JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO LA
MHE. UMMY MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO KUHUSU WANANCHI KUSHAMBULIA WATUMISHI WA AFYA HASA MADAKTARI NA WAUGUZI
KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI, TAREHE 29MACHI, 2016
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii nikiwa Waziri mwenye dhamana
ya masuala ya afya nchini, kutoa tamko kuhusiana na matukio ya hivi karibuni yaliyo
ripotiwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusiana na vitendo vya
kusikitisha wanavyo fanyiwa watumishi wa sekta ya afya, wakiwemo Madaktari kama
vile kushambuliwa kwa maneno na vipigo. Pasi na shaka, vitendo hivyo vita athiri
upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wanao pewa huduma hizo hususani
wa kipato cha chini.
Matukio haya yana jumuisha tukio lililotokea
tarehe 27.03.2016 katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, ambapo Dr Dickson
Sahini alishambuliwa na ndugu wa mgonjwa aliyepelekwa hapo kuhudumiwa.
Napenda kutamka kwamba nimesikitishwa sana
na tukio hilo, na nina laani vikali matukio ya watumishi wa afya kushambuliwa kwa
maneno au kwa vitendo na wananchi wanao patiwa huduma. Jambo hili likiendelea litawavunja
moyo watumishi wa afya na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ningependa kuwa fahamisha kwamba kwa ujumla
wake sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi sana katika maeneo ya miundo
mbinu, dawa na vifaa tiba, watumishi wa kutosha, pamoja na kuwa na watumishi wasio
zingatia nidhamu, weledi na maadili katika kutimiza majukumu yao.
Ninatambua kwamba changamoto hizi zipo siku
nyingi, na zimekuwa zikitafutiwa majawabu na Serikali za awamu zilizopita ikiwemo
ile ya awamu ya nne. Lakini sote ni mashahidi kwamba Serikali ya awamu ya tano,
chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dr John Joseph PombeMagufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, inachukua hatua za makusudi katika kutatua changamoto hizi,
likiwemo pia suala zima la utendaji unaozingatia uwajibikaji.
Kwa
hiyo ninawasihi sana wanachi wanaopatiwa huduma katika vituo vyetu vya afya kote
nchini kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mikononi na kufanya vitendo
vinavyoweza kuwakwaza watumishi wa afya.
Kwa
vile nchi yetu inafuata misingi ya utawala unaozingatia sheria, ni vyema wananchi
wakafuata taratibu zilizowekwa wanapohisi kwamba hawakupatiwa huduma za afya wanavyostahili.
Aidha
nachukua fursa hii kuvitaka vyombo na mamlaka husika kuto sita kuwachukulia hatua
wananchi wanaokwenda kinyume na matakwa ya sharia ili kuwahakikishia watoa huduma
za afya usalama na amani wakati wa utoaji wa huduma hiyo.
Nina agiza
vile vile kwamba hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini ziweke
utaratibu mwepesi wa wananchi kufikisha malalamiko yao pindi wanapo ona kwamba hawa
kupatiwa huduma za afya kwa kiwango stahiki.
Napenda
pia kuahidi kwamba tutajitahidi kutatua changamoto za kimfumo zilizopo katika utoaji
wa huduma za afya nchini ili kuufanya utoaji wa huduma kuwa bora zaidi.
Ndugu Wananchi,
Ninatambua kwamba sehemu kubwa ya watumishi
katika sekta ya afya nchini wanafanya kazi zao kwa ufanisi, upendo, uadilifu na
kwa kuzingatia matakwa ya weledi (professionalism) na miiko ya taaluma zao
(ethics). Pia ninatambua kwamba wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na
wanatumia muda wa ziada kuendelea kuwa hudumia wagonjwa hadi wanapoona wapo salama. Nina wapongeza kwa dhati watumishi
hawa na nina washukuru na kuwatia moyo waendelee kuwa na tabia hiyo nzuri, kwa maslahi
ya Taifa letu.
Hata
hivyo ninasikitishwa sana na tabia ya watumishi wa afya wachache ambao wanafanya
kazi kinyume na maadili na matakwa ya weledi wa taaluma zao. Napenda kusisitiza
kuwa Wizara yangu haita vumilia matukio ambayo watumishi wa Sekta ya Afya wata kwenda
kinyume na matakwa ya weledi na maadili ya taaluma zao katika vituo vya kutolea
huduma za afya nchini.
Hivyo hatuta sita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu
wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kudhibiti hali hii.
Nimesha
elekeza vyombo vya kusimamia maadili ya watoa huduma za afya nchini, yaani Baraza
la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la WauguzinaWakunga Tanzania (TNMC)
kuchukua hatua mara moja, kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zao, juu ya watoa huduma
wote wanaotuhumiwa kukiuka misingi ya weledi na maadili ya taaluma zao. Endapo tuhuma
zao zitathibitika, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kufutiwa usajili
au leseni zao ikibidi.
Hivyo
kwa tamko hili nina waasa na kuwa agiza watoa huduma wa afya wote nchini kufanya
kazi zao kwa bidii, kwa nidhamu na kwa kuzingatia weledi na maadili ya kitaaluma
kama inavyoelekezwa.
Ndugu Wananchi,
Napenda
pia kukumbusha kwamba kazi hii ya usimamizi wa mahusiano mema kati ya watoa huduma
za afya na wananchi, na usimamizi wa weledi na maadili katika vituo vya kazi, itafanikiwa
kwa ushirikiano wa pamoja wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi,
Kamati za Usimamiaji wa Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya, Kamati za Usimamiaji
wa Huduma za Afya za Hospitali, na Wananchi wote kwa ujumla katika kuwasimamia,
kuwaelekeza na kutambua mapungufu ya kimfumo au yale yanayo husu watumishi wa afya
yaliyopo na kuchukua hatua zinazo stahili mara moja. Ni lazima tuzingatie Sheria,
Kanunina Taratibu katika kutimiza jukumu hili. Wizara ya Afya itaendelea kuvijengea
uwezo Mabaraza ya kitaaluma ya wataalamu wa afya ili kutimiza
wajibu wao kikamilifu.
Tufanye
kazi kwa pamoja ili kutekeleza kaulimbiu ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli,
inayosema ‘HAPA KAZI TU’.
Asanteni
sana.
Imetolewana:
Mhe.Ummy Mwalimu (Mb)
Waziriwa Afya, Maendeleoya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto
Mtwara –Tanzania
29 Machi 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni