Jumamosi, 23 Januari 2016

RAIS MAGUFULI ASEMA ATALITUMIA JESHI LA WANANCHI TANZANIA KATIKA KUJENGA UCHUMI




Rais Magufuli (kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Davis Mwamunyange wakati wa ufungaji wa zoezi la Onesha Uwezo Medani lililofanyika Monduli nje kidogo ya Jiji la Arusha jana.




Rais Magufuli akijadiliana jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Davis Mwamunyange wakati akielekea kupewa maelezo ya zoezi zima la Onesha Uwezo Medani.



Rais Magufuli akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi katika tukio hilo la Ufungaji.



Rais Magufuli akielekea kwenye uwanja wa maonesho akiwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Davis Mwamunyange.



Rais Magufuli akipewa maelezo ya zana mojawapo ya Kivita katika Zoezi la Onesha Uwezo Medani Mkoani Arusha. Picha na IKULU



Rais Magufuli (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi mara baada ya kufunga zoezi la Onesha Uwezo Medani Monduli Mkoani Arusha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunga “Zoezi la Onesha Uwezo Medani” lililoandaliwa na kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ambalo ni sehemu ya Jeshi la wananchi Tanzania katika eneo la Lang’arurusu nje kidogo ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.


Akizungumza na Askari na Maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania kabla ya kufunga zoezi hilo, Rais Magufuli amesema katika awamu yake ya tano ya uongozi amedhamiria kulitumia Jeshi la wananchi Tanzania katika kujenga uchumi, ikiwemo kuanzisha viwanda na kampuni za ujenzi ili kuharakisha maendeleo.


Ametoa mfano wa kiwanda cha Nyumbu ambacho kipo chini ya jeshi la wananchi Tanzania na kueleza kuwa wakati umefika wa kukiimarisha na kukiendeleza kiwanda hicho, ili kiweze kufanya uzalishaji mkubwa kwa manufaa ya nchi ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.


“Zipo nchi nyingi ambazo majeshi yao yanatumika katika uchumi na yanafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano, wakati umefika na sisi kufanya hivyo. Hata hizi sare za jeshi na viatu, hatuna sababu ya kuvinunua kutoka nje ya nchi, tunaweza kutengeneza sisi wenyewe” Alisisitiza Rais Magufuli.


Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuandaa “Zoezi Onesha Uwezo Medani” ambalo limethibitisha uwezo, weledi na utayari lilionao katika jukumu lake la kiulinzi.


Ameahidi kuwa ataendeleza juhudi zilizofanywa na viongozi wenzake waliotangulia za kuliimarisha kwa vitendea kazi na maslai ya wanajeshi ili liweze kutekeleza wajibu wake bila vikwazo.


Pamoja na kuwapongeza Askari na maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania walioshiriki katika zoezi hilo, Rais Magufuli ameagiza Askari Mgambo na Askari wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) walioshiriki zoezi hilo kuajiriwa na jeshi la wananchi Tanzania.


Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Wizara yake itaongeza na kusimamia juhudi za kuliboresha jeshi hilo kwa zana, vifaa na maslai kwa wanajeshi ili kuwajengea uwezo na morali ya kutekeleza majukumu yao ya kuilinda nchi, pamoja na kutoa msaada stahiki kwa nchi zenye kuhitaji ulinzi wa amani popote duniani.


Kwa upande wake Mkuu wa majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Jeshi la wananchi Tanzania lipo imara na litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, nidhamu ya hali ya juu na uzalendo mkubwa.


Kabla ya kuwahutubia maafisa wa jeshi la wananchi, Askari na wananchi waliohudhuria ufungaji wa “Zoezi Onesha Uwezo Medani”, Rais Magufuli ameoneshwa zana mbalimbali za kivita ikiwa ni pamoja na kushuhudia upigaji wa mizinga ya masafa mafupi, masafa ya kati na masafa marefu.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
22 Januari, 2016

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni