Jumanne, 6 Desemba 2016

Binti wa miaka 20, amejichoma kisu tumboni kisa mama yake kumhoji sababu za kushika ujauzito ili hali ana mtoto mdogo!!


Polisi mkoani Ruvuma inamshikilia binti mwenye umri wa miaka 20 Eva Kapinga, mkazi wa kata ya Mateka Halmashauri ya Manispaa ya Songea, kwa tuhuma za kumuua mtoto wake, Catherine Kapinga mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu (1.5), kisha nae kujichoma kisu tumboni kwa lengo la kutaka kujiua.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amesema tukio hilo limetokea juma lililopita siku ya alhamisi (December 1) mwaka huu majira ya saa 1:30 jioni katika Mtaa wa Mateka C Kata ya Mateka Tarafa ya Songea Magharibi.

Taarifa za awali kuhusu mauaji hayo zinaeleza kuwa Eva (20) alikuwa na malumbano na mama yake mzazi , Sofia Mayunga, ambae alikuwa akimuuliza sababu za kushika ujauzito mwingine ili hali ana mtoto mdogo wa umri wa mwaka mmoja na nusu (Catherine Kapinga), inaelezwa kuwa jambo hilo ndilo lilimkasirisha Eva na kuamua kujichoma kisu tumboni.

Kamanda Mwombeji akaongeza kuwa baada ya Eva kujichoma kisu tumboni watu waliokuwa jirani walimkimbiza kwenye Hospitali ya Mkoa na taarifa za tukio hilo zikafikishwa polisi ambapo askari walifika eneo la tukio wakiwa wameongozana na mganga, na kwa bahati mbaya walimkuta mtoto Catherine ameshafariki dunia, hivyo walikwenda Hospitali ya Mkoa ambako Eva alikuwa amelazwa akiwa na hali mbaya ambapo aliendelea kulazwa chini ya ulinzi.


Kamanda Mwombeji amesema wanaendelea na uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi utakapo kamilika mtuhumiwa Eva atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni