Jumatatu, 18 Aprili 2016

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

  

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 18 APRILI, 2016

Ndugu wanahabari,

Kama mnavyofahamu, Serikali kupitia Wizara yangu imeweka utaratibu wa kutoa kila wiki taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini  ili kuifahamisha jamii hali ilivyo na hatua zinazochukuliwa na Wizara  kudhibiti ugonjwa huu. Hadi kufikia tarehe 17 April 2016, jumla ya wagonjwa 20,882 wametolewa taarifa, na kati ya hao ndugu zetu 329 wamepoteza maisha tangu ugonjwa huu uliporipotiwa Agosti 2015.

Takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 10 hadi 17 Aprili 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa wiki hiyo ni 212  ikilinganishwa na 368 wa wiki iliyotangulia.  (April 04 hadi  Aprili 10, 2016). Mikoa ambayo bado imeendelea kuripoti ugonjwa wa kipindupindu ni 10. Mikoa iliyopata wagonjwa wengi zaidi ni Morogoro (wagonjwa 51 na Kifo 1), Mara (45), Kilimanjaro (31), Pwani (24), na Tanga (24). Aidha hakuna Mkoa mpya uliotoa taarifa ya kuwepo kwa wagonjwa wa Kipindupindu.
Pia katika wiki hii Halmashauri zilizoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Morogoro vijijini (23), Same (20), Tarime mjini (20), Mvomero (wagonjwa 18, na Kifo 1) na Kinondoni (16). Vile vile, katika wiki hii Mikoa ambayo haijapata mgonjwa wa Kipindupindu ni Kigoma, Dodoma, Singida, Shinyanga, Tabora, Lindi, Kagera, Rukwa, Katavi, Mbeya, Simiyu, Iringa na Mtwara.

Tafsiri kubwa tunayoipata kutoka kwenye takwimu hizi ni kwamba kwa sasa ni dhahiri kuwa juhudi zetu za pamoja za kupambana na ugonjwa wa Kipindupindu zimeonyesha matunda. Wizara inawapongeza wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa na katika kusimamia kikamilifu  miongozo inayotolewa na Wizara .

Vile vile, napenda kusisitiza kwamba pamoja na kwamba tuna Mikoa ambayo haijaripoti wagonjwa au mikoa ambayo imekuwa haina wagonjwa wapya kwa muda, bado hali si salama, hususani wakati huu wa mvua za masika, na kwa kuwa na uwepo wa mwingiliano mkubwa wa watu kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usafiri na za biashara. Hali hii bado inaweza kupelekea ugonjwa wa Kipindupindu kuenezwa kutoka mkoa wenye uambukizo na kwenda kwenye mikoa mingine. Hivyo ni budi mikoa yote nchini kuendelea  kuchukua hatua za tahadhari ili kuzuia maambukizi, na pia kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa kila siku, hata kama hakuna wagonjwa, na kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huo.

Ndugu wanahabari,

Kufuatia Agizo la Mhe. Waziri Mkuu alilolitoa kwangu tarehe 31 mwezi Machi 2016, Wizara yangu itaendelea kutoa miongozo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya juu ya hatua gani za kutekelezwa ili kuweza kudhibiti Ugonjwa huu na kuweza kuutokomeza kabisa. Ninamshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa kuniamini na kunipa mamlaka ya kutoa miongozo kwa wakuu hawa juu ya ugonjwa wa kipindupindu. Aidha ninapenda kumhakikishia Mhe. Waziri Mkuu kuwa Wizara yangu itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kutokomeza ugonjwa huu kwa kushirikiana kwa karibu sana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini, pamoja na Viongozi wa Wizara nyingine. Wizara pia itaendelea kumshirikisha Mhe. Waziri Mkuu kuhusu hatua mbalimbali za udhibiti wa ugonjwa huu, na kuainisha changamoto zitakazojitokeza ili kuweza kudhibiti ugonjwa huu. Aidha Wizara yangu pia itaendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo tuliyoyatoa kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wiki mbili zilizopita katika kikao kilichofanyika Mkoani Dodoma ili kuweza kutathmini mwenendo wa ugonjwa huu na kuudhibiti. Ili kusimamia hili Wizara inaagiza mikoa kutuma taarifa za shughuli mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huu kila wiki kwa mujibu wa miongozo itakayotolewa na Wizara.

Ndugu wanahabari,

Katika kipindi hiki cha masika, Wizara inatoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira. Napenda kurudia   kwamba n marufuku   kw watu   kutitirisha   maj tak ovyo, hasa katika kipindi hiki,  kwani kwa kufanya hivyo vimelea vya ugonjwa vinaweza kuenezwa kirahisi sana kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Tunahimiza mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote watakaokiuka sheria ya Afya ya Jamii.  Aidha tunawasihi viongozi mbalimbali wa ngazi zote; za vitongoji, vijiji, kata na tarafa kusimamia kikamilifu suala hili, hususan wakati huu wa mvua za masika. Wizara inasisitiza kwamba kila jitihada zifanyike kote nchini ili kuhakikisha kuwa jamii yote ya Watanzania inatumia maji safi na salama. Hii ni pamoja na kuzingatia taratibu za kutibu maji ya kunywa katika ngazi ya kaya.

Ndugu wanahabari,
Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
§  Utoaji na upatikanaji wa takwimu sahihi za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara, na bila kuingiliwa na viongozi wa kisiasa au kiserikali.
§  Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yote ya mijini na vijijini ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu,
§  Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia Mamlaka za maji zilizopo katika ngazi zote nchini,
§  Kuhakikisha upatikanaji wa ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
§  Kuhakikisha utunzaji salama wa maji ya kunywa yaliyotibiwa,
§  Kufikisha wagonjwa wa Kipindu pindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu,
§  Kuhakikisha upatikanaji na matumizi sahihi ya ORS katika maeneo mbali mbali nchini ili kupunguza athari za ugonjwa

Aidha, Vyombo vya usafiri vihakikishe vinatekeleza yafuatayo ili kudhibiti ugonjwa usisambae;
§  kuwa na dawa ya jiki na pakiti za ORS kwenye sanduku la huduma ya kwanza kwa ajili ya kusafisha gari na kumhudumia mgonjwa atakaekuwa anatapika na kuharisha kabla ya kupelekwa kituo cha afya kilicho karibu,
§  visipeleke abiria kujisaidia sehemu ambazo hazina vyoo, maarufu “kuchimba dawa”
§  Visiwapeleke abiria kwenye sehemu za vyakula ambazo zipo kwenye mazingira ambayo si safi,

Hitimisho

Wizara inaendelea kuwashukuru wataalamu wa sekta mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla, kwa kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu hapa nchini. Tunawasihi hali hii iendelee kwa juhudi kubwa zaidi ili tuweze kutokomeza Kipindupindu nchini haraka iwezekanavyo. Kipindupindu kinataka kuota mizizi katika jamii zetu, tusikubali jambo hili litokee. Kwa ushirikiano wa pamoja tunaweza kukitokomeza kabisa

Asanteni sana

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni