Jumanne, 7 Juni 2016

Jeshi la Polisi lawataka wananchi kuondoa hofu na wasiwasi badala yake kutoa ushirikiano ili kuwabaini wahalifu!!!

Jeshi la polisi nchini limesema kua hali ya amani na usalama nchini ipo shwari licha ya kuwapo kwa baadhi ya matukio machache  ya kihalifu katika mikoa michache kama vile Mwanza, Tanga na Dar es salaam.

Katika Pres iliyotolewa na kupitia msemaji wa Jeshi la Polisi Advera J. Bulimba  Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jeshi limewatoa hofu wananchi na kusema kua matukio hayo tayari yanaendelea kushughulikiwa na baadhi ya watuhumiwa wanaojihusisha na matukio wamesha kamatwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani ili sheria kuchuku mkondo wake.  

Hata hivyo rai imetolewa kua wakati jeshi likiendelea na uchunguzi wa matukio hayo  wananchiwametakiwa kuondoa wasiwasi na badala yake watoe taarifa za ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuhakikisha wale wote wanaojihusisha na uhalifu wanakamatwa.

Sanjari na kuimarisha ulinzi pia jeshi limesema kuwa zoezi la uhakiki wa silaha lililoanza tarehe 21/03/2016 bado linaendelea nchi nzima ambapo linafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu hadi tarehe 30/6/2016. 

Zoezi hili la uhakiki wa silaha lipo kwa mujibu ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, ambapo kifungu cha 66 cha sheria hiyo kinamtaka kila mmiliki kuhakiki kumbukumbu za silaha yake au risasi pale atakapoamriwa na mamlaka husika.

Imeelezwa kua lengo la kuhakiki kumbukumbu za wamiliki wa silaha ni kupata taarifa sahihi za wamiliki hao lakini pia taarifa zitakazosaidia kubaini wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria. Aidha, zipo sababu nyingine kwa mfano, wapo wamiliki ambao walikwishahama kutoka katika makazi yao ya awali na kuhamia katika makazi mapya.

Pia wapo baadhi ya wamiliki ambao walishafariki na silaha zao bado hazijakabidhiwa katika vituo vya polisi, jambo ambalo linaweza kusababisha silaha hizo kutumika katika vitendo vya uhalifu.

Zoezi la uhakiki wa silaha linakwenda sambamba na ulipaji wa madeni ya ada za leseni za kumiliki silaha ambayo wamiliki wanadaiwa.

Kufuatia zoezi la uhakiki wa silaha linaloendelea, wito umetolewa kwa wamiliki wote wa silaha kujitokeza kuhakiki silaha zao haraka katika kipindi hiki kilichobaki wakiwemo watu binafsi, makampuni binafsi, Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali. 

Aidha, wananchi ambao ndugu zao walikuwa wanamiliki silaha na kwa sasa wamefariki, au wamepatwa na matatizo ya kiafya wazisalimishe silaha hizo katika vituo vya Polisi ndani ya kipindi hiki cha zoezi la uhakiki wa silaha.

Sambamba na zoezi hili la uhakiki wa silaha zinazomilikiwa kihalali, wito umetolewa kwa watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha hizo katika vituo vya Polisi, ofisi za serikali na kwenye nyumba za ibada na watakaofanya hivyo ndani ya muda uliopangwa hawatachukuliwa hatua zozote za kisheria.

Na kwamba baada ya tarehe 30/06/2016 hakutakuwa na msamaha kwa yeyote atakayekuwa amekaidi zoezi hili.

Baada ya muda huo, Jeshi la Polisi nchini litaendesha operesheni kali kwa lengo la kuwasaka na kuwakamata wale ambao watakuwa hawakujitokeza katika zoezi la uhakiki au kusalimisha silaha ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni zao na silaha zao kutaifishwa na kuwa mali ya serikali.

Wamiliki wa silaha za kiraia wanaozimiliki kihalali wanatakiwa kuzitunza silaha zao ipasavyo ili zisiangukie kwenye mikono ya wahalifu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni