Jumanne, 12 Julai 2016

Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala latoa Tamko, Vituo 8 vyapewa adhabu kama onyo,kusitisha huduma kwa muda na kufutiwa usajili, akiwemo Dr. Mwaka wa Foreplan Clinic, ambaye amefutiwa usajili na kuzuiwa kutoa huduma!!


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO.

BARAZA LA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA

TAARIFA KWA UMMA 12/07/2016
UTANGULIZI:

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lilianzishwa kisheria chini ya Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Na. 23 ya Mwaka 2002- Sura 244. kwa lengo la kusimamia , kudhibiti na kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala. Baraza lilizinduliwa rasmi mwaka 2005.

USAJILI WA WAGANGA WA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA.
Kwa mujibu wa sheria, waganga, wauza dawa na wasaidizi wa waganga wa tiba asili na tiba mbadala pamoja na vituo kama hospitali,kliniki na maduka ya dawa za tiba asili na tiba mbadala ni lazima zisajiliwe na Baraza kabla ya kuanza shughuli ya utoaji wa huduma.

Utaratibu wa kisheria ulioainishwa unahitaji mtoa huduma kuchukua fomu katika ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya au halmashauri, kuijaza na kupeleka katika serikali za mtaa au kijiji ambapo inajadiliwa na wajumbe wa kamati ya afya ya mtaa au kijiji na kupitishwa ,inapelekwa katika ofisi za kata,kisha ofisi za mganga mkuu wa wilaya au halmashauri na kwenda kwa mganga mkuu wa mkoa na mwisho kuletwa Wizarani katika ofisi ya Msajili wa Baraza la Tiba Asili la Tiba Mbadala.
Utaratibu huo uliwekwa ili kuepuka usajili wa waganga matapeli, waovu wasioenenda kwa maadili na wasiotambulika na wananchi wa sehemu husika wanayotolea huduma.

Hata hivyo ni muhimu watu wote wanaohusika na utoaji wa fomu na kupitisha maombi ya usajili wawe watumishi wa serikali au wajumbe wa kamati za afya za serikali ya mitaa au vijiji, kutokuweka urasimu, kutokuchelewesha zoezi na kutokuweka mazingira ya rushwa kwa waombaji(watoa huduma). 

Kumekuwepo na baadhi ya watendaji na wenyekiti wa serikali za mitaa au vijiji pamoja na waratibu kuchelewesha maombi ya usajili kwa makusudi na wengine kuwatoza hela isiyohalali waombaji hao.

Baraza linakemea tabia hiyo, na kusisitiza kuchukua hatua za kisheria na kuwashtaki wale wote watakaohusika na tabia hiyo. Fomu hizo za maombi zinajadiliwa kwenye vikao vya kawaida vya kisheria vya kamati za afya za serikali za mitaa au vijiji na si vinginevyo, hivyo waganga hawapaswi kutozwa fedha yeyote.

Baraza linasisitiza kuwa usajili wa waganga kiserikali unatolewa na na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala hautolewi na chama chochote cha waganga, shirika lolote au taasisi nyingine yeyote.

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala limepata taarifa ya baadhi ya waganga wakishirikiana na watu wengine kughushi vyeti vya Baraza na kuviuza kwa gharama,pia wengine kuuza fomu za maombi ya usajili, na viongozi wengine wa vyama mbalimbali vya waganga, kuchana vyeti vya baraza ambavyo ni nyaraka za serikali na kuwarubuni waganga kwa kuwatoza hela na kuwapa vyeti vya vyama vyao na kuwaambia kuwa usajili wa serikali haufai, baraza linashughulikia taarifa hizo na limeaanza kuchukua hatua za kisheria kwa wale wanaohusika na tuhuma hizo, na linawaonya wengine kuacha mara moja tabia hiyo.

Baraza linawataarifu waganga wote wa tiba mbadala kuwa litaanza uhakiki wa vyeti vyao vya sekondari na vyuoni, hivyo waviandae na kuviwasilisha Baraza ndani ya mwezi mmoja.
Mhe.Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alitoa tamko la serikali kupitia vyombo vya habari tarehe 16/01/2016 lililowaagiza Waganga wote wa tiba asili na tiba mbadala kuhakikisha kuwa wamejisajili ifikapo Juni 15, 2016. Waganga, wasaidizi na wauza dawa waliojisajiliwa mjini ni 480 na vijijini ni 1,840,jumla yavituo ni 64, kiwanda 1, usajili wa kudumu wa waganga 109 na fomu ambazo hazikupata usajili ni 30 jumla ya maombi yote ya usajili yaliyoletwa Baraza ni 2,523.

Hivyo waganga 10,958 walisajiliwa hadi Januari 2016 na waganga 2320 wamesajiliwa baada ya tamko la Mhe. Waziri na kufanya idadi ya wasajiliwa kuwa 13278, vituo 112 na usajili wa kudumu wa waganga 540 tangu usajili wa Baraza ulipoanza.

Baraza linatoa pongezi za dhati kwa ofisi za waganga wakuu wa mikoa na wilaya au halmashauri zake za mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mwanza kwa kuleta maombi mengi zaidi ya usajili na kuhamasisha usajili wa waganga wengi, hata hivyo linasisitiza mkoa wa Manyara kuhamasisha usajili ambapo ni waganga wawili tu ambao wamesajiliwa na msaidizi wa mganga mmoja tangu usajili ulipoanza Baraza.

Aidha, Baraza limepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wateja, juu ya muda wa kupata leseni ya usajili baada ya kuleta maombi kuwa ni mrefu na kuna ucheleweshaji mkubwa, baraza limepokea malalamiko hayo na linaangalia utaratibu mzuri ambao utapunguza urasimu na ucheleweshaji mkubwa wa leseni, ili kuwawezesha wateja kutopata usumbufu mkubwa. Hata hivyo kwa sasa ni muhimu waganga kufuata sheria.

TAARIFA YA USAJILI WA DAWA.
Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala limechukua hatua za kukutana na wadau mbalimbali wanaohusika katika uchunguzi wa dawa (TFNC, TFDA, NIMR, ITM, maabara kuu ya taifa, Idara ya Kemia ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Idara ya Mimea ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam , Mkemia mkuu wa serikali,) Ili kuhakikisha kuwa watumiaji wa dawa za tiba asili na tiba mbadala wanatumia dawa zisizoleta madhara kwa afya zao.

Baraza litaanza kusajili dawa za tiba asili za aina ya pili(category 2 materia medica) tu.
 
Baraza liko katika hatua za mwisho za kukamalisha taratibu za usajili wa dawa na litatangaza rasmi usajili wa dawa hizo utakapoanza. Hata hivyo Baraza linahamasisha waganga wote kupeleka dawa zao kwa mkemia mkuu wa serikali ili kutambua kama hazina sumu na zinafaa kwa matumizi ya binadamu kwa hatua za awali.


MATANGAZO NA VIPINDI KWENYE VYOMBO VYA HABARI:
Kwa mujibu wa sheria mganga kabla ya kupeleka tangazo lake katika vyombo vya habari ni lazima kwanza tangazo hilo lipitiwe na baraza na kupewa kibali. Pia taarifa yeyote inayohusu tiba asili na tiba mbadala ni lazima ipitishwe na baraza kabla ya kufikia umma.

Sababu ya kutoa kibali ni kuondoa uwezekano wa kuwepo kwa matangazo ya uongo na yasiyofaa, taarifa zisizo za kweli na kushushia hadhi tiba asili na tiba mbadala.

Ieleweke kwamba huduma za tiba asili na tiba mbadala zinagusa zaidi maisha na afya za wananchi moja kwa moja na hivyo si vyema zikaachwa ziendeshwe kiholela bila utaratibu wa kitaalamu na kimaadili.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na baadhi ya matangazo na vipindi vinavyorushwa katika redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii kuhusu utoaji wa matibabu ya tiba asili na tiba mbadala kinyume cha utaratibu na maadili.

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala limekuwa likifuatilia matangazo ya waganga kwenye vyombo vya habari na kubaini uwepo wa matangazo yasiyokuwa na kibali cha Baraza, baadhi ya waganga kuendelea kutoa elimu ya tiba asili na tiba mbadala kwa umma kinyume na katazo la waziri, pamoja na kutangaza vituo vya kutolea huduma ambavyo havijasajiliwa na Baraza, 
Baraza limewaita baadhi ya matabibu waliowekwa kwenye tuhuma mbalimbali na kuhojiwa na kamati ya maadili na baadae maamuzi ya baraza kufanyika kwa kuzingatia ukubwa wa makosa yao na urudiwaji wa mara kwa mara wa makosa hayo. 

Baraza linasisitiza kufuata sheria kwa kuwa litakuwa makini sana na halitakuwa na huruma kwa yeyote aliyesajiliwa atakayevunja sheria ili kuipa heshima inayostahili huduma ya tiba asili na tiba mbadala kwani ni huduma ya afya kama ilivyo tiba ya kisasa. 

Hivyo wafuatao ni wale waliopewa adhabu.
Tabibu Esbon Baroshigwa wa kituo cha Aman Herbal Clinic – amepewa barua ya onyo
Tabibu Castory Ndulu wa kituo cha Ndulu Herbal Clinic– amepewa barua ya onyo
Tabibu Simon Rusigwa wa kituo cha Sigwa Herbal Clinic – amesimamishwa kutoa huduma za tiba asili kwa miezi sita. 
Tabibu John Lupimo wa kituo cha Lupimo Sanitarium Clinic.– amesimamishwa kutoa huduma za tiba asili kwa miezi sita
Tabibu Fadhil Kabujanja wa kituo cha Fadhaget Sanitarium Clinic– amefutiwa usajili, na hivyo haruhusiwi kutoa huduma.
Tabibu Juma Mwaka Juma wa kituo cha Foreplan Clinic– amefutiwa usajili na hivyo haruhusiwi kutoa huduma.
Tabibu Abdallah Mandai wa kituo cha Mandai Herbal Clinic – amefutiwa usajili na hivyo haruhusiwi kutoa huduma .

Baraza linawaagiza waratibu wote chini ya waganga wakuu wa mikoa na wilaya au halmashauri popote vilipo vituo vya waganga waliositishwa au kufutiwa usajili kuhakikisha kuwa vituo vyao vinasitisha kutoa huduma na kuviondoa kwenye orodha mpaka pale mtakapojulishwa vinginevyo.

Aidha, kutokana na ukiukwaji mkubwa wa sheria unaofanywa na baadhi ya watoa huduma wa tiba asili na tiba mbadala, Baraza la tiba asili na tiba mbadala linaweka utaratibu mzuri wa utoaji wa vibali vya matangazo hivyo utoaji wa vibali umesitishwa kwa muda hadi hapo itakapotangazwa vingenevyo, waganga wote wenye vibali vya kutangaza wavirejeshe mara tu baada ya muda wa kibali cha kutangaza walichopewa kuisha.

Baraza linawatangazia waganga wote wenye nia ya kutangaza huduma zao wasiingie mikataba mipya na vyombo vya habari,ili kuepuka usumbufu na kupata hasara mpaka hapo watakapojulishwa. 

Ni muhimu waganga kuzingatia muda wa kibali chako cha matangazo unapoisha.

Baraza linatambua kuwa wateja wake wanajihusisha na shughuli nyingine zaidi ya tiba ya asili na tiba mbadala,hivyo halizuii wateja kutangaza shughuli zao nyingine, isipokuwa tabibu yeyote atakayetangaza au kutoa elimu nyinginezo, asihusishe na tiba anayotoa, dawa zake au kutumia jina la tabibu katika hayo, atakapofanya hivyo amejitangaza na kutangaza tiba zake bila kibali hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

AGIZO KWA WARATIBU WA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA WA MIKOA NA WILAYA AU HALMASHAURI

Waratibu wote mnatakiwa kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waganga wote ambao hawajajisajili na kutoa taarifa katika ofisi ya Msajili wa Baraza la tiba asili na tiba mbadala kwa kila hatua iliyochukuliwa.

Pia kuleta majina ya waganga wote wanaoendelea kutoa matangazo ya tiba asili na tiba mbadala na kutoa elimu bila kibali cha baraza ili kuwachukulia hatua za kisheria.

Hitimisho.
Baraza linasisitiza kuwa waganga waendelee kufanya usajili kupitia kwenye ofisi za waratibu wa tiba asili katika wilaya na halmashauri zao husika, pia watoe huduma katika sehemu walizosajiliwa na wasitoe huduma kwenye nyumba za kulala wageni.
Aidha, kila mtoa huduma lazima asajiliwe yeye mwenyewe, msaidizi/wasaidizi wake, na kituo chake cha kutolea huduma pia kiwe kimesajiliwa kupitia ofisi za mganga mkuu wa halmashauri husika.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
……………………………….
Dkt. Edmund Kayombo
MWENYEKITI WA BARAZA
LA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA.
12/07/2016

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni