Alhamisi, 10 Machi 2016

Leo march 10, ni siku ya figo duniani, kauli mbiu “Chukua Hatua Mapema Kuepuka Magonjwa ya Figo kwa Watoto”



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAARIFA KWA UMMA TAMKO LA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
 
KUHUSU SIKU YA FIGO DUNIANI, TAREHE 10 MACHI, 2016,

Siku ya Figo Duniani huadhimishwa duniani kote kila AlhamisI ya pili ya mwezi Machi tangu mwaka 2006. Mwaka huu itaadhimishwa leo tarehe 10/3/2016. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Figo mwaka 2016 ni “Chukua Hatua Mapema Kuepuka Magonjwa ya Figo kwa Watoto”.

Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo ya figo yanayoikabili jamii yetu hususani watoto.Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inaadhimisha siku hii.

Wizara Kwa kushirikiana na Chama cha Watalaam wa Magonjwa ya Figo Tanzania kutoa elimu ya kujikinga na madhara ya magonjwa ya figo kwa kuzingatia kanuni za afya na kupima mapema ili kutambua na kupata matibabu kwa wakati.

Magonjwa ya figo huathiri utendaji wa viungo hivi muhimu katika mwili wa binadamu, miongoni mwa kazi za figo mwilini ni kutengeneza kemikali inayochochea utengenezaji wa chembe nyekundu za damu, kusaidia upatikanaji wa madini yanayoimarisha mifupa, kusaidia upatikanaji wa vitamin D mwilini, kurekebisha shinikizo la damu na kuondoa maji, uchafu utokanao na utendaji wa mwili na sumu mwilini. Magonjwa ya figo huathiri watu mbalimbali katika jamii bila kujali umri, kuanzia watoto wachanga mpaka wazee.

Magonjwa ya figo hutokana na sababu mbalimbali kulingana na umri wa waathirika. Magonjwa haya kwa watoto husababishwa na magonjwa mengine yakiwemo malaria, kichocho, homa ya manjano, kuhara, ugonjwa wa kisukari kwa watoto na maambukizi ya bakteria ya koo na ngozi.

Pia yapo magonjwa yanayotokana na matatizo ya mfumo wa mkojo ambayo watoto huzaliwa nayo. Zipo sumu na dawa za mbalimbali zinazoathiri figo ikiwa ni pamoja na dawa za maumivu kama diclofenac hasa zinapotumika kiholela.

Matumizi ya mitishamba yameripotiwa kuathiri utendaji wa figo. Kwa watu wazima chanzo kikubwa cha magonjwa ya figo ni ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu. Pia utumiaji wa dawa, mitishamba na magonjwa ya kuambukiza kama ilivyo kwa watoto yanaweza kuathiri figo kwa watu wazima. Yapo pia magonjwa mengi ambayo huathiri figo moja kwa moja mfano mawe ya figo na njia ya mkojo. 

Tafiti za ugonjwa wa figo zinaonyesha kuwa kati ya mwezi Agosti 2014 na Februari 2015 kati ya watoto 513 waliopimwa magonjwa ya figo katika Hospitali za Bugando na Sekou Toure asilimia 16.2% walikuwa na matatizo ya figo. Katika utafiti huo ilionekana watoto waliokuwa na magonjwa ya figo walikuwa na malaria, ugonjwa wa seli mundu (sickle cell anaemia) maambukizi ya bakteria kwenye koo na ngozi na kutumia mitishamba kabla ya kufika Hospitali. Utafiti huu unaonyesha wazi uwepo wa matatizo ya figo kwa watoto.

Utafiti mwingine uliofanyika Mkoani Kilimanjaro kati ya mwezi Januari na Juni 2014, uliohusisha watu 481 kutoka katika kaya 146, asilimia 7% walionekana kuwa na matatizo ya figo. Utafiti huu ulionyesha uhusiano wa karibu kati ya uwepo wa tatizo la figo na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na matumizi ya mitishamba.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya figo duniani kwa mwaka 2016, inalenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu kinga dhidi ya ugonjwa wa figo kwa watoto.

Jamii inawahamasishwa kuchukua hatua kuwahi Hospitali pale tunapohisi mtoto anaweza kuwa na ugonjwa unaoweza kusababisha matatizo ya figo. Pia ni muhimu kwa wananchi wote kuchukua hatua ya kupima ili kujua kama wana matatizo ya figo.

Pia ni muhimu kwa wananchi wote kuchukua hatua ya kupima ili kujua kama wana matatizo ya figo hasa wale wenye matatizo yanayosababisha matatizo ya figo hususani kisukari na shinikizo la damu.

Wizara inatoa wito kwa watoa huduma za afya kuhakikisha wanawapima matatizo ya figo mara kwa mara wale wote wanaosumbuliwa na magonjwa yanayoathiri figo yakiwemo kisukari na shinikizo la damu.

Pamoja na magonjwa yaliyoripotiwa kusababisha matatizo ya figo, yapo mambo yanayochochea uwezekano wa kupata magonjwa ya figo yakiwemo ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi, mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.

Ili kuzuia magonjwa ya figo na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata magonjwa yanayosababisha matatizo ya figo, na kwa wagonjwa ambao wana magonjwa yanayoathiri figo kama kisukari na shinikizo la damu ni vizuri wakazingatia ushauri wa wataalamu ama kutumia dawa kama wanavyoelekezwa ili kuzuia uwezekano wa kupata matatizo ya figo.

Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo matatizo ya figo.

Aidha, Serikali, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kimataifa na Taasisi zinazotoa huduma bila faida zinaendelea kuandaa na kurekebisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoimarisha uzuiaji na udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutumia maadhimisho haya kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani. Serikali inaendelea kuandaa miongozo na mikakati ya kisera kwa kushirikisha jamii katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo magonjwa ya figo, kisukari na shinikizo la damu.

Serikali imeimarisha ushiriki wa wadau mbalimbali na inaendelea kuhimiza Taasisi za Umma na za Binafsi kuweka mkazo ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa figo, Serikali imekuwa ikigharimia matibabu ya wagonjwa wenye matatizo ya figo ikiwemo upandikizaji wa figo kwa wale wagonjwa ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi kabisa.

Pia Serikali imejitahidi kusogeza huduma za figo kwa wananchi kwa kuanzisha huduma za figo kwa Hospitali za Rufaa baada ya kupeleka wataalamu wa magonjwa ya figo.

Hospitali zenye wataalamu wa magonjwa ya figo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya KCMC, Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando na Hospitali ya Benjamin William Mkapa iliyopo Dodoma.

Mpaka sasa wagonjwa 190 wakiwemo watoto wawili wamepata huduma ya kupandikizwa figo na wanapata huduma katika kitengo cha figo Muhimbili na katika Hospitali nyingine za rufaa. Pia Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha huduma za upandikizaji wa figo zinapatikana hapa nchini haraka iwezekanavyo ili kupunguza gharama za kupelekwa wagonjwa nje ya nchi na kutoa huduma kwa watanzania wengi zaidi.

Miongoni mwa mikakati iliyopo ni kuimarisha huduma za figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa wataalamu nje ya nchi kwa mafunzo ili kufanikisha upatikanaji wa hizo huduma hapa Tanzania. Tanzania inaungana na Mataifa mengine duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011 la kuwa na mpango kabambe wa kuthibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Lengo ni kuhakikisha Mataifa yote duniani yanapunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia lengo hili ni muhimu kushirikisha wadau wengi zaidi na kufanya kazi kwa ushirikiano. Wengi wetu wanaweza kuwa na matatizo ya figo bila kujitambua hasa wale wenye magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu.

Magonjwa ya figo yanaweza kuwa na dalili kadhaa zikiwemo kuvimba mwili kunakoanzia usoni, kupungua au kukosa mkojo kabisa, kukojoa mkojo wenye damu au rangi ya kahawia, kuwa na shinikizo la damu, kuchoka mwili na kupungukiwa na damu. Dalili hizi hujitokeza baada ya figo kupata athari kubwa, hivyo inawezekana kabisa mtu kuwa na tatizo la figo bila kuwa na dalili.

Mara unapoona una dalili nilizozitaja hapo juu ni vizuri ukaenda Hospitali ili upimwe na wataalamu na kupata matibabu au ushauri. Matatizo ya figo yakigundulika mapema inawezekana kupata matibabu ambayo yatazuia uharibifu wa figo na kumuwezesha mgonjwa kuishi bila kuhitaji matibabu makubwa ambayo ni ya gharama kubwa ikiwemo kupandikizwa figo.

Hivyo Wizara inatoa wito kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya yake kwa kuwa ugonjwa huu unaweza usionyeshe dalili yoyote mapema. Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya afya.

Endapo mtu atatambuliwa kuwa ana ugonjwa wa figo anashauriwa kutumia huduma za afya kulingana na ushauri atakaopewa na wataalam wa afya. Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya figo, kisukari na shinikizo la damu lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, wanaaswa kutumia huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na magonjwa hayo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
10 Machi, 2016

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni