Bodi ya Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF) iliyokaa Ijumaa Aprili 22, 2016 jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine ilijadili hali ya mwenendo wa tasnia ya habari nchini hasa juu ya haki ya wananchi kupata habari.
Katika kujadili hali hiyo, TEF imeguswa kwa namna ya kipekee
kabisa na mwenendo mzima wa urushaji wa bahari za Bunge kwa njia ya redio na Luninga,
hususani katika mkutano wa tatu wa Bunge la 11 unaoendelea mjini Dodoma
kwa kipindi hiki.
Itakumbukwa kwamba Muhimili wa Bunge
kupitia kitengo
chake cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Aprili 15 2016 ulitoa taarifa kwa umma
ikieleza utaratibu mpya ambao sasa umeanza kutumika katika kurusha matangazo ya
redio na luninga kutoka Bungeni.
Katika taarifa hiyo, Ofisi ya Bunge
ilisema kuwa imeamua kuboresha mfumo wa urushaji wa Matangazo ya Bunge kwa
Bunge lenyewe kurusha Matangazo ya Vikao vyake pamoja na Vipindi mbalimbali
vyenye Maudhui kuhusu Shughuli za Bunge ambazo hazijapata fursa ya kufahamika
vyema kwa umma kuanzia katika Mkutano wa Bunge la Bajeti unaoendelea sasa.
Ofisi hiyo ilisema kuwa mfumo huo mpya
ni Utamaduni wa kawaida kwa kila Bunge hususani Mabunge ya Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Madola kuwa na Studio zake kwa lengo la kurusha Matangazo ili
yawafikie wadau kupitia vituo vyao.
Kwa maana hiyo, Bunge lilisisitiza
kuwa chini ya utaratibu huo mpya, jukumu la kurusha Matangzo ya Vikao vya Bunge
litafanywa na Bunge lenyewe kupitia FEED MAALUM ili kurahisisha kila Kituo cha
Radio na Televisheni kupata Matangazo hayo kwa sehemu walipo bila kufunga
Mitambo yao Bungeni Dodoma.
Katika kutekeleza uamuzi huo na mfumo
huo mpya, kila kituo cha Televisheni na Redio sasa watatumia Masafa ya
Matangazo ya Bunge (Frequencies) bure kupitia FEED MAALUM itakayorushwa na
Satellite ya INTELSAT 17 ambayo iko nyuzi 66 Mashariki kwa masafa maalum ambayo
pia yaliwekwa wazi.
Kwa mantiki hiyo, Bunge sasa limezuia
vituo vyote vya televisheni nchini kupeleka kamera zake ndani ya Bunge kwa kuwa
habari hizo zitapatikana kwenye feed maalum ambayo ni ya Bunge ambayo
inasimamiwa na waandishi wa Bunge ambao pia ndio wanaamua nini kionyeshwe kwa
utashi wao.
Baada ya kutafakari hatua hizi mpya za Bunge na baada ya kufuatilia kile kinachorushwa, mambo
kadhaa yamethibitika:-!
Mosi, habari kutoka ndani ya Bunge
sasa zinachujwa mno kupitia mfumo huu mpya wa feed maalum.
Pili, ubora za picha zinazorushwa
kupitia feed hii nao ni wa kiwango cha chini pia.
Kwa
mantiki ya kawaida kabisa, hatua hizi zote zimepunguza na kukwaza haki ya
wanahabari kufanya kazi yao kwa uhuru, lakini pia inawanyima wananchi haki ya
kupata kwa uhakika na bila kuchujwa kile kinachofanywa na wawakilishi wao.
Kwa kuzingatia haya yote, TEF inasema bayana kwamba.
Hatua hizi mpya za kuzuia kamera za
televisheni kuingia Bungeni ni hatua za dhahiri kabisa za kukwaza uhuru wa
habari nchini na kukuza censorship nchini. Hali hii haisaidii siyo Bunge tu,
bali hata wabunge, wananchi na taifa kwa ujumla katika kupiga hatua za kweli
katika kujenga demokrasia na kulinda haki za kupata habari na uhuru wa
kujieleza nchini.
TEF imeanza kuingiwa na hofu kwamba
sababu za awali zilizokuwa zimetolewa za kuzuia utangazaji wa moja kwa moja wa
Bunge kupitia TBC kwa sababu ya gharama, huenda hazikuwa za dhati. Hali hii
imejionyesha hasa baada ya vituo binafsi vya televisheni kujitokeza na
kuendelea kuonyesha vikao vya bunge moja moja, lakini navyo sasa vimenyimwa
fursa hiyo kwa utaratibu huu mpya wa feed maalum.
Ni dhahiri sasa, ushiriki wa wananchi
katika kufuatilia mwenendo wa Bunge na wabunge wao umekwazwa sana kwa hatua
hizi mpya na kwa maana hiyo, kupunguza ushiriki wa wananchi katika mfumo wa
utawala wa nchi yao
Kwa kuzingatia haya yote, TEF inatoa
rai kwa uongozi wa Bunge kufikiria upya hatua hizi za kuzidi kufunika shughuli
za Bunge kwenye blanketi zito la usiri na censorship, hivyo kuruhusu kituo chochote cha televisheni
chenye nia, uwezo na utayari wa kurusha matangazo ya Bunge moja moja bila
kulazimika kujiunga na feed maalum iliyoanzishwa.
Tunaamini kwamba kama hali hii ya
kutumia feed maalum itaachwa iendelee hakika Tanzania kama taifa tunapiga hatua
nyuma kwa yale mazuri machache tuliyokuwa tumeyafikia, mojawapo, uhuru wa Bunge
kuendesha mambo yake kwa uhuru na uwazi mkubwa hivyo kuwa mfano mojawapo wa
taasisi za umma zinazojiendesha kwa uwazi.
Imetolewa leo, Jumapili Aprili 24 2016
jijijni Dar es Salaam na Jukwaa la Wahariri Tanzania
Theophil
Makunga
Neville Meena
Mwenyekiti
Katibu
Mmoja wa wanahabari akiulzia swali kwa viongozi wa jukwaa la Wahariri (hawapo pichani) |
Viongozi wa jukwaa la Wahariri wakisikiliza maswali kwa umakini wakati wa mkutano huo. |
Wanahabari wakiuliza swali kwa viongozi wa jukwaa la wahariri |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni