Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group
(T) Ltd (BCEG) ya China imekabidhi ramani za viwanja vya soka kwa uongozi wa
klabu ya Yanga ya Dar es Salaam Tanzania iweze kuchagua mojawapo tayari kwa
ujenzi utakaoanza Novemba mwaka huu makao makuu mitaa ya Twiga na Jangwani,
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo
yaliyofanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizoko jirani na Uwanja wa Taifa,
Meneja Msaidizi wa BCEG, David Zhang Chengwei, alisema ni jukumu la Yanga sasa
kuamua aina ya uwanja inaouhitaji, kulingana na uwezo wao wa kipesa, ingawa
vyote ni vya kisasa.
Chengwei alibainisha kuwa bajeti ya Yanga katika
mchakato wa uwanja ndio itakayoamua aina ya uwanja kulingana na gharama za
ujenzi, huku akiongeza kuwa hata kukamilika kwake kutategemea na utayari wa
fungu la ujenzi huo, ingawa sio chini ya miaka miwili.
“Gharama za ujenzi wa uwanja namba moja ‘A’ ni dola
milioni 50, pamoja na ofisi, ukumbi wa mikutano, maduka, maegesho na sehemu ya
mazoezi (gym). “Uwanja ‘B’ gharama zake ni dola milioni 40, huku ule ‘C’ ni
dola milioni 30, ingawa vyote vina mahitaji muhimu niliyotangulia kuyataja,”
alisema Chengwei.
Kwa mujibu wa ramani hizo, Uwanja A ambao ni wa
kufunikwa juu, utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 50,000, kama ulivyo Uwanja
B utakaochukua watazamaji 40,000, wakati Uwanja C utakaokuwa umefunikwa jukwaa
kuu pekee utaingiza watazamaji 30,000 walioketi.
Akizungumza baada ya kupokea ramani hizo, Mjumbe wa
Bodi ya Wadhamini Yanga, ambaye pia ni Rais wa zamani klabu hiyo, Francis
Kifukwe, aliishukuru BCEG kwa hatua iliyofikia katika mchakato huo, huku
akiwataka kuwa na subira aweze kuwasilisha kwa Wanayanga, kuamua juu ya ramani
ya uwanja wautakao.
Kifukwe aliongeza kuwa kutokana na ukubwa wa Yanga,
si jambo zuri kwa yeye kudokeza ramani itakayotumiwa na kwamba uamuzi juu ya
hilo ni wa Wanajangwani wote na kuwa baada ya mwezi mmoja watakuwa wamepata
jibu juu ya uwanja uliochaguliwa na kukabidhi uteuzi huo kwa BCEG.
Alipoulizwa kama wanatarajia kuzipata kwa njia gani
pesa za ujenzi huo, Kifukwe alisema kuna njia mbalimbali za kuwezesha kukusanya
pesa za kujengea uwanja, ingawa kubwa na lililo wazi ni ukweli kuwa zitatoka kwa
Wanayanga wenyewe.
Aliongeza kuwa Yanga ina eneo la kutosha (hekari 11)
kuweza kujenga uwanja wowote kati ya hivyo vitatu walivyokabidhiwa, kwani
ukubwa wa eneo lao ni zaidi ya lile lililotumika kujenga Uwanja wa Uhuru kwa
zaidi ya hekari tatu na kwamba chaguo lao litazingia matakwa na uwezo wa
kifedha na si eneo.
BCEG ni kampuni iliyojenga Uwanja wa Taifa kwa miaka
mitatu na huu wa sasa wa Uhuru unaoendelea kwa mwaka wa pili, na uzoefu unawapa
matumaini ya kumaliza dimba la Wanajangwani hao haraka, labda kama pesa za
ujenzi zitatoka kwa mafungu ya kusuasua
Kikosi cha yanga sasa kipo nchini Rwanda mji wa Kigali
kikiendelea kujifua kwa ajili ya mpambano unaotarajiwa kupigwa hapo kesho dhidi APR (watoto wa kagame)
Hizo hapo chini ni baadhi ya picha za wana yanga wakiendelea
kujifua kabla ya mtanage, baadhi ya mashabiki wa timu ya yanga wanasema kuwa rais wa Rwanda Paul Kagame kesho atakua katika wakati mgumu kiushabiki kwa kua atapaswa kuonesha uzalendo kwa timu ya APR wakati huo huo yeye ni shabiki mkubwa wa timu ya yanga, hivo ni mechi ambayo itakua na hisia kali,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni