Bundi |
Bundi ni aina ya ndege
anayehusianishwa sana na masuala ya ushirikina. Tumesimuliwa tangu utotoni,
kuwa bundi akilia kwenye paa ya nyumba, basi ni uchuro.
Kama kuna mgonjwa ndani,
atakufa. Wengi wetu tumekua tukiamini hivyo. Hakuna ukweli katika hilo,
Nitafafanua kwanini bundi
kulia kwenye paa si uchuro bali ni hali ya kawaida, kisayansi bundi ana tabia
ya kutulia mchana na kuhangaika kutafuta chakula chake wakati wa usiku. Kama
ilivyo kwa popo, bundi anaona zaidi usiku. Anapenda kukamata panya. Bundi
anapenda pia kula viumbe vilivyokufa na kuoza, huvutwa na harufu ya uoza.
Nyumba zetu nyingi zina
panya darini, na bundi akikuta usiku kuna nyumba ina mwanga wa taa, basi
hutokea akatua kwenye paa ya nyumba hiyo na kuangaza kuona vivuli vya panya, hilo
linafafanua kisayansi kwa nini bundi atue kwenye paa la nyumba
Inakuwaje basi mgonjwa
anapofariki dunia usiku ambapo bundi ametua kwenye paa na kulia? Hapa hakuna
cha uchuro. Ni hali ile ile niliyoilezea hapo juu. Kinachoongezeka hapa ni
harufu ya mgonjwa.
Ni kawaida na jadi yetu
kwa wanandugu kupangiana zamu ya kukesha na mgonjwa aliye kitandani mahututi.
Anayekesha huacha taa ikiwaka. Hutokea, kwa sababu mbali mbali, mgonjwa akiachwa
bila kuoga. Mgonjwa hutoa harufu. Mazingira hayo, kama ni ya kijijini au mahali
palipo na msitu wenye bundi, humvutia bundi kutua kwenye paa ya nyumba alimo
mgonjwa.
Bundi huyo atakaa juu ya
paa akisikilizia panya na hata kuvutwa na harufu. Atachoka kusubiri, atalia na
kujirukia zake akiacha nyuma kilio kikubwa. Kila aliyesikia sauti ya bundi huyo
atashtuka na hata kuanzisha kilio.
Kisaikolojia mgonjwa naye
atakata tamaa ya kuishi, yawezekana kabisa, kabla ya kupambazuka, mgonjwa
atakata roho. Ni hapo ataanza kutafutwa mchawi, maana bundi haji bure kwenye
paa ya mgonjwa,
Tuache kutafuta majibu
mepesi kwa maswali magumu. Imekuwa kama hulka yetu. Moja ya jibu jepesi kwa
matatizo yetu ni ' kurogwa'.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni