UNAPATAJE chakula chako? Je,
unakinunua au unakikuza mwenyewe? Si zamani sana wanadamu wengi walikuwa
wakulima wanaokuza mazao kwa ajili tu ya kujilisha wenyewe. Lakini sasa
katika nchi fulani zilizoendelea kiviwanda, ni mtu 1 kati ya watu 50
anayekuza vyakula vyake mwenyewe. Mabadiliko hayo yalianzaje?
Maendeleo katika ukulima yalianza
polepole kisha yakapamba moto. Kila hatua ya maendeleo ilileta
mabadiliko makubwa kwa familia nyingi, na bado yanaendelea ulimwenguni
pote. Kuchunguza jinsi maendeleo katika kilimo yalivyoathiri watu
kutakusaidia kuelewa ulimwengu wa sasa.
Mabadiliko Makubwa Yaanza
Kwa kushangaza, katika karne ya 12
mbinu ya kutumia farasi waliofungwa ukanda shingoni huko Ulaya ilikuwa
hatua moja muhimu iliyofanya watu waache kukuza mazao kwa ajili tu ya
kujilisha wenyewe. Iliwezesha farasi kufanya kazi bila kujinyonga.
Farasi waliofungwa wangeweza kuvuta kwa nguvu, kasi, na kwa muda mrefu
zaidi kuliko fahali waliokuwa wakitumiwa hapo awali. Kwa kutumia nguvu
hizo za farasi, wakulima wangeweza kukuza chakula kingi. Wangeweza
kutumia plau za chuma kulima mashamba ambayo hayangeweza kulimwa hapo
awali. Hatua nyingine muhimu ilikuwa kukuza mazao kama vile maharagwe,
njegere, klova, na alfalfa ambayo yangeweza kurutubisha ardhi kwa
nitrojeni. Udongo wenye rutuba ulizalisha mazao mengi zaidi.
Maendeleo hayo ya mapema yalitosha
kuwasaidia wakulima kuzalisha chakula cha ziada ili wakauze. Hilo
lilisababisha miji kukua ambako watu wangeweza kukunua chakula chao na
kufanya kazi viwandani na kufanya biashara. Baadhi ya matajiri waliokuwa
wakitokeza bidhaa viwandani, wafanyabiashara, na wakulima walikuja kuwa
wabuni wa mashini za kwanza za kulima.
Katika mwaka wa 1700 hivi, Jethro
Tull, mkulima Mwingereza, alivumbua mashini ya kupanda mbegu
iliyokokotwa na farasi ambayo ilichukua mahali pa kupanda mbegu kwa
mikono, mbinu iliyopoteza mbegu nyingi. Mnamo 1831, huko Marekani, Cyrus
McCormick, alivumbua mashini ya kuvuna iliyokokotwa na farasi. Mashini
hiyo ingeweza kuvuna nafaka mara tano zaidi ya mtu moja akitumia mundu.
Pia wakati huohuo, wafanyabiashara walianza kuleta mbolea Ulaya kutoka
pwani ya Milima ya Andes huko Amerika Kusini. Kutumiwa kwa mashini na
mbolea kulitokeza mazao mengi shambani. Lakini hilo liliwaathirije watu?
Maendeleo katika mbinu za ukulima
yalisababisha mvuvumko wa kiviwanda kwa kufanya miji iwe na vyakula
vingi vya bei rahisi. Mvuvumko huo ulitukia kwanza huko Uingereza katika
mwaka wa 1750-1850 hivi. Maelfu ya familia zilihamia miji yenye viwanda
ili watu wakafanye kazi katika migodi ya makaa ya mawe, viwanda vya
kufua vyuma, vya kutengeneza meli, na vya nguo. Hali ziliwalazimisha
kufanya hivyo. Wakulima wadogo hawangeweza kugharimia mbinu hizo mpya za
ukulima kwa hiyo walipokea malipo madogo kwa chakula walichokuza na
hivyo hawangeweza kulipa kodi ya nyumba. Walilazimika kuacha mashamba
yao na kuishi katika mitaa ya mabanda yaliyosongamana na yenye magonjwa
mengi. Badala ya familia kulima pamoja, wanaume walilazimika kufanya
kazi mbali na nyumbani. Hata watoto walifanya kazi kwa saa nyingi
viwandani. Punde si punde, mataifa mengine yaliathiriwa pia na
mabadiliko hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni