Serikali
mkoani Mbeya imekamata kiwanda bubu cha kufungasha sukari, ambacho kinadaiwa
kufungasha upya sukari ya ndani kwenye mifuko yenye ujazo wa kati ya nusu kilo
na kilo moja na kisha sehemu ya sukari hiyo kuuzwa nje ya nchi na nyingine
kusambazwa mitaani.
Kukamatwa kwa kiwanda
hicho kunatokana na hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Munasa akiwa
ameongozana na askari Polisi kuingia mwenyewe mitaani kutekeleza agizo la Rais
Dk. John Magufuli la kuwasaka wafanyabiashara ambao wameficha sukari kwenye maghala.
Akiwa mitaani, ndipo
akabaini uwepo wa kiwanda hicho kikiwa katika nyumba moja ya makazi ya watu
iliyopo maeneo ya Soweto Jijini Mbeya, huku mifuko inayotumika kufungashia
sukari hiyo ikiwa na nembo isiyoonyesha mahali sukari hiyo ilipotengenezewa.
Akizungumza baada ya
kubaini uwepo wa kiwanda hicho, Munasa alisema kuwa viwanda vya aina hiyo
ndivyo vinavyotumika kufungasha sukari ambayo wakati mwingine huwa
imepitwa na wakati na kuwauzia wananchi, hali ambayo inaweza kuwasababishia
madhara kiafya.
“Viwanda vya aina hii
ndivyo vinavyotumika kufungasha sukari feki, iliyopitwa na wakati, wao kwenye
mifuko hii wanaandika tarehe nyingine ya sukari kumaliza muda wake, hali ambayo
inaweza kuwadhuru watumiaji,” alisema Munasa.
Aidha Munasa alimuuliza
Mmiliki wa kiwanda hicho, Bushir Sanga kama ana kibali kutoka kwenye viwanda vya
ndani vinavyompa mamlaka ya kubadilisha jina la sukari, ambapo alisema kuwa
hana kibali cha kutoka kwenye viwanda kinachomruhusu kufanya hivyo.
Hata hivyo Sanga ambaye
pia ni mfanyabiashara maarufu wa sukari Jijini Mbeya alidai kuwa ana kibali cha
kufanya shughuli hiyo kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), na pia
anatambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuwa huwa analipa kodi.
“Ninayo leseni ya TFDA
na pia huwa nalipa kodi hivyo natambuliwa hata na TRA hivyo shughuli yangu ya
kufungasha sukari ni halali kisheria,” alisema Sanga.
Maelezo hayo hayakutosha
kumshawishi Mkuu wa wilaya kuwa mfanyabiashara huyo hana kosa, hivyo akawaamuru
askari wa Jeshi la Polisi kumkamata na kumfikisha kituoni ili achukuliwe
maelezo na baadaye afikishwe kwenye vyombo vya sheria ili sheria ifuate mkondo
wake.
Kutokana na uhaba wa
sukari uliolikumba Taifa, Rais Dk. John Magufuli ameviagiza vyombo vya dola
kuwatafuta na kuwakamata wafanyabiashara ambao wameficha sukari kwenye magahala
ili bidhaa hiyo ionekane ni adimu na hatimaye iweze kupanda bei.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni