KAMPUNI YA RELI
TANZANIA(TRL) TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI -PRESS RELEASE MTU MMOJA AFARIKI
KATIKA AJALI YA KICHWA TRENI KUGONGANA NA BASI LA UDA JANA USIKU:
Mtu mmoja afariki
dunia baada ya basi la UDA kukigonga kichwa cha treni cha Kampuni ya Reli
Tanzania(TRL) katika makutano ya reli na barabara ya Kamata saa 3:20 usiku jana
Julai 26, 2016.
Marehemu ametambuliwa
kwa jina la Omari Abdallah Nyumba mkazi wa Mbagala, Aidha majeruhi 43 wa ajali
hiyo walipelekwa hospitali ya Taifa ya Mhimbili ambapo watatu kati yao ni
mahututi.
Taarifa za awali za
Kikosi cha Polisi Reli zinaeleza kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya dereva
Majuto Hamis wa basi hilo la UDA aina ya Hecher lenye namba za usajili T969 CVP
kukaidi amri ya kusimama iliyotolewa na Mfanyakazi wa TRL.
Dereva huyo ni mmoja
wa majeruhi ambaye amevunjika miguu na yuko chini ya ulinzi wa Polisi wa Reli
akiwa wodini baada ya majeruhi wote kupatiwa huduma. Kichwa cha treni
kilichogongwa ni cha kazi za sogeza Namba 7317 kilikuwa kikitokea kituo kikuu cha
treni cha Dar es Salaam.
Kikosi cha Polisi TRL
wameahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya majeruhi wa ajali hiyo. Tokea
uanze mwaka huu kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa sheria za barabarani kwa
watumiaji wa vyombo vya moto hasa madereva wa pikipiki za bodaboda kutokuwa
makini katika kuzitii sheria hizo zinazosimamia makutano ya reli na barabara.
Tokea kuanza kwa mwaka
huu wa 2016 ajali nyingi zimeripotiwa hapa jijini Dar es Salaam, Morogoro,
Dodoma, Manyoni mkoani Singida zikihusisha vyombo hivyo.
Wito unatolewa na
Uongozi wa TRL kwa watumiaji wa vyombo vya moto boda boda , magari mkubwa na
mabasi na wananchi kwa jumla kuzingatia sheria ili kuepuka madhara makubwa
ikiwemo kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na pia upotevu wa rasilimali
muhimu ambazo kama zikitumiwa vizuri zitaboresha maisha ya wananchi na Taifa
kwa ujumla.
Imetolewa na Afisi ya
Uhusiano:
Kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
Julai 27, 2016
DAR ES SALAAM
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni