Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi
(DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva
waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.
“mabasi kati ya 30 – 50 yatapita kwenye njia
zote za mradi huo. Zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo
waendesha daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya
mabasi yaendayo kasi si ya kwao, hivyo waanze kuzoea,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana wakati
alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa
na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa
ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
alizungumzia mradi wa mabasi yaendayo kasi wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Bw.
Sharifu Ramadhani ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri
kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja. “Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na
huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi taxi
ni gharama kubwa,” alisema.
Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi
huo, Majaliwa alisema: “Hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya
kukatia tiketi ambapo abiria atakuwa na kadi kama za benki ambayo anaijaza
fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia
kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.”
Alisema tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha
hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22,
2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni