Katika
kuelekea kusheherekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani,Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Mh.Ummy Mwalimu , jana kwenye
taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo hospitali ya Taifa Muhimbili, amejitolea
kuwasomesha watoto wawili wa kike Zahara Selemani kutoka Meru na Beatrice Alfredy kutoka Karatu,waliolazwa hospitalini hapo kusubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo,
Mh. Ummy alichukua jukumu
hilo wakati akipokea msaada wa shilingi milioni 222,200,000 kutoka taasisi ya
Baps Charities.
Kaulimbiu ya maadhimisho
mwaka huu inasema "50-50 ifikapo 2030;Tuongeze Jitihada"
Wiziri Ummy amebainisha
kuwa, kiasi cha msaada unaotolewa utawezesha wagonjwa kupatiwa matibabu ya moyo
hivyo kuwa, faraja kubwa kwa wagonjwa waliokuwa wakisubiria huduma hizo
kwa muda mrefu kutokana na kushindwa gharama za matibabu yake.
Aidha, kwa upande wake,
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amepongeza kwa msaada
huo kwani utasaidia kutoa matibabu kwa watoto hao 101, huku pia taaisi yake
ikikabiliwa na changamoto ya wagonjwa wengi ambapo amezitaka taasisi na wadau wengine
kujitokeza kuchangia ilikupunguza wagonjwa wanaosubiria kupatiwa matibabu hasa
upasuaji.
Prof. Janabi
ameeleza kuwa, matibabu ya wagonjwa wa moyo yana gharama kubwa kwani kwa mtoto
mmoja ndani ya nchi yanafikia hadi Milioni nne (Mil 4) huku kwa nje ya nchi
matibabu hayo yakifikia hadi Milioni 16, gharama hizo ni kubwa hivyo
wadau na taasisi binafsi zimeombwa kujitokeza ilikuokoa maisha ya wagonjwa
wengi hasa watoto ambao wapo katika taasisi hiyo na mikoa mingine
|
Waziri Ummy Mwalimu apokea msaada wa fedha wa zaidi ya Mil 220, kwa matibabu ya
wagonjwa wa moyo |
|
Mh. Waziri, Ummy Mwalimu akimsalimia miongoni mwa watoto wanao subiri kupatiwa matibabu katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo hospitali ya Taifa Muhimbili, |
|
Zahara Selemani (10) kutoka Meru akifurahi baada ya kuahidiwa kusomeshwa |
|
Mtoto Beatrice Alfred (13) mkazi
wa karatu na mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi sumaye akilia kwa furaha baada ya waziri Ummy Mwalimu kujitolea kumsomesha |
|
Baadhi ya wazazi na wakiwa na watoto wanaosubiri kupatiwa matibabu ya upasuaji wa moyo katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo hospitali ya muhimbili |
|
Mama mzazi wa mtoto Beatrice akilia baada ya kupata msaada wa kusaidiwa kusomeshewa mtoto huku akiwa na uhakika wa mwanae kupatiwa matibabu ya upasuaji wa Moyo.
*********************************
WIZARA YA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO TAARIFA KWA UMMA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI:8 MACHI, 2016
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto inawataarifu wananchi wote kuwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Wanawake, hutoa fursa kwa Serikali, wananchi, wadau, na wanawake wenyewe kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.
Siku ya wanawake Duniani husisitiza kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani, kuhamasisha jamii kutafakari kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake ya kila mwaka; kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na asasi mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kuwaendeleza wanawake; na kuhamasisha jamii kuhusu utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya Serikali yenye lengo la kudumisha Amani, Usawa na Maendeleo.
Kaulimbiu ya kitaifa ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2016 inasema “50 – 50 Ifikapo 2030; Tuongeze Jitihada”.
Kaulimbiu hii inasisitiza kuwa na mikakati thabiti yenye mwelekeo wa kufikia Agenda 2030 ya malengo inayohimiza kufikia asilimia 50 kwa 50 ya ushiriki wa wanawake na wasichana katika nyanja zote za maendeleo.
Kuanzia mwaka 2005 Serikali ilipitisha uamuzi kuwa, maadhimisho haya yafanyike Kitaifa kila baada ya miaka mitano kutoa muda wa utekelezaji wa maazimio na kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano ambapo Mwaka 2015 Maadhimisho yalifanyika Kitaifa mkoani wa Morogoro.
Kwa mwaka 2106, mikoa yote itaadhimisha siku hii katika maeneo yao kwa kuzingatia hali na mazingira ya mikoa husika. Kwa mfano mkoa wa Dar es salaam, utaadhimisha siku hii katika Manispaa ya Kinondoni.
Wizara inatoa wito kwa mikoa yote kuhamasisha wananchi na wadau wote kushiriki maadhimisho ya siku hii adhimu na kuzingatia ujumbe wa kauli mbiu ya mwaka 2016.
Rai imetolewa kwa wadau wote kuwa, tuunge mkono jitihada za Serikali katika kutoa haki na ushiriki sawa katika fursa za uongozi wa kisiasa na kiuchumi; na kupima mafanikio yaliyofikiwa na kuweka mipango yenye matokeo makubwa, na kubainisha shuhuda za wanawake waliotoa mchango uliotukuka katika kuwezesha maendeleo ya wanawake na taifa kwa ujumla. Nashauri wanahabari wote kuelimisha jamii kuhusu kaulimbiu ya Siku ya Wanawake kwa mwaka 2016 ili kila mwananchi aweze kutambua jukumu alionalo katika kufikia lengo la ushiriki sawa wa wanawake na wasichana katika uchumi; afya, elimu, ajira, sheria na siasa ifikapo mwaka 2030.
Nawatakia mafanikio mema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu. Sihaba Nkinga KATIBU MKUU 3/3/2016
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni