Mambo 9 muhimu ya kufahamu kuhusu Ukatili kwa watoto
Tatizo la Ukatili dhidi ya watoto, linaongezeka siku hadi siku,
na kuleta athari mbalimbali za kimwili, kiakili, (kisaikologia) na kiafya kwa watoto.
Watoto wanaumizwa, kubakwa, kunajisiwa, kutelekezwa, kusafirishwa kibiashara na
kufanyishwa kazi za hatari zinazoathiri afya zao. Matendo haya ya kikatili
hayakubaliki kabisa.
Yafuatayo ni mambo 9 muhimu ya kufahamu kuhusu ukatili kwa
watoto:
1. Aina za ukatili
Ukatili dhidi ya watoto upo wa aina nyingi. Ukatili wa
Kijinsia, ni vitendo au maneno yanayoweza kusababisha madhara kwa mtu
au kundi la watu kutokana na maumbile yao. (Mf: kuguswa bila ridhaa, jaribio la
kubaka/kubaka, kulazimisha kufanya ngono n.k). Ukatili wa Kimwili ni
kama kupigwa, kusukumwa, au kutishiwa kuuwawa kwa silaha. (Mf: kuonyeshwa
kwamba hutakiwi, vipigo vya mara kwa mara) na Ukatili wa
Kiakili/Kisaikolojia, kutelekezwa, kubaguliwa, kutishwa. (Mf:
kuitwa majina mabaya, kunyimwa huduma za msingi, kufanyishwa kazi ngumu n.k)
dada wa kazi akimfanyia ukatili mtoto
2. Wahusika wa Ukatili dhidi ya watoto
Utafiti wa Ukatili dhidi
ya Watoto Tanzania ulifanyika mwaka 2009 na uliongozwa na Kikosi Kazi
kinachojumuisha Sekta mbalimbali za Serikali, Asasi za Kiraia na Wadau wa
Maendeleo. Katika utafiti huo ilionekana kuwa ndugu wa
karibu kama mjomba, baba, walezi na walimu ndio wanaosababisha ukatili dhidi ya
watoto. Kwa kuona hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine
wakaona umuhimu wa kuanzisha mpango wa kuelimisha jamii kuzuia ukatili dhidi ya
watoto.
3. Nini kifanyike kupunguza ukatili kwa
watoto
Wananchi wote kwa ujumla wana jukumu la kuhakikisha kwamba
wanawalinda watoto. Wazazi / walezi wanapaswa kujua watoto wao walipo na
wanachokifanya kila wakati na kuhakikisha usalama wa mahali watoto wanapopenda
kutembea mara kwa mara. Watoto wapewe moyo kuripoti vitendo mbalimbali vya
ukatili.
watoto
wakicheza katika mazingira hatarishi, hivyo ni jukumu la mzazi kujua usalama wa
eneo ambalo mtoto/watoto hucheza
|
4. Umuhimu wa kituo cha huduma ya simu
kwa mtoto - namba 116
Kituo cha huduma ya simu kwa mtoto ni muhimu
katika mifumo ya ulinzi wa mtoto nchini. Ni sehemu pekee ambayo mtoto au
Mzazi/Mlezi anaweza kupiga simu na kutoa taarifa za ukatili kwa siri na kupata
huduma ya ushauri nasaha na rufaa kwa msaada zaidi kwa mujibu wa tatizo lolote
linalohusu ukatili dhidi ya watoto. PIGA SIMU BURE kwenda namba 116 kutoa
taarifa za ukatili dhidi ya watoto.
5. Uchumi na Familia
Familia zikiwa na hali ngumu ya kiuchumi husababisha ugomvi kati
ya wanafamilia na hii huweza kupelekea kutelekezwa kwa watoto au kuwatenga
watoto na familia, jambo ambalo litaongeza hatari ya ukatili na unyanyasaji wa
watoto. Vilevile ugumu wa maisha ni kisababishi cha watoto wanaofanya kazi
katika umri mdogo, kuchuuza /kufanya biashara ya watoto, mimba zisizotarajiwa
na ndoa za utotoni. Hivyo basi ni muhimu wazazi/walezi kujishughulisha na kazi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa wanachama wa vikundi ili waweze
kuzalisha mapato ya kusaidia mahitaji ya familia.
Mtoto huyo akiwa katika kazi ya kupasua kokoto kazi ambayo inahitaji nguvu tofauti na uwezo wa mtoto
6. Madhara ya adhabu kwa watoto
Kuna madhara mengi sana ambayo yanaweza kuwapata watoto kutokana
na kupewa adhabu mbalimbali. Adhabu huleta hasira na chuki ambayo haisaidii
kuleta mabadiliko ya tabia. Kadri adhabu inapokuwa kali zaidi ndivyo
inavyopelekea mtoto kuwa na matatizo ya kutojithamini, kuwa mhalifu, kupata
magonjwa ya akili na kuwa na tabia ya ukatili. Adhabu mara nyingi haitoi
mchango chanya kwa maendeleo ya mtoto
7. Ishara ambazo huonyeshwa na watoto
waliofanyiwa ukatili
Ni muhimu kwa wazazi/ walezi kutambua ishara mbalimbali
zinazoonyeshwa na mtoto aliyefanyiwa ukatili. Ishara hizo ni kama vile mtoto
kutojiamini hata kama anafanya kitu sahihi anakua na hofu kwa sababu tu anahisi
anaweza kupigwa. Mtoto kukataa kwenda sehemu ambazo amezoea mf. shule,
ukifuatilia kwa ukaribu utakuta kuna mtu anamfanyia ukatili huko au njiani.
8. Wasikilize kwa makini
Ni muhimu kujijengea mazingira ya kumsikiliza mtoto kwa makini.
Unapofanya hivyo ni muhimu ajue kuwa unamsikiliza, aidha kwa kutumia ishara
bila maneno; kama vile kuashiria kwa kichwa. Mtazame mara kwa mara kwa mtazamo
wa kirafiki. Unaweza pia kurudia aliyokwambia kwa maneno mengine.
Mama akiwa karibu na watoto wake, hali ambayo huwafanya watoto kua huru na wenye furaha daima |
9. Umuhimu wa vyombo vya habari
kupambana na ukatili
Kwa mujibu wa mwongozo wa vyombo vya habari wa kuandika habari
za watoto uliochapishwa na Baraza la Habari Tanzania
(MCT), “Watoto wanahitaji uangalizi maalum wa kuwajali na kuwalinda.
Wakati wa kuandika habari za watoto, vyombo vya habari vinapaswa kujenga
taswira sahihi kwa watoto ili kuwaepusha katika hatari ya kuadhibiwa au
kunyanyapaliwa. Watoto ni binadamu wanaohitaji kutambuliwa, kupewa hadhi, utu,
heshima na zaidi ya yote kulindwa. Kutokana na ukweli huo, uelewa, umakini na
weledi wa uandishi wa habari zinazowahusu wao kwa kuzingatia hali yao na
mahitaji yao ni muhimu. Kimsingi vyombo vya habari vinatakiwa kuboresha uandikaji
wa habari za watoto na wakati huo huo kulinda usalama wao kimwili na
kihisia/jaziba.
muandishi
Emmanuel Lengwa wa gazeti la nipashe na ITV, alieripoti habari ya ukatili dhidi ya Bahati Kaminyonge na wazazi wake, mtoto Bahati alifungiwa ndani kwa miaka 10 huko Mbozi Mkoani Mbeya,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni