Jumatano, 16 Desemba 2015

KILIMO BORA CHA NYANYA.



Utangulizi:

Nyanya ni zao la mboga ambalo hulimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Inahisiwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru/Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.

Uzalishaji wa nyanya duniani na hapa Tanzania

Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na Marekani, Italia na Mexico. Kwa upande wa Afrika nchi zinazo lima ni kama; Malawi, Zambia na Botswana. Zao hili hulimwa pia katika nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya, uganda na Tanzania.

Zao la nyanya linalimwa karibu maeneo yote ya Tanzania. Uzalishaji wa nyanya ni mkubwa kuliko mazao mengine ya mbogamboga yanayolimwa hapa Tanzania, uzalishaji wa nyanya kwa mwaka ni jumla ya tani 129,578 ikiwakilisha asalimia 51 ya mazao yote ya mboga. Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo ya Tanzania maeneo yanalolima sana nyanya ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Tanga (Lushoto), Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida. Morogoro ndiyo inayoongoza kwa kilimo hichi ikiwa na wazalishaji wenye zaidi ya hekta 6,159 (ekari 15,398). Pamoja na kwamba eneo la uzalishaji linaongezeka kwenye maeneo mengi lakini uzalishaji wa nyanya bado ni mdogo sana.

Uzalishaji mdogo unasababishwa na kupungua kwa rutuba ya ardhi, upepo, joto, ukame. Sababu nyingine ni pamoja na ukosefu wa aina za nyanya zenye mavuno mengi amabazo zinahimili mazingira ya kwetu, wadudu, magonjwa na magugu.

Mazingira

Hali ya Hewa:
Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa n.k.)

Udongo:
Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 - 7.0.

Aina za Nyanya

Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:

  1. Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Tebgeru 97. Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.
  2. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa)

Kotokana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika makundi mawaili:

  1. 1. OPV (Open Pollinated Variety) - Aina za kawaida
  2. 2. Hybrid – Chotara: Hizi ni aina zenye mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.
  3. Katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema.

Kuandaa Kitalu cha Nyanya

Mambo muhimu ya kuzingatia:

  • Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu
  • Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha
  • Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko kidogo ili kuepuka maji yasituame kwenye kitalu, mtelemko ukiwa mkali sana nao sio mzuri kwani husababisha mmomonyoko wa udongo.
  • Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au viazi mviringo (au mazao ya jamii ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.)
  • Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa miche kwenda sehemu nyingine. Pia kurahisisha usambazaji wa miche kwenda sehemu nyingine.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni