JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA
AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA
MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO, TAREHE 29 MACHI, 2016
Ndugu wanahabari,
Wizara yangu imejiwekea utaratibu wa kutoa taarifa
kila wiki kwa umma kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu nchini pamoja na
kueleza juhudi mbalimbali za kuudhibiti zinazoendelea kuchukuliwa. Ugonjwa wa
kipindupindu umedumu hapa nchini kwa takribani miezi saba (7) sasa tangu uanze
mnamo mwezi Agosti, 2015 ambapo hadi kufikia tarehe 27 Machi 2016, jumla ya
watu 19,815 wameugua ugonjwa huo, na
kati yao watu 312 wamepoteza maisha.
Takwimu za wiki iliyopita
kuanzia tarehe 21 hadi 27 Machi 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa
kipindupindu imepungua ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa wiki hiyo
ni 685 ikilinganishwa na 738 wa wiki iliyotangulia. (Machi
14 hadi 20, 2016) ambapo ni punguzo kwa asilimia 7.2. Idadi ya vifo imepungua sana toka 16 wiki iliyotangulia hadi 4
wiki iliyopita, sawa na asilimia 75.
Mikoa ambayo bado imeendelea kuripoti ugonjwa wa kipindupindu ni 13. Mikoa iliyopata wagonjwa wengi
zaidi ni Kilimanjaro (162), Geita
(97), Manyara (88), Mwanza (74) na Iringa (60).
Hadi
sasa, mikoa ya Njombe na Ruvuma haijaripoti
kuwa na mgonjwa wa Kipindupindu.
Ndugu wanahabari,
Wakati tunasubiri kipindi
cha Masika kianze wakati wowote, tunaashiria ongezeko la ugonjwa ya Kipindupindu
iwapo wananchi hawatazingatia kanuni za usafi binafsi na mazingira. Hivyo basi,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea
kusisitiza kuwa udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu unahitaji juhudi kubwa zaidi
ya wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali hususan wakati tunaelekea kipindi
hiki cha masika.
Aidha Wizara inapenda
kutoa pongezi kwa Mikoa na Wilaya zinazoendelea kutoa taarifa sahihi na kwa
wakati pamoja na juhudi za kudhibiti ugonjwa huu. Ninaendelea kusisitiza kuwa
ni lazima kwa Mikoa na Wilaya kutoa taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu
kwa kuzingatia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ujulikanao kama “Integrated
Disease Surveillance and Response (IDSR)”, ambao unasimamiwa na Waganga Wakuu
wa Mikoa na Wilaya. Utoaji wa taarifa sahihi na kamili (ikiwa pamoja na
linelist) kwa wakati utasaidia kuweka mikakati ya upesi ya kudhibiti ugonjwa
huu usisambae kwa kasi na kuleta madhara zaidi. Hii pia inaambatana na
uchukuaji wa sampuli za wagonjwa kwa vipimo kama mwongozo unavyosema ili kuweza
kudhibiti ugonjwa huu kwa wakati muafaka.
Ndugu wanahabari,
Kufuatia tahadhari niliyotoa kwa
mikoa yote nchini kwa Waganga Wakuu wa Mikoa kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Homa ya
Manjano nchini Angola na kuweka mipango thabiti ya utambuzi, wiki hii
iliyopita, wataalam wetu waliweza kutambua wagonjwa wawili (2) ambao
walionyesha kuwa na dalili za kutokwa damu katika sehemu za uwazi na kufariki
dunia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Aidha vipimo vya wagonjwa hawa wawili
vilichukuliwa na kudhibitishwa kuwa hawakuwa na ugonjwa wa Ebola au Homa ya
Manjano. Taratibu za mazishi zilifuatwa
kuzingatia miongozo ya Kitaifa. Hadi leo tarehe 29 Machi 2016, Wizara
inafuatilia watu 55 waliokuwa karibu na wagonjwa hawa na hadi sasa hakuna mtu yeyote
ambaye ameonyesha dalili kama za wagonjwa waliokwisha kufariki. Watu hawa
watafuatiliwa kwa takribani siku 21 kama taratibu za magonjwa ya milipuko ya
aina hii zinazoelekeza.
Ndugu wanahabari,
Nahimiza yafuatayo yazingatiwe katika
kudhibiti magonjwa ya milipuko;
1. Utoaji wa taarifa mapema katika vituo
vya kutolea huduma za afya pale wanapoona wagonjwa wana dalili za magonjwa ya milipuko
2. Kutilia mkazo usafi wa mazingira kwa
ujumla
3. Watumishi wa afya waendeelee kutoa elimu kwa
wananchi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu na jinsi ya kujiepusha kupata
maambukizi.
4.Ngazi mbalimbali ziendelee kuchukua
tahadhari (Preparedness) kwa magonjwa haya.
Hitimisho
Wizara inaendelea kutoa wito kwa
wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika jitihada za
kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu. Aidha, Wizara inaendelea kuwashukuru wataalamu
wa sekta husika, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja
waandishi wa habari na wananchi kwa
ujumla kwa kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa
Kipindupindu.
Asanteni sana
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni