Jumanne, 22 Desemba 2015

Mahindi kutoka mkoa wa Rukwa yabuma sokoni








WAKULIMA mkoani Rukwa wamelazimika kuuza mahindi yao kwa walanguzi kwa bei ya rejareja baada ya kukosa soko la uhakika ambapo gunia lenye uzito wa kilo 100 linauzwa Sh 30,000.

Hayo yalibainishwa na Meneja wa Kituo cha Kilimo cha Laela wilayani Sumbawanga, Ray Mtetewaunga alipokuwa akizungumza tuonane blog  kando ya mdahalo wa wadau wa kilimo uliofanyika hivi karibuni.
“Kutokana na wakulima mkoani hapa kukosa soko la uhakika la kuuzia mazao yao ya chakula hususan mahindi wamekuwa wakilazimika katika misimu kadhaa ya mavuno kuuza mahindi yao kwa walanguzi kwa bei ya kutupwa kati ya Sh 10,000 na 25,000.

Msimu huu wa kilimo ambapo mavuno ya mahindi yamekuwa hafifu bei imepanda kiasi kidogo ambapo wakulima wanauza kwa walanguzi gunia moja lenye uzito wa kilo 100 kwa bei ya rejareja ya Sh 30,000” alisema.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Viwanda (TCCIA) mkoani Rukwa, John Msabaha alisema kuwa masoko ya mahindi ndani na nje ya nchi sio tatizo tena isipokuwa mahindi kutoka mkoa wa Rukwa hayauziki katika masoko hayo kutokana na kutokuwa na ubora unaohitajika.

Pieta Mawazo mkulima kutoka kijiji cha Kavifuti wilayani Sumbawanga akichangia katika mdahalo huo, alieleza kuwa baadhi ya wakulima ambao si waaminifu wamekuwa wakichanganya ufuta na mchanga hivyo kupoteza ubora wake katika masoko ya ushindani.
Ofisa Kilimo wa Hamashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kwileluye Habona amebainisha chagamoto za uzalishaji na uuzaji wa zao la mahindi akisema kuwa wakulima wanashindwa kulima maeneo makubwa kutokana na ukosefu wa soko la uhakika ambapo husababisha kuuza mahindi kwa bei ya chini ukilinganisha na gharama za uzalishaji.

“Kwa mfano gharama ya kuzalisha gunia moja la mahindi lenye uzito wa kilo 100 ni Sh 39,615 kwa wastani , lakini mkulima amekuwa akiuza gunia hilo kati ya Sh 15,000 hadi 20,000 kwa walanguzi pale ambapo Serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga wanapokuwa haijanunua,”alieleza Kwileluye.

Takwimu za ulinganifu wa kiasi cha mahindi kilichouzwa kwenye masoko rasmi na yasiyo rasmi kwa misimu miwili ya mwaka 2013-14 na 2014 -15 inaonesha kuwa wakulima wilayani Sumbawanga walivuna tani 115,412.9 za mahindi ambapo NFRA Kanda ya Sumbawanga ilinunua tani 9,441.76 sawa na asilimia 8.18 ya ziada ya mahindi iliyozalishwa kwa msimu huo .
Katika msimu huo wa mavuno tani 105,971.14 ziliuzwa nje ya mfumo usio rasmi kwa bei ya kutupwa.

Katika msimu wa 2014-15 wakulima walizalisha ziada ya tani 121,627.9 za mahindi ambapo NFRA ilinunua tani 14, 241.9 za mahindi na tani 107,385.9 zilikuzwa katika masoko yasiyo rasmi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni