Hotuba ya Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo
Ndugu Kabwe Z R Zitto kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama iliyoketi
jijini Dar es Salaam tarehe 25 Aprili 2016
Ndugu Mwenyekiti wa Chama, Ndugu Makamu
Wenyeviti wa Chama, Ndugu Katibu Mkuu Ndugu wajumbe wa Kamati Kuu Ndugu Wajumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa Mabibi na Mabwana:
Leo tunakutana miezi sita baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 na takribani mwaka mmoja tangu tuzindue rasmi Chama chetu
kinachopigania kujenga siasa na jamii ya Ujamaa wa Kidemokrasia. Aidha, leo
tunakutana tukikaribia mwaka mmoja tangu tuzindua Azimio la Tabora ambapo
tulidhamiria kuhuisha Azimio la Arusha ambalo mwakani linatimiza miaka 50 tangu
litangazwe na Chama cha TANU kule mjini Arusha.
Aidha, na muhimu Zaidi, tunakutana miaka
miwili tangu chama chetu kiliposajiliwa rasmi. Nawapongeza Kamati ya Maendeleo
ya Jamii kwa kuandaa maadhimisho ya wiki ya chama kuanzia tarehe 1 Mei 2016.
Tangu tulipokutana Tabora mpaka leo kuna mambo mengi sana yametokea ikiwemo
Uchaguzi Mkuu ambao umewezesha Chama chetu kupata uwakilishi Bungeni na
kuongoza Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji na uwakilishi kwenye Halmashauri
za Wilaya 11 nchini. Chama chetu kimekua na sote kwa pamoja tujipongeze kwa
hatua kubwa tuliyopiga. Katika kujipongeza kwetu kuna watu mbalimbali ambao kwa
namna moja au nyingine wametusaidia kufika hapa tulipo.
Wengine wametangulia mbele ya haki, akiwemo
Ndugu yetu Mzee Estomih Malla aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na
mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini, na wengine katika ngazi
mbalimbali za chama. Viongozi wetu wa chama katika ngazi za kuanzia matawi,
kata na majimbo; katika ngazi ya mkoa na Taifa walijitahidi kwa kadiri ya uwezo
wao kukifanya chama kisonge mbele na kupanda mbegu. Nachukua fursa hii
kuwapongeza wote kabisa na kuwashukuru kwa kazi kubwa mliyofanya.
Kwa namna ya kipekee kabisa nampongeza
Mgombea wetu wa Urais, Mama Anna Elisha Mghwira na Mgombea Mwenza wake Ndugu
Hamad Yusuf, kwa kuzunguka nchi nzima kukitangaza chama chetu na kukiweka
katika ramani ya siasa nchini. Kazi haijaisha, lazima iendelee ili kuweza
kutimiza malengo yetu ya kujenga siasa mpya katika nchi yetu, siasa za masuala
na kuachana kabisa na siasa za matukio. Katika uchaguzi uliopita tulipenda
mbegu na ikaota.
Kazi kubwa tuliyo nayo sasa ni kuilea mbegu
hii na kuhakikisha kwamba inakua kwa kasi ili hatimaye mwaka 2020 chama chetu
kiweze kuchukua usukani wa kuongoza nchi yetu. Mpango Mkakati mtakoujadili na kuupitisha
leo umeanisha kwa kina namna ya kuilea na kuikuza mbegu hii. Timu yetu ya
Watendaji wa Makao Makuu ya chama na Vikao vya Halmashauri Kuu tayari
vimepitisha Mpango Mkakati kwa upande wao na sasa ni zamu ya Mkutano huu wa
Halmashauri Kuu kujadili na kupitisha Mwelekeo wa Chama chetu katika Miaka
mitano ijayo.
Kama myakavyoona, Kauli Mbiu yetu mpya inayopendekezwa ni SIASA
ni MAENDELEO (Developmental Politics). Tunataka tujihangaishe na mambo ya
wananchi, kero za wananchi, changamoto za wananchi na kushiriki nao kupata
mawajawabu ya Changamoto hizo. Tunataka kila mahala ambapo Chama chetu kimepata
uwakilishi kuongoza tofauti na vyama vingine; kuonyesha kuwa kweli tunataka
kufanya siasa tofauti.
Kila Mtaa ambao ACT Wazalendo ina Mwenyekiti
au mjumbe, kila Kijiji ambacho tunaongoza na kila Kata ambayo tuna Diwani,
lazima iwe tofauti kimaendeleo na kiuwakilishi. Kila Mamlaka ya Serikali ya
Mtaa ambayo tunaongoza tuonyeshe tofauti na Mamlaka ambazo wenzetu wanaongoza.
Tujikite kwenye mambo ya wananchi. Ndio Siasa ya Ujamaa inataka hivyo.
Hali ya Nchi yetu Kisiasa, Kiuchumi na
Kijamii Kisiasa Hivi sasa nchi yetu ina Serikali mpya. Rais ameanza kazi kwa
kasi kubwa katika eneo moja muhimu sana ambalo lilikuwa moja ya msingi mkubwa
wa kuanzishwa chama chetu – kupambana na ufisadi. Rais anaita ‘kutumbua
majipu’. Chama chetu kilimuunga mkono Rais katika hatua ya mwanzo kabisa katika
jambo hili.
Ninaamini kuwa bado tutaendelea kumuunga
mkono kwani ufisadi ni kansa na ni lazima kwanza kuizuia isisambae na kisha kuanza
kuitibu kabisa. Hatua ambazo zinachukuliwa sasa na Rais ni hatua muhimu sana
katika kuondoa ‘kutogusika’ kwa baadhi ya watu katika nchi yetu. Mnamkumbuka
wakati tunazindua Chama tulizungumzia kuhusu ‘cartels’ - vikundi maslahi
ambavyo vimeshika uchumi wa nchi yetu.
Hata hivyo, tunasema kuwa bado Rais hafanyi
inavyopaswa. Bado Rais anapapasa suala la Ufisadi. Kuna mambo ya muda mrefu
ambayo tunaendelea kama nchi kuyalipia Rais ameyakalia kimya. Mfano ni suala la
Tegeta Escrow. Bado Mtambo wa IPTL upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali
inawalipa matapeli hawa zaidi ya Tshs. 8 bilioni wazalishe au wasizalishe
umeme. Hivi ndio vikundi maslahi ama cartels katika sekta ya Nishati ambavyo
bila kuvibomoa Rais ataonekana anachagua katika vita hii.
Suala la HatiFungani ya dola za kimarekani 6
milioni. Ni kweli kwamba kuwa kuna watu tayari wamefikishwa mahakamani kwa
rushwa ya dola milioni sita. Lakini Serikali imeficha inaowaita madalali wa
rushwa hiyo. Walioitoa rushwa hiyo Benki ya Standard ya Uingereza haipo
mahakamani. Waliopokea rushwa hiyo maafisa wa Wizara ya Fedha hawapo
mahakamani. HatiFungani hii ambayo Serikali imeanza kulipa riba yake ni ghali
mno na imeongeza Deni la Taifa kwa kiwango cha shilingi 1.2 trilioni bila ya
riba.
Itakapofika mwaka 2020 ambapo tutakuwa tumemaliza kulipa deni hili,
tutakuwa tumelipa zaidi ya shilingi 1.8 trilioni, shilingi bilioni 600 zaidi!
Watanzania zaidi ya 2000 duniani kote wameweka saini kutaka Taasisi ya Rushwa
kubwa nchini Uingereza ( SFO ) kufungua upya shauri hili na kuitaka Benki ya
Standard iwajibike kwa ufisadi huu dhidi ya nchi masikini kama yetu.
Rais wetu angeongoza Watanzania kukataa
mikopo ya namna hii ambayo inafukarisha nchi ingekuwa ni hatua kubwa sana.
Lakini TAKUKURU wanaona ni sifa kuweka ndani watu kwa bilioni 12 bila kuwaambia
watu watakaofaidika na bilioni 600 zaidi tutakazolipa katika deni hili. Ndio
naama tunasema Rais na Serikali yake bado hawafanyi kazi ya kutosha katika vita
dhidi ya rushwa. Sio suala la kutumbua majipu tu, ni suala la kuweka mfumo
madhubuti ambao utazuia rushwa kabisa.
Chama chetu cha ACT Wazalendo ni lazima
kiendelee kuunga mkono juhudi zozote za kuondoa ufisadi nchini kwetu. Hata
hivyo Chama chetu ni lazima kiendelee kukosoa Serikali pale ambapo tunapoona
mambo hayaendi sawa. Tusiogope kuikosoa Serikali kwa hoja kwani kukosoa
Serikali ni tukio muhimu sana la kizalendo. Hivi sasa Wabunge wa vyama vya
Upinzani wamesusia Bunge kwa sababu kuu tatu. Moja ni Bunge kutoonyeshwa moja
kwa moja na Televisheni ya Taifa na Televisheni Binafsi, mbili ni Matumizi nje
ya mpango wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge na tatu ni Serikali kutokuwa na
‘instruments’ kwa Mawaziri.
Hoja hizi ni hoja za msingi sana. Ni Haki ya
wananchi kuona moja kwa moja namna ya wawakilishi wao wanavyofanya kazi.
Censorship ni moja ya dalili za kujenga udikteta nchini. Kwamba anayepaswa
kuonekana moja kwa moja ni mtu mmoja tu; inakuwa kama Korea Kaskazini hivi!
Hili ni jambo ambalo Chama chetu lazima kiungane na vyama vingine kulikemea
kwani ukiliacha hatujui kitafuata nini. Kwamba Bunge lina studio zake nk, ni jambo
la kuhadaa tu wananchi. Umeshawapa wananchi uhuru wa kuona Bunge moja kwa moja
kwa miaka 10, halafu leo unawanyang’anya? Mwalimu Nyerere alipata kusema “
jambo lolote linalowapa uhuru wananchi ni jambo la kimaendeleo”. Suala la
gharama ni hoja dhaifu mno maana kampuni huru kama Azam TV na Startv walikuwa
wanaonyesha bila hizo gharama za Serikali. Ni lazima kushikamana na wenzetu
katika jambo hili.
Suala la Matumizi kufanyika nje ya Mfumo wa
Bajeti ni suala la kisheria. Bajeti inaongozwa na Sheria mbalimbali kama vile
Sheria ya Fedha ( The Finance Act), Sheria ya Matumizi na Sheria ya Fedha za
Serikali ( Public Finance Act). Kuna taratibu za Fedha za Serikali kuhamishwa
kutoka fungu moja kwenda fungu jengine au ndani ya fungu husika. Katika Sheria
zote hakuna mahala Rais amepewa mamlaka ya kuhamisha fungu lolote lile. Hivyo,
hoja iliyotolewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Ujenzi
kuongezewa fedha mara 4 zaidi ya fedha ilizotengewa na Bunge ni hoja yenye
nguvu sana.
Izingatiwe kuwa Rais alikuwa Waziri katika
Wizara iliyoongezewa Fedha hizo. Sio hoja ya kupuuza. Tukipuuza leo Rais
anaweza kuamua kufanya lolote na nchi ikaingia kwenye taharuki. Lazima
tumkatalie ili ajifunze kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi
yetu. Mwalimu Nyerere alipata kusema “ Kuna mambo Rais akifanya, ya hovyo
wananchi wakatae, awe Rais awe Rais square”. Dhana ya Mamlaka ( Power) ni dhana
ngumu sana, ukilamba bila kuzuiwa utaendelea kulamba tu. Tumzuie Rais kupoka
madaraka ya vyombo vingine vya dola.
Tumuunge mkono kutekeleza madaraka yake ya
Urais lakini lazima tuhakikishe kwamba haingilii mamlaka ya vyombo vingine.
Suala la ‘instrumen ts’ ni suala linaloendana na suala la matumizi
kubadilishwa. Kimsingi bila instruments Baraza la Mawaziri lina watu 2 tu – Rais
na Makamu wa Rais. Kama Waziri Mkuu hana instruments hakuna Waziri Mkuu. Kama
Mawaziri hawana instruments, hakuna mawaziri. Hivi sasa Serikali ina mawaziri
hewa na hata maamuzi yao ni hewa. Instruments ni jambo la kisheria. Ndio
zinatoa mamlaka kwa Mawaziri kufanya kazi. Hivyo kutokana na kutokuwa na
Instruments kimsingi Rais ni Waziri wa Wizara zote nchini hivi sasa.Natoa wito
kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ahakikishe Mawaziri wanapewa instruments ili
waweze kuwepo kisheria na maamuzi yao yawe ya kisheria. Chama chetu kisikubali
nchi kuendeshwa na mtu mmoja kwa jina la Rais. Nchi yetu inaendeshwe kikatiba.
Hata hivyo nataka kuwaasa Wabunge katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge la 11 lazima liwe tofauti na
Mabunge yaliyopita. Mabunge yaliyopita yalikuwa na kazi ya kupambana na ufisadi
kwa sababu Serikali iliyopita ilionekana kutofanya kazi hiyo vizuri. Bunge lilijipa
kazi ya ‘kutumbua majipu’ na kuilazimisha Serikali kutekeleza Maazimio ya
Bunge. Hivi sasa kazi hiyo ya kutumbua majipu inafanywa na Serikali yenyewe,
inafanywa na Rais mwenyewe. Hivyo Bunge lazima litafute wajibu mpya katika
kipindi hiki. Bunge na hasa wabunge wa upinzani lazima sasa kutazama njia
mbadala za kuifanya Serikali iwajibike. Kwa mfano, ni dhahiri nafasi ya wazi
kabisa ni katika kuanisha mwelekeo wa nchi na kujenga mfumo madhubuti wa
uwajibikaji.
Ni lazima kubadilika na kubadili aina ya
siasa. Tusifanye mambo yanayotarajiwa; kwa mfano kutoka tu bungeni halafu
tunarudi tena. Kama Serikali inaenda kinyume na sheria, katiba na kanuni, kwa
nini tusifanye mikutano ya wananchi, bunge la wananchi ambapo tunajadili kwa
uwazi mambo yanayotusibu. Tunaweza kutumia vizuri digital technology
kuhakikisha ujumbe wetu unafika kwa wananchi bila kujali kama TBC wanaweka live
au la. Ni lazima tuwe innovative katika Siasa. Tusifanye siasa za kila siku.
Kiuchumi Serikali imewasilisha mpango wa Bajeti ambapo inatarajiwa kukusanya na
kutumia zaidi ya shilingi trilioni 29 katika mwaka wa fedha 2016/17. Hii ni
sawa na asilimia 28 ya Pato la Taifa ambalo sasa ni shilingi trilioni 98. Hata
hivyo kwa fedha zetu za madafu inaonekana ni nyingi sana, kwani inatokana na
kuporomoka kwa shilingi dhidi ya fedha za kigeni hasa dola ya kimarekani.
Hata hivyo ni Bajeti kubwa yenye ongezeko
kubwa hasa katika makusanyo ya ndani na mikopo ya ndani. Serikali itaongeza
wigo wa kodi na hata kufikia wachuuzi wadogo wadogo kama wamachinga ili kuweza
kupata fedha za kutekeleza Lakini pia Serikali itakopa fedha nyingi sana kutoka
nje ya nchi, takribani shilingi trilioni 2. Aidha, serikali itakopa sana kwenye
benki za ndani na hivyo kufukuzana na wafanyabiashara katika mikopo ya ndani.
Haya ni mambo ambayo ni muhimu kuyatazama katika muktadha mzima wa uchumi wa
nchi yetu.
Nina mashaka makubwa sana kama wachumi Serikalini
waliikalia vizuri Bajeti ianyopendekezwa kwani kuna maeneo ambayo yanatia
mashaka makubwa. Kwa mfano, Serikali inasema itaongeza mapato wakati mapato
katika bidhaa zinazoingizwa kutoka nje yameanza kushuka. Kwa mujibu wa Taarifa
ya Benki Kuu ya Mwezi Februari 2016, mizigo kutoka nje katika Bandari ya Dar es
Salaam imeshuka kwa 40%. Katika mazingira hayo na kuzingatia kuwa tunategemea
kodi ya forodha kwa asilimia 30 ya mapato yetu, mapato yatashuka tu. Vilevile
Serikali imeshindwa kuzingatia kuwa Uchumi wa Dunia sasa unashuka na Uchumi wa
Afrika unashuka. Tanzania sio kisiwa na inategemea sana uchumi wa Dunia na hasa
nchi kama China ambapo uchumi wao umeporomoka sana. Chama chetu kiitake
Serikali kuitazama upya Bajeti na kuelekeza fedha za kutosha katika maeneo
yatakayowezesha uzalishaji wa ndani na hasa katika sekta ya kilimo ili
kudhibiti kuporomoka kwa uchumi wa Dunia.
Kijamii Hali ya wananchi ni mbaya; bidhaa
zimeanza kupanda bei kuliko ilivyokuwa kabla ya uchaguzi. Chama chetu kijadili
kwa undani hali ya maisha ya wananchi na kutoa tamko na mapendekezo ya namna ya
kukabiliana na hali hiyo. Hali ya huduma za afya na elimu bado ni mbaya na
hakuna mabadiliko makubwa ya ubora wa elimu na huduma za afya. Chama chetu
kishauri Wabunge kuwatazama wananchi katika michango yao Bungeni ili Bajeti ya
nchi yetu ihangaike na keri za wananchi.
Hitimisho Ninawaomba wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya Chama muendelee kuwa wamoja na tuweze kujenga chama imara chenye kujali
shida za wananchi. Tuna wajibu mkubwa na uwezo wa rasilimali fedha mdogo licha
ya kwamba tuna rasilimali watu kubwa yenye kuweza kuleta mabadiliko. Ninawaomba
tusivunjike moyo bali tutumie kila tulichonacho kujenga chama chetu katika
misingi ya Ujamaa wa Kidemokrasia nchini kwetu.
Nawatakia mkutano mwema.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto,Mb
Kiongozi wa Chama
Jumatatu 25 Aprili 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni