Jumatatu, 11 Januari 2016
KAMANDA wa Polisi mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari aeleza mazingira yaliyopelekea bw.John Jeremiah (45) na Mwanae Patrick kupoteza maisha kwa kushambuliwa na simba
KAMANDA wa Polisi mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari ameasa wakulima na wafugaji wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Katavi wilayani Mlele, wanakuwa na makazi imara na salama dhidi ya wanyamapori.
Alisema kutokuwa na makazi imara na salama kumesababisha vifo vya mkazi wa kijiji cha Sitalike wilayani Mlele, John Jeremiah (45) na mwanawe Patrick John (5).
“Endapo familia ya marehemu Jeremiah ingekuwa na nyumba imara ya kuishi , yeye (Jeremiah ) na mwanawe Patrick wasingeuawa na simba,” alisema.
Akisimulia mkasa huo, Kidavashari alisema kuwa katika kitongoji cha Makaburi Wazi , kijiji cha Sitalike wilayani Mlele, Jeremiah na mwanawe Patrick waliuawa kwa kushambuliwa na simba .
Alisema tukio hilo ni la Januari 4 , mwaka huu saa 3:00 usiku katika kitongoji cha Makaburi Wazi kijijini Sitalike ambapo simba jike mzee aliwashambulia na kumuua baba huyo na mwanawe.
Simba huyo alifika katika nyumba ya Jeremiah ambayo ni kambi ya muda kwa ajili ya uangalizi wa mashamba na kuanza kushambulia kuku wawili, kisha aliingia ndani na kumshambulia vibaya Jeremiah sehemu za siri, shingoni na kichwani.
“Licha ya kupiga kelele za kuomba msaada ambazo ziliweza kusikika kwa majirani lakini hakupata msaada wa haraka,” alisema.
Kamanda alisema, simba huyo alimnyakua mtoto Patrick na kumburuza hadi vichakani na kuanza kumla kiwiliwili chake chote na kubakiza kichwa na mikono.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni