Marehemu Daud Mwangosi enzi za uhai wake |
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imesema mtuhumiwa wa kesi ya mauaji
ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Daudi
Mwangosi, ana kesi ya kujibu.
Mtuhumiwa huyo Pacificius Cleophace Simoni alifikishwa mahakamani
hapo akituhumiwa kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika
kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012.
Akitoa uamuzi huo jana, Jaji wa mahakama hiyo, Paul Kiwelo
alisema; “Mahakama imejiridhisha kwamba katika shauri lililoko mbele yetu,
tuhuma ambazo zimetolewa dhidi ya mtuhumiwa na kwa kuzingatia ushahidi
uliotolewa na upande wa Jamuhuri, mtuhumiwa ana kesi ya kujibu kwahiyo
natupilia mbali ombi la upande wa utetezi lililotaka kesi hii itupiliwe mbali
kwa madai kwamba hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaomuhusisha mtuhumiwa
na mauaji hayo.”
Jaji Kiwelo alisema mtuhumiwa huyo ataanza kujitetea kesho baada
ya kuridhia ombi hilo lililotolewa na wakili wa upande wa utetezi Lwezaula
Kaijage na kuungwa mkono na mawakili wa Jamuhuri, Sandy Hyra na Ladslaus
Komanya.
Mara baada ya Jaji huyo kutoa uamuzi huo, askari Polisi zaidi ya
20 waliokuwa ndani ya chumba cha mahakama hiyo, walimfunika shuka mtuhumiwa
huyo ili wanahabari wasipate fursa ya kumpiga picha.
Mtuhumiwa huyo alitolewa mahakamani hapo na kundi la askari hao,
akiwa amefichwa katikati yao, hatua ambayo pia iliwazuia wanahabari kufanya
kazi yao vizuri. Tofauti na watuhumiwa wengine, mtuhumiwa huyo aliyekuwa askari
wa FFU Iringa kabla ya kufikishwa mahakamani hapo aliondolewa katika eneo la
mahakama kwa kutumia gari dogo la Polisi aina ya Landlover badala ya
kupandishwa katika kalandinga kama inavyofanywa kwa watuhumiwa wengine.
Kabla na baada ya kesi hiyo kusikilizwa baadhi ya wanahabari
walilalamika kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Ruth Massam namna
baadhi ya askari waliokuwa wamevaa kiraia na sare za jeshi hilo walivyokuwa
wakiwatisha wakati wakiwazuia kupiga picha.
Wanahabari hao walilalamika kwamba kila kesi hiyo inapofikishwa
mahakamani hapo, kumekuwa na kawaida ya kuwepo kwa idadi kubwa ya askari
wanaovaa kiraia na wale wanaovaa sare, huku baadhi yao wakiwa na silaha za moto
jambo ambalo pia linawaogopesha na kuwakwamisha kufanya kazi zao kwa staha.
Akizungumzia malalamiko hayo, Msajili huyo alisema mahakama
inaendelea kuyafanyia kazi huku akisisitiza shughuli za kimahakama ni shughuli
zao ambazo hazipaswi kuingiliwa na mtu mwingine na kwamba atazungumza na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ili asaidie kutoa maelekezo kwa baadhi ya
askari wake wanaotaka kuingilia uhuru wa mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni