Jumapili, 6 Machi 2016
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADILI YA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI. TAREHE O4 MACHI 2016
Ndugu Wanahabari,
Nachukua fursa hii kutoa maelezo machache kuhusu maadili katika utoaji wa huduma za afya nchini:
Katika uhai wa mwanadamu, kuna kipindi kimoja au kingine hupatwa na ugonjwa, na ana haki ya kupata matibabu. Hapa kwetu Tanzania tuna Sera, taratibu, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali ambayo tumejiwekea ili kuhakikisha haki hiyo inapatikana kwa watanzania wote. Katika utoaji wa huduma ya afya nchini, tunavyo vituo 7,247 vya umma na binafsi katika ngazi mbalimbali, vyenye kuhudumiwa na wataalam wa afya wa kada na ngazi tofauti.
Nachukua fursa hii kwanza kabisa kuwapongeza watoa huduma wote ambao wanafanya kazi zao kwa ufanisi, upendo na uadilifu. Wengi wanatumia muda wa ziada kuendelea kuwahudumia wagonjwa hadi wanapoona wapo salama. Napenda kuwashukuru na kuwatia moyo waendelee kuwa na tabia hiyo nzuri, kwa maslahi ya Taifa letu.
Ndugu Wanahabari,
Katika utoaji wa huduma za afya, yapo maadili ambayo mtoaji huduma anapaswa kuyajua na kuyazingatia. Maadili hayo ni kama ifuatavyo:
Faragha:
Mtoa huduma wa afya anapaswa kuongea na mgonjwa au ndugu wa mgonjwa kwa lugha ya upole, yenye maelekezo na faraja. Aepuke maneno makali kwa mgonjwa.
Kutomshika mgonjwa mwili wake bila ridhaa yake.
Uaminifu:
Mtoa huduma anatakiwa kumheshimu mgonjwa na kumsikiliza kwa makini pale anapomueleza tatizo lake.
Mtoa huduma asimtoze mgonjwa gharama zisizostahili na kama kuna gharama zozote zilipwe sehemu husika ya kupokelea fedha.
Asiongeze gharama za matibabu tofauti na ile iliyotajwa kwenye miongozo husika.
Inapotokea mgonjwa anadhurika na dawa aliyopewa na daktari, daktari yule anapaswa kumtaarifu mgonjwa, na kuchukua hatua zinazostahili.
Usawa:
Mtoa huduma wa afya anapaswa kutoa huduma kwa usawa bila kuangalia mwenye uwezo wa kifedha au asiye na uwezo wa kifedha, Imani, jinsia, ukabila na umri.
Mtoa huduma wa afya anapaswa kutoa maelezo ya kitu/hatua gani zitafanywa na kutoa majibu na maoni ya vipimo vilivyochukuliwa.
Mtoa huduma wa afya pia anapaswa kumpa mgonjwa msaada wowote wa kimatibabu wakati wowote anapohitaji.
Usiri:
Mtoa huduma lazima ahifadhi siri za mgonjwa na kulinda usalama wa taarifa za mgonjwa.
Anatakiwa kutumia ushauri wa kitaaluma katika kutoa maamuzi ya mgonjwa.
Uhusiano:
Mtoa huduma wa afya anapaswa kumthamini mgonjwa kama anavyojithamini yeye mwenyewe.
Mtoa huduma wa afya anapaswa kuwa na uhusiano mzuri na watumishi wenzake, anapaswa kuhakikisha kuwa watumishi wengine walio sehemu yake ya kazi wanawahudumia wagonjwa inavyostahili.
Mtoa huduma wa afya anapaswa kuipa kipaumbele afya ya mgonjwa anapotoa huduma.
Aidha mtoa huduma wa afya anapaswa kuyajua, kuonya na kusahihisha mapungufu yanayotokea katika sehemu yake ya kazi.
Mtoa huduma wa afya anatakiwa kuzingatia kiapo cha taaluma yake katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi ya kila siku.
Kwa tamko hili ninawaasa na kuwaagiza watoa huduma wa afya wote nchini kufanya kazi zao kwa bidii na kwa kuzingatia weledi na maadili ya kitaaluma kama inavyoelekezwa. Ninasikitishwa sana sana na tabia ya watumishi wachache ambao wanafanyakazi kinyume na maadili ya taaluma zao. Tumezisikia wote taarifa mbaya kutoka Geita, Mtwara, Nyamagana, Temeke na kwingineko ambazo wagonjwa au ndugu wa wagonjwa wamekuwa wakihudumiwa vibaya.
Napenda kusisitiza kuwa Wizara yangu haitavumilia matukio ambayo watumishi wa Sekta ya Afya watakwenda kinyume na matakwa ya maadili ya Taaluma zao katika vituo vya kutolea huduma ya afya nchini. Hivyo hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kudhibiti hali hii.
Nimeshaelekeza vyombo vya kusimamia maadili ya watoa huduma za afya nchini, yaani Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) kuchukua hatua mara moja juu ya watoa huduma wote wanaotuhumiwa ikiwemo wa Mtwara, Temeke na Nyamagana. Endapo tuhuma zao zitathibitika, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya mhusika ikiwemo kufutiwa usajili au leseni zao.
Ni muhimu pia nikakumbusha kwamba kazi hii ya usimamizi wa maadili katika vituo vya kazi itafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala pamoja na Wakurugenzi katika kuwasimamia, kuwaelekeza na kutambua mapungufu yaliyopo na kuchukua hatua zinazostahili.
Tufanye kazi kwa pamoja ili kutekeleza kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli inayosema ‘HAPA KAZI TU’.
Asanteni sana.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni