Serikali mkoani Geita, imepiga marufuku walimu kuvaa mavazi
yasiyolingana na taaluma yao na upakaji wanja na rangi mdomoni kupita kiasi
wanapokuwa kazini.
Ofisa utumishi wa
wilaya ya Geita, Thabitha Bugema alitoa agizo hilo wakati akizungumza na walimu
wakuu wa shule za msingi na waratibu elimu kwenye kikao cha muongozo wa kutumia
fedha za elimu bure zilizotolewa na serikali
Bugema alisema baadhi
ya walimu wanavaa mavazi ya upotoshaji ambayo hayaendani na ofisini
huku walimu wa kiume wakivaa suruali za jeans, fulana zenye nembo ya timu za mpira na wengine huvaa
mlegezo na kunyoa nywele mitindo isiyo ya heshima
“Nashindwa kuelewa wapo
walimu wanavaa kama wauza baa na kujipaka lipstick (rangi ya mdomo) na wanja kama
anakwenda kwenye kumbi za muziki usiku, wakuu wa shule sitegemei kuwaona
mkifumbia macho walimu wa aina hiyo,” alisema Bugema
Alisema kila mtumishi
wa Serikali anafahamu mavazi ya ofisini na kuwataka walimu kubadilika na kuvaa
mavazi ya heshima yanayo endana na taaluma yao.
Nae Ofisa Elimu Msingi
Wilaya ya Geita, Deus Seif alisema wamepokea sh.80 milioni kwa ajili ya elimu
bure na kuwataka wakuu wa shule kuhakikisha zinatumika kama ilivyopangwa
Mkuu wa wilaya hiyo, Manzie Mangochie aliwataka walimu na waratibu elimu kufanya mikutano ya wazazi ya kuwaelimisha maana ya elimu bure na kuwaeleza mambo ambayo serikali inafanya na wajibu wa mzazi kwa watoto.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni