakati Uwanja C utakaokuwa umefunikwa jukwaa kuu pekee utaingiza watazamaji 30,000 walioketi.

Akizungumza baada ya kupokea ramani hizo, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Yanga, ambaye pia ni Rais wa zamani klabu hiyo, Francis Kifukwe, aliishukuru BCEG kwa hatua iliyofikia katika mchakato huo, huku akiwataka kuwa na subira aweze kuwasilisha kwa Wanayanga, kuamua juu ya ramani ya uwanja wautakao.

Kifukwe aliongeza kuwa kutokana na ukubwa wa Yanga, si jambo zuri kwa yeye kudokeza ramani itakayotumiwa na kwamba uamuzi juu ya hilo ni wa Wanajangwani wote na kuwa baada ya mwezi mmoja watakuwa wamepata jibu juu ya uwanja uliochaguliwa na kukabidhi uteuzi huo kwa BCEG.

Alipoulizwa kama wanatarajia kuzipata kwa njia gani pesa za ujenzi huo, Kifukwe alisema kuna njia mbalimbali za kuwezesha kukusanya pesa za kujengea uwanja, ingawa kubwa na lililo wazi ni ukweli kuwa zitatoka kwa Wanayanga wenyewe.

Aliongeza kuwa Yanga ina eneo la kutosha (hekari 11) kuweza kujenga uwanja wowote kati ya hivyo vitatu walivyokabidhiwa, kwani ukubwa wa eneo lao ni zaidi ya lile lililotumika kujenga Uwanja wa Uhuru kwa zaidi ya hekari tatu na kwamba chaguo lao litazingia matakwa na uwezo wa kifedha na si eneo.

BCEG ni kampuni iliyojenga Uwanja wa Taifa kwa miaka mitatu na huu wa sasa wa Uhuru unaoendelea kwa mwaka wa pili, na uzoefu unawapa matumaini ya kumaliza dimba la Wanajangwani hao haraka, labda kama pesa za ujenzi zitatoka kwa mafungu ya kusuasua

Kikosi cha yanga sasa kipo nchini Rwanda mji wa Kigali kikiendelea kujifua kwa ajili ya mpambano unaotarajiwa kupigwa hapo kesho dhidi  APR (watoto wa kagame)  


Hizo hapo chini ni baadhi ya picha za wana yanga wakiendelea kujifua kabla ya mtanage, baadhi ya mashabiki wa timu ya yanga wanasema kuwa rais wa Rwanda Paul Kagame kesho atakua katika wakati mgumu kiushabiki kwa kua atapaswa kuonesha uzalendo kwa timu ya APR wakati huo huo yeye ni shabiki mkubwa wa timu ya yanga, hivo ni mechi ambayo itakua na hisia kali, 






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni