Jumanne, 6 Desemba 2016

Serikali inatarajia kuanzisha tuzo za umahiri, kwa waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii!!

Waandishi wa Habari wa Mitandao ya Kijamii wakiwa katika picha ya pamoja wakiji selfisha (selfie) na Waziri wa Habari mh. Nape Nnauye, hivi karibuni katika mkutano  mkuu wa mwaka wa waandishi wa habari za mitandao ya kijamii (TBN) uliofanyika jijini Dar es salaam.

Mwandishi wa habari za mtandao wa kijamii wa Mbeya yetu ndg. Joseph Mwaisango, akipeana mkono na Waziri wa Habari mh. Nape Nnauye,  katika mkutano wa waandishi wa habari za mitandao ya kijamii (TBN) uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam.

SERIKALI inatarajia kuanzisha tuzo za umahiri kwa waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii (blogs) nchini kuanzia mwaka 2017. Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na semina ya wanachama wa umoja wa waendeshaji wa blog nchini.


Waziri Nape alisema kuwa lengo la tuzo hizo ni kuzisaidia blogs za Tanzania kubobea katika nyanja tofauti ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda, hifadhi ya jamii kwa nia ya kuipa heshima tasnia ya habari nchini. Aidha, Waziri Nape alisema kuwa tayari Serikali imeanza mazungumzo na makampuni na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kudhamini tuzo hizo ili kuhakikisha kuwa washindi wanapatikana kwa uwazi.

“Tuzo hizo zitakuwa za kwanza kwa namna zitakazovyoendeshwa kwa uwazi hivyo makampuni zaidi yanakaribishwa kuweza kuzidhamini mashindano hayo yatakayojielekeza kwenye nyanja tofauti” alisema Waziri Nape. Waziri Nape pia alisema amewataka wamiliki na watendaji wa blogs nchini kushirikiana na Serikali ili kuweza kuijenga nchi.

“Tutumie fursa za kisiasa zilizopo, fursa za teknolojia ili kuhakikisha tiunajenga Tanzania tunayoitaka, ishaurini Serikali kwa kutumia taaluma mliyonayo ili kuweza kuipeleka nchi ya Tanzania tunayoitaka” alifafanua Waziri Nape.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni