Jumapili, 24 Aprili 2016

Baada ya kumfanyia Ndivyo Sivyo Muandishi wa Habari wa Chanel Ten leo hii, RCO aomba kuitishwe kikao kati ya Waandishi wa habari na Polisi Mkoani Rukwa

Muandishi wa habari kituo cha Chanel Ten Rukwa Bw. Wilbroad Sumia, akielezea kilicho mtokea leo hii asubuhi kati yake na kiongozi wa msafara wa polisi wakati akitekeleza majukumu yake katika eneo la tukio, eneo la Malangali Mkoani Rukwa ambako kulikua na maiti ya mwanamke ambae inasadikika kuwa ameuawa baada ya kubakwa,

Wilbroad Sumia - Muandishi wa habari,Channel Ten Rukwa
Leo asubuhi saa 11;45 nilipigiwa simu na Mwandishi mwenzetu Peti Siame akanimbia kuwa eneo la Malangali kuna maiti ya mwanamke imekutwa na inasadikika kuwa ameuawa baada ya kubakwa, niende kufanya coverage.

Nilikimbia na gari yangu hadi eneo la tukui nikamkuta katibu wa Rukwa Press Club, Crisencia Daimon, muda huo huo polisi walifika na gari yao.

Aliyekuwa kiongozi wa msafara aliniuliza kama nani kaniruhusu kupiga picha nikamjibu kuwa mimi ni mwandishi wa habari, akaniamuru nimpe camera nikagoma akatumia nguvu kupora camera nikamzuia akatoa amri kwa askari wengine kuwa wanikamate waniweke kwenye Gari.

Walikuja askari wawili wakiwa na SMG wakataka kunikamata nikawagomea nikawaambia wakitaka tuelewane watoa amri wanayotaka nitatii siyo kunigusa, wakanielewa wakaniamuru nipande kwenye Gari yao nikaenda kwenye Gari ya polisi nikapanda chini ya ulinzi.

Muda wa kuondoka yule kiongozi wa msafara wa polisi nilisikia wakimuita Juli… alikuja akaniamuru nimkabudhi vifaa vyangu vya kazi simu na camera nikatii nikampatia simu mbili na camera, Muda huo katibu wetu wa Press alitumia nguvu ya ziada kumuelekeza aache kunifanyia uhuni lakini huyo Juli hakusikia na kuendelea kutoa lugha chafu.

Baada ya kuchukua vifaa aliniuliza kama nimefika pale kwa usafiri gani nikamuambia kuwa nimefika kwa Gari yangu akamuamuru askari mmoja aende na mimi katika Gari yangu ili twende kituo cha polisi kati hapa Sumbawanga.

Nimeendesha mwenyewe Gari yangu tulipofika kituo cha polisi yule askari akaniomba kuwa tusiingie kituoni bali twende katika ofisi ya RCO Rukwa. Nimefika pale kwa RCO nikaambiwa nikae kiti cha wageni hadi alipofika yule aliyeamuru niwekwe chini ya ulinzi akaingia ndani wakawa wanajadili na RCO Bukumbi na muda huo alikuja KATIBU na Mwenyekiti wa Press wakiambatana na mwanachma mwenzetu wa Press Bwana Aidani Makombe.

Tuliitwa ndani tukaingia wote kwa RCO tukapewa viti lakini hatuulizwa chochote na badala yake RCO alitoa kitabu cha wageni akaomba tusaini na akawa anaeleza yeye RCO kuwa kilichotokea ni kutofahamiana tu tusipaniki kwa sababu waandishi wengi hatuna vitambulisho nikatoa kitambulisho changu nikampa akaomba uongozi wa Press uandae kikao na polisi tufahamiane.

Kimsingi nimedhalilishwa na kuzuiwa kufanya kazi lakini kwakuwa nina uongozi wangu wa Press naliacha mikononi mwao najua watakaa kikao kulijadili na kulitolea uamuzi.

Nimeachiwa niko HURU na vifaa vyote wamenikabidhi kwa sura hiyo. Nawashukuru wote waliopata taarifa ya kukamatwa kwangu, wote wameonesha kuwa karibu sana na mimi na Rukwa Press Club kujua kinachoendelea. Mungu anajua kipimo kinachowafaa cha shukrani zangu.


Asanteni 
Wilbroad Sumia 
Channel Ten Rukwa


Hayo ndiyo maelezo ya muandishi Wilbroad Sumia wa Chanel Ten Rukwa baada ya kuachiwa huru, 

Blog hii inakupa pole Bw. Wilbroad Sumia kwa usumbufu ulio jitokeza na kusababisha ushindwe kutekeleza majukumu yako! hata hivyo ni Muhimu kwa Uongozi wa Rukwa Press Club ukaitisha kikao kama ambavyo RCO ameomba ili kuweza kufahamina na kuwekena sawa  ili sintofahamu hii isijirudie tena!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni