Jumatatu, 14 Machi 2016

viongozi wa dini na watu mashuhuli watakiwa kusaidia kutoa elimu juu ya ugonjwa wa kipindupindu

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

 

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 14 MACHI 2016

Ndugu Waandishi wa Habari,
Taarifa ya wiki kuhusu ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini. Ugonjwa huu umedumu kwa takribani miezi saba (7) sasa tangu uanze mwezi Agosti, 2015.  Hadi kufikia tarehe 13 Machi 2016, jumla ya watu 18,399 wameugua ugonjwa huo, kati yao watu 292 wamepoteza maisha.  Takwimu za ugonjwa huu pia zinaonyesha kuwa mikoa ambayo ilikwishakupata ugonjwa imeongezeka na kufikia 23 baada ya  Mkoa wa Mtwara kuripoti wagonjwa wawili kuanzia jana tarehe 13 Machi 2016,   katika wilaya ya Masasi. Mikoa ya Njombe  na Ruvuma  ndio pekee hapa nchini ambayo bado haijaripoti mgonjwa wa Kipindupindu.

Takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 7 hadi 13 Machi 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imeongezeka ambapo idadi ya wagonjwa walioripotiwa wiki hiyo ni 758 ikilinganishwa na 544 wa wiki iliyotangulia ya tarehe 28 Februari hadi 6 Machi ambapo  ni ongezeko la asilimia  40. Mkoa wa Iringa ambao haukuwa umeripoti wagonjwa wiki iliyotangulia, wiki hii imeripoti wagonjwa katika Halmashauri  ile ile ya  Iringa.  Mikoa ambayo bado imeendelea kuripoti ugonjwa wa kipindupindu pia imeongezeka kutoka 10 hadi 12. Mikoa hiyo  inaongozwa na  Morogoro (196), Dodoma (142), Mwanza(108), Mara(86), Manyara(77), Iringa(77). Mikoa mingine ni pamoja na, Dar es salaam(42),  Mbeya(16), Arusha (10),Lindi (2), Mtwara (2) na Rukwa (2).

Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kusisitiza kuwa udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu ni lazima uwe endelevu na ushirikishe viongozi wa ngazi zote kuanzia ngazi ya chini ya kijiji kwa kushirikisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii, serikali za mitaa, afisa watendaji hadi ngazi ya Wilaya na Mkoa. Tumeshashuhudia kuwa ushirikishwaji huu umeweza kufanikisha kwa kiasi kikubwa udhibiti wa ugonjwa huu kwa baadhi ya Mikoa ambako tumeona idadi ya wagonjwa imeweza kupungua.  Aidha Wizara inapenda kutoa pongezi kwa Mikoa na Wilaya zinazoendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati. Vile vile ninaendelea kusisitiza kuwa ni lazima kwa Mikoa na Wilaya kutoa taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu kwa kuzingatia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ujulikanao kama “Integrated Disease Surveillance and Response (IDSR)”, ambao unasimamiwa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati utasaidia kuweka mikakati ya upesi ya kudhibiti ugonjwa huu usisambae kwa kasi na kuleta madhara zaidi.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara inaendelea kutia msisitizo kwa jamii, Mikoa pamoja na Halmashauri, kuendelea na juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
§  Kuhakikisha kuwa jamii inapata elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu ili iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini na watu mashuhuri watusaidie kuhamasisha jamii zao kuhusu ugonjwa huu
§  Kuhakikisha kuwa jamii ina uelewa wa kupata matibabu mapema katika vituo vya kutolea huduma. Aidha Mikoa, pamoja na Halmashauri ihakikishe upatikanaji wa chumvi chumvi za kuweka kwenye maji (ORS). Hii ikiwa ni moja ya matibabu ya awali ambapo mgonjwa mwenye dalili za Kipindupindu anasisitizwa atumie maji yaliyochanganywa na ORS wakati akiwa anapelekwa katika kituo cha kutolea huduma. Tumeshuhudia vifo vingi vinatokea katika jamii kabla ya kufika Kituo cha Kutolea huduma ambavyo vingeepukika iwapo matumizi ya sahihi ya ORS katika ngazi ya jamii yangefanyika
§  Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia Mamlaka za maji zilizopo katika ngazi zote
§  Kuhakikisha utunzaji salama wa maji ya kunywa yaliyotibiwa
§  Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yote ya mijini na vijijini ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kutokana na kudumu na kuongezeka kwa kasi ya ugonjwa huu hapa nchini Wizara yangu imeweka mikakati zaidi ikiwa ni pamoja na kupeleka ombi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu la kutaka kuitisha mkutano wa Kamati ya Dharura ya Taifa ambayo inajumuisha Makatibu Wakuu wote ili suala hili la Kipindupindu liweze kujadiliwa Kitaifa kwa Upana zaidi hasa kwa kuzingatia hali ya sasa ya mvua. Lengo ni kuimarisha mikakati  ya pamoja ya Kitaifa.

Hitimisho
Wizara inatoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika jitihada za kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu. Aidha, Wizara inaendelea kuwashukuru wataalamu wa sekta husika, Mashirika ya Kimataifa, watumishi, mikoa na Halmashauri pamoja waandishi wa habari kwa kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.


Asanteni sana,



##################################################

Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa msisitizo, kwa halimashauri,  viongozi wa dini na watu mashuhuri wasaidie kutoa elimu sahihi juu ugonjwa wa kipindupindu ili iweze kuacha imani potofu kuhusu sababu mbalimbali zinazosababisha ugonjwa huo.

Aidha wizara hiyo imesema kwamba udhibiti wa ugonjwa huo ni lazima uwe endelevu na ushirikishe viongozi wa ngazi zote kuanzia ngazi ya chini ya kijiji kwa kushirikisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii,Serikali za mitaa,afisa watendaji hadi ngazi ya wilaya na mkoa kwa kuwa unasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa kwenye baadhi mikoa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo,John Michael wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dares Salaam.

“Kuhakikisha kuwa jamii ina uelewa wa kupata matibabu mapema katika vituo vya kutolea huduma. Aidha mikoa pamoja na halimshauri ihakikishe upatikanaji wa  chumvi chumvi za kuweka kwenye maji(ORS).Hii ikiwa ni moja ya matibabu ya awali  ambapo mgonjwa mwenye dalili za kipindupindu anasisitizwa atumie maji yaliyochanganywa na ORS wakati anapelekwa katika kituo  cha kutolea huduma.

“Tumeshuhudia vifo vingi vinatokea katika jamii kabla ya kufika kituo cha kutolea huduma ambavyo vingeepukika iwapo matumizi ya ORS katika ngazi ya jamii yangefanyika,” alisisitiza.

Aliyataja mambo ambayo yanaweza kusaidia kuwa ni upatikanaji wa maji safi na salama kupitia mamlaka za maji zilizopo katika ngazi zote, kuhakikisha utunzaji salama wa maji ya kunywa yaliyotibiwa na kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yote ya mijini na vijijini ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu.

Aliongeza kwamba kutokana na kudumu na kuongezeka kwa kasi ya ugonjwa huu hapa nchini wizara yangu imeweka mikakati zaidi ikiwa ni pamoja na kupeleka ombi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu la kutaka kuitisha mkutano wa kamati ya dharura ya taifa ambayo inajumuisha makatibu wakuu wote ili suala hili liweze kujadiliwa kitaifa kwa upana zaidi hasa kwa kuzingatia hali ya sasa ya mvua. Lengo ni kuimarisha  mikakati ya pamoja ya kitaifa.

Kaimu Katibu Mkuu huyo aliongeza kwamba kwa mujibu wa takwimu za wiki iliyopita, kuanzia Machi 7 hadi Machi 13 2016 zinaonyesha kuwa ,kasi ya ugonjwa  hu alisema idadi ya wagonjwa waliopotiwa wiki hiyo ni 758 ikilinganishwa na 544 wa wiki iliyotangualia Februari 28 hadi  Machi  6, mwaka huu.


Aliitaja mikoa iliyoathirika na ugonjwa huo, Morogoro 196, Dodoma142, Mwanza,108, Mara 86, Manyara 77, Iringa 77, Dares Salaam 42, Mbeya, Mbeya, 16, Arusha 10 na Lindi 2, Mtwara 2 na Rukwa 2

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni