Na. Catherine Sungura,
Wazazi nchini wametakiwa kuwakinga watoto wao wakati waendeshapo
magari kwa kuhakikisha wanawafunga mikanda ili kuwaepusha na ajali za
barabarani na kudhibiti madhara yatokanayo na ajali.
Rai hiyo imetolewa leo na kaimu kamanda kikosi cha usalama
barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi Fortunatus Musilimu wakati
akifungua mafunzo kwa Mawakili, Mahakimu, Waendesha Mashitaka na Askari
wapelelezi wa kesi za ajali za barabarani, iliyoandaliwa na wizara ya afya kwa
kushirikiana na shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia mpango wa Bloomberg
Initiative Global Road Safety.
Alisema wazazi wengi wanapokuwa wanaendesha magari hawawafungi
mikanda watoto wao na hivyo ajali inapotokea watoto wanakuwa ni wahanga wakubwa
kwa kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu “Wazazi mnawalindaje watoto, baba
anaendesha gari, mtoto yupo kwenye usukani anaendesha nae gari, hiyo siyo
sahihi, tuwalinde watoto wawe salama kwa kuvaa mikanda”
Aidha, Kamanda Musilimu alisema tatizo la ajali barabarani
nchini imekua likiongezeka kila mwaka na hii ni kutokana na wananchi kutokuona
kama ajali ni tatizo kubwa na la haraka ambalo linafanya kuongezeka kwa vifo
nchini kulinganisha na magonjwa mengine na hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa
kiuchumi
“Watu bado hawaoni kama ajali ni tatizo, vifo vinatokea hapohapo
na watoto wanabaki kuwa tegemezi, hizi ni changamoto hivyo mshirikiane
kubadilishana uzoefu ili muweze kutatua kesi zote zinazowafikia na kupunguza
malalamiko pamoja na kutenda haki,
alisema Takwimu za hapa nchini kwa miaka miwili zinaonesha mwaka
2014 zilitokea ajali 14,360,vifo 3,760 na majeruhi 14,530 na mwaka 2015
zilitokea ajali 8,337,vifo 3,468 na majeruhi 9,383,
Hata hivyo Ripoti ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2015
zinaonesha ajali huua watu 1.25 milioni Duniani kila mwaka, watu kati ya 20 na
50 milioni hujeruhuwa kila mwaka na hivyo asilimia 90 ya ajali hizi na vifo
hutokea katika nchi zenye uchumi wa kati na wa chini kama Tanzania.
Kamanda Musilimu alisema kasi hii ya ajali ikiendelea hadi
ifikapo mwaka 2030, ajali itashika nafasi ya 5 kwa kusababisha vifo Duniani.
Mradi wa Bloomberg Initiatives ni mradi wa miaka mitano hapa
nchini umeanzishwa mwaka 2015 ukiwa na nia ya kuweka vipaumbele vya kuzuia
vyanzo vya ajali hatarishi kama vile mwendo kasi, kutokuvaa kofia ngumu, kutokufunga
mikanda,vifaa maalumu vya kuwakinga watoto kwenye magari pamoja na ulevi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni