JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
07/06/2016 TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu zangu waandishi wa habari, Katika siku za hivi karibuni,
Jeshi la Polisi nchini, limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa
wakitaka kufanya mikutano na maandamano . hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia
vyanzo vyake mbalimbali vya habari limebaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la
kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi (Civil disorder).
Aidha vyama vingine vya siasa vimeonyesha dhamira ya kupinga kile
ambacho kitasemwa na wapinzani wao. Vyanzo hivyo vya habari vimebainisha kwamba
upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya kisiasa.
Kwa hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linapiga marufuku maandamano
na mikutano ya hadhara kuanzia tarehe 07/06/2016 hadi hapo hali ya usalama
itakapotengemaa.
Jeshi la Polisi linawataka wanasiasa kuacha mara moja
kuwashinikiza wananchi kutotii sheria za nchi. Jeshi la Polisi halitasita
kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au chama chochote cha siasa
kitakachokaidi agizo hili.
Aidha Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuwa makini na wanasiasa
wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi hii na badala yake linawasihi
waendelee kushirikiana katika kujenga umoja wa nchi hii.
Asanteni sana kwa kunisikiliza .
Imetolewa na:- Nsato M. Mssanzya – CP Kamishina wa Polisi
Operesheni na Mafunzo
Makao Makuu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni