Jumanne, 5 Aprili 2016

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO 
 
 
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA
MHE. UMMY MWALIMU (MB);WAZIRI
WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO,TAREHE 4 APRILI,2016



Ndugu wanahabari, Kila wiki  serikali  kupitia Wizara  yangu imekuwa  ikitoa  taarifa  ya mwenendo  wa mlipuko   wa  ugonjwa   wa Kipindupindu na hatua zinazo chukuliwa  kudhibiti ugonjwa  huu
  
Aidha  pia  kila  mwisho  wa  mwezi,  majumusiho  hufanyika na kutolewa  taarifa.  Hadi  kufikia  tarehe  4  April  2016,  jumla  ya  wagonjwa 20,294 wametolewa taarifa, na kati ya hao 320 wamepoteza maisha kwa   kipindi   cha   robo ya   kwanza ya mwaka,

mwenendo wa Kipindupindu unaashiria  kuwa  idadi  ya  wagonjwa  inaongezeka nchini. Mwezi  Januari kulikuwa na  wagonjwa 2,272,na  mwezi  Machi  kulikuwa  na  wagonjwa 2,956.

Hili  ni ongezeko  la  asilimia 30.1% hata  hivyo,  baadhi  ya  mikoa  imeonyesha  uendelevu wa kupungua kwa idadi ya wagojwa wa Kipindupindu kwa robo ya kwanza. Mikoa hiyo ni pamoja  na  Simiyu,  Rukwa  na  Mbeya.

Takwimu  hizi  za nchi  nzima zinaashiria  kuwa  juhudi  za  kupambana  na  ugonjwa  wa  Kipindupindu  zinahitaji kutekelezwa  na kusimamiwa kikamilifu  na  mikoa  na wilaya zote  nchini.

Baada  ya Wizara  yangu  kutoa  maelekezo  na  miongozo  stahili. Vile  vile,  napenda  kusisitiza kwamba  hata Mikoa  ambayo  haina  wagonjwa ni  lazima wachukue  hatua  za tahadhari kuzuia maambukizi mapya, na ile mikoa ambayo ina wagonjwa iendelee kusimamia kikamilifu udhibiti wa mlipuko.

Katika   mwezi   Machi,   jumla   ya wagonjwa   wapya  walioripotiwa nchi   nzima walikuwa 2,956,na vifo vilikuwa 53. Takwimu za mwezi Machi (tarehe 5 Machi hadi  3  Aprili) zinaonyesha  idadi  ya  wagonjwa  imeongezeka  kwa asililmia 59.5% ikilinganishwa  na  idadi  ya  wagonjwa  wa  mwezi  Februari  (1,853).

Mikoa  ya Tanga, Pwani na Mtwara haikuwa imeriporti wagonjwa mwezi wa Februari lakini mwezi  huu wa  Machi imepata  wagonjwa  wapya. Aidha  katika  kipindi  hiki  cha mwezi mmoja kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wapya kwenye mikoa ya  Geita,  Kilimanjaro,  Manyara,  Morogoro,  na  Dodoma.  Idadi  ya  wagonjwa kutoka  mikoa  ya  Simiyu,  Mbeya  na  Iringa  imepungua  kati  ya  Februari  na  Machi 2016.

Kwa  upande  wa  takwimu  za  kila  wiki  (weekly  report),  idadi  ya  wagonjwa  wa Kipindupindu walioripotiwa kwa  wiki  ya kati  ya  tarehe 28 Machi  hadi  3  Aprili 2016 imepungua kwa  asilimia 37.2 ikilinganishwa   na   idadi   ya  wagonjwa walioripotiwa  kati  ya  tarehe 21  hadi  27 Machi  2016.  Kwa  wiki  hii  ya tarehe 28 Machi hadi 3 Aprili 2016 kulikuwa na jumla ya wagonjwa wapya 430 na vifo saba (7).

Idadi ya  vifo  kwa  wiki  hii  imeongezeka  kutoka  vifo vinne vilivyoripotiwa katika wiki  iliyopita. Kwa  wiki  hii  mikoa  iliyo pata wagonjwa  wengi  zaidi ni Kilimanjaro (128), Mara (102), Morogoro (67), Geita (46), Mwanza (40) na Dar es Salaam(31).

Halmashauri kumi zilizoongoza kwa idadi ya wagonjwa wapya wiki hii  ni  Same  (74),  Tarime  Vijijini  (52),  Moshi  Vijijini  (44),  Mvomero  (27),  Rorya 3(26),  Ilemela  (25),  Korogwe  Mjini  (25),  Morogoro  Vijijini  (25),  Chato  (24)  na Tarime Mjini (20) Ugonjwa wa Kipindupindu hadi sasa haujaripotiwa kutoka mikoa ya Njombe
na Ruvuma.

Ndugu wanahabari,
Wizara inapenda kutoa pongezi kwa Mikoa na Wilaya zinazoendelea kutoa taarifa sahihi  na  kwa  wakati  pamoja  na  juhudi  za  kudhibiti  ugonjwa  huu.  Ninaendelea kusisitiza kuwa ni lazima kwa Mikoa na Wilaya kutoa taarifa ya wagonjwa wapya wa  Kipindupindu  kwa  kuzingatia  mfumo  wa  ufuatiliaji  wa  magonjwa  ujulikanao kama   “Integrated    Disease    Surveillance    and    Response    (IDSR)”,    ambao unasimamiwa  na  Waganga  Wakuu  wa  Mikoa  na  Wilaya. 

Utoaji  wa  taarifa  sahihi na  kamili  (ikiwa  pamoja  na  linelists)  kwa  wakati  utasaidia  kuweka  mikakati  ya upesi ya kudhibiti ugonjwa huu usisambae kwa kasi na kuleta madhara zaidi.

Ndugu wanahabari,Wizara  inasisitiza  kuwa  kwa  wakati  huu  wa  masika,  uwezekano  wa  kuongezeka kwa ugonjwa wa Kipindupindu ni mkubwa, hivyo ni lazima wananchi wazingatie kanuni  za  usafi  binafsi  na usafi  wa mazingira.

Kama  tunavyoelekeza  mara  kwa mara, ni  marufuku   kwa   watu   kutitirisha   maji taka ovyo, na pale   hilo litakapofanyika basi hatua  za kisheria  zitachukuliwa.

Aidha  tunawasihi  viongozi mbalimbali wa ngazi zote; za vitongoji, vijiji, kata na tarafa kusimamia kikamilifu sheria ya Afya ya Mazingira hususan wakati huu wa mvua za Masika.

Tukumbuke kwamba kipindupindu kinahitaji juhudi kubwa zifanywe na wananchi na viongozi wa  ngazi  mbalimbali, hivyo  tushirikiane kuhakikisha  tunaepuka  kuchafua vyanzo vya maji. 

Aidha, Serikali kupitia  Wizara  yangu  na kwa kushirikiana  na  wadau mbalimbali inaendelea  na juhudi  za  kutoa  miongozo,  maelekezo  na  ufuatiliaji  juhudi za kudhibiti ugonjwa huu likiwemo zoezi la ugawaji wadawa kwa ajili ya
kutakasa  maji  (Chlorine  tablets,  mfano waterguard)  katika mikoa  iliyoathiriwa zaidi na Kipindupindu.

Ndugu wanahabari,
Nahimiza yafuatayo yazingatiwe katika kudhibiti magonjwa ya milipuko;

1.
Utoaji  wa  taarifa  mapema  katika  vituo  vya  kutolea  huduma  za  afya  pale wanapoona wagonjwa wana dalili za magonjwa ya milipuko.

2.
Kutilia  mkazo  usafi  wa  mazingira  kwa  ujumla
kama  Ofisi  ya  Rais TAMISEMI  inavyoelekeza.  Kila  Jumamosi  ya  mwisho  wa  mwezi,  ni  budi tushirikiane katika kufanya usafi wa mazingira kwani hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ugonjwa huu.
 

3.
Watumishi wa afya waendeelee kutoa tiba kwa wagonjwa wa Kipindupindu kwa  uadilifu  na kwa  kuzingatia  miongozo  inayotolewa.  Aidha  waendelee kutoa elimu kwa wananchi ya kujiepusha kupata maambukizi.

4.
Juhudi  za  udhibiti  wa  kipindupindu  zifanyike  kwa  ushirikishwaji  wa  karibu wa viongozi wa kijamii, hususan viongozi wa kidini na wa kimila

5.
Viongozi   na   Watendaji   katika ngazi mbalimbali   waendelee   kuchukua tahadhari  (Preparedness)  kwa  magonjwa  haya na  mengine  yatokanayo  na Mvua za Masika.

6.
Wamiliki wote wa vyombo vya usafiri wana agizwa kutoa taarifa mara moja kwenye kituo cha afya kilichopo karibu pindi umuonapo abiria anayetapika au kuharisha.

Hitimisho Wizara inaendelea kutoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja  katika  jitihada  za  kutokomeza  ugonjwa  wa Kipindupindu. 

Aidha, Wizara inaendelea  kuwashukuru wataalamu  wa  sekta  husika, Mashirika  ya Kimataifa,Watumishi, Mikoa  na  Halmashauri  pamoja na waandishi  wa  habari na  wananchi
kwa ujumla kwa kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.

Asanteni sana

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni