TAMKO LA
MHE. UMMY MWALIMU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWA
VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADILI YA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI. TAREHE O4 MACHI 2016
Ndugu Wanahabari,
Nachukua fursa hii kutoa maelezo
machache kuhusu maadili katika utoaji wa huduma za afya nchini:
Katika uhai wa mwanadamu, kuna kipindi
kimoja au kingine hupatwa na ugonjwa, na ana haki ya kupata matibabu. Hapa
kwetu Tanzania tuna Sera, taratibu, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali
ambayo tumejiwekea ili kuhakikisha haki hiyo inapatikana kwa watanzania wote. Katika
utoaji wa huduma ya afya nchini, tunavyo vituo 7,247 vya umma na binafsi katika
ngazi mbalimbali, vyenye kuhudumiwa na wataalam wa afya wa kada na ngazi
tofauti.
Nachukua fursa hii kwanza kabisa kuwapongeza watoa huduma wote ambao wanafanya kazi zao
kwa ufanisi, upendo na uadilifu. Wengi wanatumia muda wa ziada kuendelea kuwahudumia wagonjwa hadi wanapoona wapo
salama. Napenda kuwashukuru na kuwatia moyo waendelee kuwa na tabia hiyo nzuri,
kwa maslahi ya Taifa letu.
Ndugu
Wanahabari,
Katika utoaji wa huduma za afya, yapo
maadili ambayo mtoaji huduma anapaswa kuyajua na kuyazingatia. Maadili hayo ni
kama ifuatavyo:
Faragha:
- Mtoa
huduma wa afya anapaswa kuongea na mgonjwa au ndugu wa mgonjwa kwa lugha ya
upole, yenye maelekezo na faraja. Aepuke maneno makali kwa mgonjwa.
- Kutomshika
mgonjwa mwili wake bila ridhaa yake.
Uaminifu:
- Mtoa
huduma anatakiwa kumheshimu mgonjwa na kumsikiliza kwa makini pale anapomueleza
tatizo lake.
- Mtoa
huduma asimtoze mgonjwa gharama zisizostahili na kama kuna gharama zozote
zilipwe sehemu husika ya kupokelea fedha.
- Asiongeze
gharama za matibabu tofauti na ile iliyotajwa kwenye miongozo husika.
- Inapotokea
mgonjwa anadhurika na dawa aliyopewa na daktari, daktari yule anapaswa
kumtaarifu mgonjwa, na kuchukua hatua zinazostahili.
Usawa:
- Mtoa
huduma wa afya anapaswa kutoa huduma kwa usawa bila kuangalia mwenye uwezo wa
kifedha au asiye na uwezo wa kifedha, Imani, jinsia, ukabila na umri.
- Mtoa
huduma wa afya anapaswa kutoa maelezo ya kitu/hatua gani zitafanywa na kutoa
majibu na maoni ya vipimo vilivyochukuliwa.
- Mtoa
huduma wa afya pia anapaswa kumpa mgonjwa msaada wowote wa kimatibabu wakati
wowote anapohitaji.
Usiri:
- Mtoa
huduma lazima ahifadhi siri za mgonjwa na kulinda usalama wa taarifa za mgonjwa.
- Anatakiwa
kutumia ushauri wa kitaaluma katika kutoa maamuzi ya mgonjwa.
Uhusiano:
- Mtoa
huduma wa afya anapaswa kumthamini mgonjwa kama anavyojithamini yeye mwenyewe.
- Mtoa
huduma wa afya anapaswa kuwa na uhusiano mzuri na watumishi wenzake, anapaswa
kuhakikisha kuwa watumishi wengine walio sehemu yake ya kazi wanawahudumia
wagonjwa inavyostahili.
- Mtoa
huduma wa afya anapaswa kuipa kipaumbele afya ya mgonjwa anapotoa huduma.
- Aidha
mtoa huduma wa afya anapaswa kuyajua, kuonya na kusahihisha mapungufu
yanayotokea katika sehemu yake ya kazi.
- Mtoa
huduma wa afya anatakiwa kuzingatia kiapo cha taaluma yake katika utekelezaji
wa majukumu yake ya kazi ya kila siku.
Kwa
tamko hili ninawaasa na kuwaagiza watoa huduma wa afya wote nchini kufanya kazi
zao kwa bidii na kwa kuzingatia weledi na maadili ya kitaaluma kama
inavyoelekezwa. Ninasikitishwa sana sana na tabia ya watumishi wachache ambao
wanafanyakazi kinyume na maadili ya taaluma zao. Tumezisikia wote taarifa mbaya
kutoka Geita, Mtwara, Nyamagana, Temeke na kwingineko ambazo wagonjwa au ndugu
wa wagonjwa wamekuwa wakihudumiwa vibaya.
Napenda
kusisitiza kuwa Wizara yangu haitavumilia matukio ambayo watumishi wa Sekta ya Afya
watakwenda kinyume na matakwa ya maadili ya Taaluma zao katika vituo vya
kutolea huduma ya afya nchini. Hivyo hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa
mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kudhibiti hali hii.
Nimeshaelekeza
vyombo vya kusimamia maadili ya watoa huduma za afya nchini, yaani Baraza la
Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC)
kuchukua hatua mara moja juu ya watoa huduma wote wanaotuhumiwa ikiwemo wa
Mtwara, Temeke na Nyamagana. Endapo tuhuma zao zitathibitika, hatua stahiki
zitachukuliwa dhidi ya mhusika ikiwemo kufutiwa usajili au leseni zao.
Ni
muhimu pia nikakumbusha kwamba kazi hii ya usimamizi wa
maadili katika vituo vya kazi itafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja wa Wakuu wa
Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala pamoja na Wakurugenzi katika kuwasimamia,
kuwaelekeza na kutambua mapungufu yaliyopo na kuchukua hatua zinazostahili.
Tufanye
kazi kwa pamoja ili kutekeleza kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
inayosema ‘HAPA KAZI TU’.
Asanteni
sana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni