Jumatatu, 4 Aprili 2016

Ofisa mtendaji na Mwenyekiti wa kitongoji watupwa lupango kwa tuhuma za ubadhilifu

Wananchi wa kitongoji cha Nsalala Wilaya ya Mbeya wakisikiliza taarifa inayowahusu Ofisa mtendaji na Mwenyekiti wa kitongoji cha Nsalala,
Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Prosper Msivala, akisoma taarifa mbele ya wananchi
(Picha na Thomson Mpanji)

Ofisa mtendaji na Mwenyekiti wa kitongoji cha nsalala wakipandishwa kwenye kalandinga la polisi mara baada ya kusomwa kwa taarifa ya tume ya uchunguzi na kubainika kuhusika na tuhuma za kuuza ardhi

Ofisa Mtendaji na Mwenyekiti wa kitongoji cha Nsalala  Wilaya ya Mbeya wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuuza ardhi ya kijiji  kwa Sh8.6 milioni bila ridhaa ya wananchi
 
Tukio hilo lilitokea katika mkutano wa hadhara uliofanyika kufuatia wananchi kuwatuhumu viongozi hao kwa kuuza mali ya umma kisha kuziweka fedha hizo kwenye akaunti zao binafsi.
Wakizungumza katika mkutano huo wananchi hao walisema baada ya kubaini wizi huo  walimwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Upendo  Sanga wakitaka kuundwa kwa Tume ya uchunguzi ili kubaini fedha zinazodaiwa kuhodhiwa na viongozi hao bila ridhaa ya wananchi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo Mkurugenzi aliituma tume ya uchunguzi ambapo ilibaini tuhuma mbalimbali dhidi ya viongozi hao na kusoma maagizo mbele ya mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni  katika uwanja wa shule ya msingi Nsalala.
Akisoma taarifa hiyo  mbele ya wananchi  Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Prosper Msivala, alisema uchunguzi umebaini kuwa Mwenyekiti  anatuhumiwa kwa makosa kushiriki kuuza mali ya Umma kinyume cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011.
licha ya kutuhumiwa kuuza ardhi Mwenyekiti huyo  anatuhumiwa Kutunza fedha zilizotokana na mauzo hayo kwenye akaunti zake binafsi mbili zilizopo Benki ya NMB Mbalizi Road zenye namba 6251000804 na 62510009.
 
Kwa upande wa mtendaji wa kitongoji hicho  mwanasheria huyo alisema kuwa anatuhumiwa  kwa  matumizi mabaya ya madaraka kwa kushindwa kusimamia Kitongoji na kuwapotosha wananchi, kughushi nyaraka na mihutasari ya vikao nakukodisha eneo la maziko kwa shughuli za kilimo bila kufuata taratibu.
Mwanasheria huyo aliongeza kuwa kutokana na makosa hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ameagiza eneo lililouzwa kurudishwa mara moja kwenye Mamlaka ya Mji mdogo kanzia sasa.
aidha Mkurugenzi aliagiza kumsimamisha kazi mtendaji huyo  ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili na kuagiza  vyombo vya Dola kumchukulia hatua kali za kisheria Mwenyekiti wa Kitongoji .
Baada ya Mwanasheria kumaliza kuisoma barua hiyo kutoka kwa Mkurugenzi viongozi hao wote kwa pamoja  walichukuliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano  maalum.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni