Diwani wa Kata ya Katumba Katika Manispaa ya Mpanda Mkoani katavi
Bwn Senator Baraka Jerith (30) amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za Rushwa
zinazomkabili.
Mapema asubuhi Tume ya kudhibiti na kupambana na Rushwa Mkoani
katavi wamemfikisha diwani huyo kizimbani Kwa tuhuma za kushawishi na kupokea
Rushwa jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Mwanasheria wa Takukukuru Saimoni Buchwa aliyesaidiwa na Mwenzake
Bahati Stafu Haule akisoma hati ya Mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Mhe Chiganga Tengwa katika kesi iliyosajiliwa kwa
Na CC 1/2016
ameileza Mahakama kwamba Mshitakiwa anatuhumiwa na Makosa Mawili
ambayo ni kushawishi na kosa la Pili kupokea Rushwa.
Katika Kosa la Kwanza Inadaiwa kwamba Mshitakiwa alishawishi kwa
nia ya kupokea Rushwa kinyume na Kifungu Cha Sheria ya Kudhibiti na kupambana
na Rushwa Kifungu cha 15(1)(a) Sheria na 11 ya Mwaka 2007 kwamba Mnamo tarehe
11/5/2016 Mshitakiwa alimshawishi ndugu CHARLES MSUKUMA kwamba atamsaidia
kutohamisha mifugo yake katika eneo tengefu la makazi ya Wakimbizi la Katumba
iwapo angekubali kutoa Shilingi Milioni Moja ili asitekeleze amri hiyo kama
alivyoamuriwa na Mahakama ya Mwanzo Katumba yeye kama Diwani wa Kata hiyo jambo
ambalo ni kinyume na Sheria za Nchi.
Katika kosa la Pili, Mshitakiwa anashitakiwa kwa Kosa la kupokea
Rushwa kinyume na Kifungu cha 15(1)(b) cha Sheria ya kudhibiti na kupambana na
Rushwa Na 11 Mwaka 2007.
Kwamba Mnamo tarehe 12 mwezi mei 2016 katika Mgahawa wa Mtu
aitwaye Ngandieta katika Kata ya Katumba Diwani huyo alipokea kiasi cha
Shilingi Laki Nne Kama sehemu ya malipo ya fedha waliokubaliana awali.
Aidha Mshitakiwa amekana Makosa yote na Mahakama kumtaka
adhaminiwe Kwa masharti ya kuacha Mahakamani Pesa Taslimu Milioni mbili au Hati
ya Mali isiyohamishika yenye thamani ya kulingana na fedha hiyo.
Mwanasheria wa Takukukuru Saimoni Buchwa ameiomba Mahakama
kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa kwa Shauri hilo Kwa kuwa upelelezi wa
shauri hilo haujakamilika.
Mshitakiwa amepelekwa mahabusu kwa kutotimiza masharti na kukosa
wadhamini. Kesi imepangiwa tarehe 31/5/2016 itakapo tajwa tena.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni