Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe |
Wakati Mhariri wa Gazeti la Dira na mwenzake wako mahakamani
kujibu mashtaka ya kuandika na kusambaza taarifa za uongo kwa lengo la
kusababisha hofu nchini, uongozi wa StarTV umepiga marufuku gazeti hilo kusomwa
asubuhi na kumwomba radhi Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe
kwa usumbufu aliopata kufuatia kituo hicho cha runinga kusoma gazeti la Dira
siku ya Jumatatu tarehe 20 Juni, 2016.
Taarifa kutoka ndani ya Sahara Media Group Ltd, wamiliki wa
StarTV, zimesema msimamo huo ulichuliwa na kiongozi wao mkuu Anthony Diallo
jana na taarifa hizo zimethibitishwa leo kwa njia ya simu na Dk. Mwakyembe.
"Ni kweli nimeongea na Diallo, nimeelewa changamoto za
kuongoza watu wengi na nimepokea apology yao, jambo ambalo ni uungwana.
"Nimefarijika kuwa nao wametambua kuwa gazeti hilo halina viwango, hivyo
hawatalisoma tena asubuhi", alisema Dk. Mwakyembe.
Wakati huohuo, Waziri huyo mwandamizi katika Serikali ya Awamu ya
Tano amesema maandalizi ya kufungua kesi ya kashfa dhidi ya mmiliki, mhariri,
mchapishaji na wasambazaji kwa taarifa za uongo zilizo chapishwa hivi karibuni
na gazeti hilo yanaendelea vizuri.
Mhariri wa Gazeti la Dira ya Mtanzania,Bw. Musa Mkama na mwandishi
Prince Newton wameachiwa kwa dhamana ya sh. 5 milioni kwa kila mmoja baada ya
kupandishwa kortini katika mahakama ya Kisutu kwa kosa la kuandika habari zinazodaiwa
kuwa niza uongo na kuleta taharuki katika jamii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni