Jumapili, 19 Novemba 2017

Halmashauri ya Wilaya ya Kyela yajipanga kufanya kampeni ya kumhamasisha kila wananchi kuotesha miche 50 ya Cocoa!!


Wananchi wilayani Kyela mkoani Mbeya wametakiwa kuotesha kwa wingi miche ya zao la Cocoa kwenye maeneo yao katika msimu wa mvua ili kuongeza uchumi kwa kila moja na mapato ya Halmashauri.

Hayo yamesemwa  na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Hunter Mwakifuna wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa madiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela Hunter Mwakifuna akizungumza katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Akiuliza swali hilo diwani wa kata ya Mababu, Furahisha Mwasogela (CCM) juu ya mstakabali wa zao hilo kuendelea kupotea kila mwaka na wananchi wakiendelea kuwa maskini.

“Mweshimiwa Mwenyekiti ninataka kujua mstakabali wa zao la Cocoa kwani kwa sasa wananchi wamekata tamaa kulilima na uchumi umekuwa ukiporomoka, hata mapato ya Halmashauri tunakosa je Serikali imejipanga vipi kuhakikisha zao hilo linaendelea kudumu?”, aliuliza swali diwani huyo.

Aidha akijibu swali hilo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo alisema, Serikali ya wilaya hiyo imejipanga kuwaelimisha wananchi ili kujua umuhimu wa zao hilo na kuongeza upandaji wa miche mipya ambayo itakuwa na uzalishaji mkubwa.

Mwakifuna alisema ili kufanikisha adhima hiyo Halmashauri hiyo imeanzisha mashamba darasa kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi na wamefanya mazungumzo na kampuni ya Bioland ambao ni watengenezaji na wasambazaji wa miche hiyo ya Cocoa.

“Halmashari hii inatarajia kufanya kampeni ya kumhamasisha kila wananchi kupanda miche isiyopungua 50 ya zao la Cocoa katika kipindi cha robo ya msimu unaokuja ili kuongeza tija ya uzalishaji”, alisema Mwakifuna.

“Tumekuwa na shamba darasa katika eneo la Ndadalo lakini pia tumewahamasisha wadau wengine ambao ni kampuni ya Bioland inayotengeneza miche ya Cocoa na kuisambaza kwa wakulima wetu”, alifafanua Mwakifuna.

Aidha alisema wananchi wakiitikia wito huo wakupanda miche kwa wingi zao hilo litakuwa kinara kwa uzalishaji jambo ambalo litawainua kiuchumi wananchi pamoja na kuiwezesha Halmashauri kuendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Musa Mgata alisema katika kipindi cha mwaka 2016-2017 Halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya shilingi milioni 155 ikiwa ni mapato yaliyotokana na zao la Cocoa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni