CHAMA CHA ACT WAZALENDO TAARIFA KWA UMMA Leo Juni 3/2016
Chama cha ACT Wazalendo Kimeelezea msimamo wake juu ya uamuzi
uliofanywa na Kamati ya Bunge ya Maadili na Madaraka ya Bunge kuwasimamisha
wabunge saba wa upinzani akiwemo Mbunge wa ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe.
Uamuzi huu wa Kamati ya Maadili ambayo sehemu kubwa ya wajumbe
wake ni wabunge wa Chama cha Mapinduzi(CCM) unafuatia msimamo wa wabunge wa
upinzani wakiongozwa na Mbunge wa Chama chetu kupigania maslahi ya wananchi
kupata habari za bunge.
ACT Wazalendo inaamini Wabunge hawa wametolewa kafara kwa kupinga
vikali uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.
Chama kimeandaa mapokezi haya yaliyopewa jina maalum la
“Opereshen” Linda Demokrasia, lengo likiwa ni kuwapa nafasi mashujaa
waliofukuzwa bungeni kwa ajili ya kusimamia maslahi ya umma, kuelezea
kilichotokea na kinachoendelea bungeni ambacho watawala hawataki kijulikane.
Pia katika mkutano wa hadhara Kiongozi wa Chama ndugu Zitto Kabwe
atafafanua kwa kina muktadha wa siasa za sasa na hatari ya kuua vita dhidi ya
ufisadi kutokana na namna demokrasia inavyofifishwa Kwa kutambua umuhimu wa
utetezi wa maslahi ya wananchi na kuisimamia serikali kupitia Bunge Chama chetu
baada ya mkutano wa Dar esSalaam utakaofanyika Jumapili ya Juni 5 mwaka huu
katika viwanja vya Mbagala Zakiem, pia Chama kitafanya mikutano mingine mikubwa
ya hadhara katika mikoa ya Mwanza ( 11 Juni, 2016), Kigoma (12 Juni, 2016),
Mbeya (18 Juni, 2016) na Morogoro (19 Juni, 2016).
Chama kimeviandikia barua vyama vya CUF, CHADEMA na NCCR-Mageuzi
kuviomba kushiriki kwenye mapokezi hayo.
Tunasubiri majibu ya vyama tulivyowaalika kwa kuwaandikia barua
kwa kuwa mpaka sasa hawajatujibu rasmi kama watashiriki ama la zaidi ya
kutufahamisha kuwa wamepokea barua zetu
ACT-Wazalendo,inaamini “Operesheni Linda Demokrasia” ni muhimu
ikapiganwa na vyama vyote pasipo kujali itakadi ya vyama kwa kuwa hoja hiyo ya
kutaka Bunge lioneshwe moja kwa moja ilipoibuliwa na Mbunge Ndugu Zitto Kabwe
kuhoji hatua ya serikali kubana uwazi Bungeni,wabunge wote wa upinzani
walisimama na kuiunga mkono hoja na kuitetea
Ndugu Ado Shaibu Ado Katibu,
Itikadi Uenezi na Mawasiliano ya Umma,
ACT Wazalendo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni