Wakati Rais John Magufuli akitoa
salamu za pole kwa wakazi wa jiji la Mwanza, kutokana na mauaji ya watu watatu
waliouawa kwa kukatwa mapanga wakiwa msikitini,
Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata)
limelaani mauaji ya watu watatu waliouawa kwa kukatwa mapanga wakati wakiswali msikitini.
Aidha, Baraza
hilo limewataka waislamu kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya
usalama ili wahalifu hao waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya
sheria.
Kauli hiyo
imetolewa na Mufti na Shekhe Mkuu Abubakari Zubeir wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu mauaji hayo yaliyotokea Jumatano saa mbili usiku
wakati waumini hao wakifanya ibada.
Shekhe Zubeir alisema tukio hilo la watu
wasiojulikana kuvamia msikiti na kuwaua waumini ni la kinyama ambalo halipaswi
kuvumiliwa.
Alisema
Uislamu ni dini ambayo moja ya misingi yake ni kulinda nafsi kama anavyosema
Mwenyezi Mungu katika Kitabu Kitakatifu cha Quran na kuongeza baraza hilo
linawapa pole wafiwa wote pamoja na waumini wa Masjid Rahmaan kwa msiba huo.
Aidha, alitoa
agizo kwa Bakwata Mkoa wa Mwanza kufuatilia kwa karibu hali za majeruhi na
wafiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni