Jumanne, 5 Aprili 2016

Uwanja wa ndege wafungwa kwa muda baada ya ndege mbili kugongana.

Ndege ya Batik Air ambayo ilikua na abiria 49
Ndege ya TransNusa
Uwanja wa ndege wa mji wa Jakarta nchini Indonesia umefungwa kwa muda baada ya ndege mbili kugongana.
Ndege ya kubeba abiria ya shirika la Batik Air ilikuwa ikipaa ubawa wake ulipogonga sehemu ya nyuma ya ndege ya shirika la TransNusa iliyokuwa kwenye njia ya kutumiwa na ndege zinazo kupaa au kutua.
 
Ubawa wa ndege hiyo iliyokuwa ikipaa uliwaka moto.
Maafisa wanasema hakuna aliyejeruhiwa wakati wa ajali hiyo iliyotokea Jumatatu usiku.
 
Abiria wote waliondolewa salama.
Kisa hicho kilitokea katika uwanja wa ndege wa Halim Perdanakusuma mjini Jakarta ambao hutumiwa sana kwa safari za ndege za ndani ya nchi.
 
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, ndege hiyo ya Batik Air ilikuwa na watu 49, abiria pamoja na marubani.
Msemaji wa kampuni ya Lion Air Group, inayomiliki Batik Air ameambia mashirika ya habari ya kimataifa kwamba rubani amekatiza safari baada ya ajali hiyo na abiria wako salama.
 
Maafisa wa wizara ya uchukuzi ya Indonesia wamesema ndege hizo ziliharibiwa wakati wa kisa hicho. Video iliyopakiwa mtandaoni inaonesha miali ya moto ikitoka kwenye ubawa wa ndege ya Batik Air.
 
Indonesia ina historia mbaya ya usalama wa ndege licha ya kuendelea kufana na uchukuzi wa ndege hasa ndege za kubeba abiria za bei nafuu.
 
Mwaka 2013, ndege ya Lion Air ilipita njia ya uwanja wa ndege wa Denpasar, Bali na kutumbukia baharini. Watu 22 walijeruhiwa.
 
Mwaka uo huo, ndege nyingine ya Lion Air iliteleza ikitua kisiwa cha Sulawesi na kugonga ng’ombe.
 
Mwaka 2014, ndege ya kampuni ya AirAsia nchini Indonesia iliyokuwa safarini kutoka Surabaya hadi Singapore ilianguka baharini na kuua watu wote 162 waliokuwa ndani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni