Jumanne, 12 Julai 2016

Muandae mtoto (mwanafunzi) kwa kufanya haya kabla na baada ya kuanza shule ya msingi

Moja ya kikwazo cha mwanafunzi kushindwa kimasomo ni kuzoea mazingira ya shule ambayo ameandikishwa au amefaulu kujiunga nayo.

Kama wengi wetu tunavyofahamu,
watoto wengi hulelewa na wazazi wao na kushinda kutwa nzima wakideka na kubembelezwa, huku wakiwa na uangalizi wa karibu kutoka kwa ndugu wanaowafahamu.

Sasa unapokuja muda wa mtoto aliyelelewa hivyo kuandikishwa shule na kushinda na watu ambao hakuwazoea, anaweza kuathirika kisaikolojia kwa kushindwa kujiamini na wakati mwingine kukinai mapema masomo.


Wasi wasi wa kupigwa na wenzake ambao ni watukutu unaweza kumfanya mwanafunzi akaanza kutoroka shule au kutozingatia masomo kwa kiwango stahili.

Wataalamu wanaliorodhesha suala la mtoto kuanza shule kama tatizo linaloweza kuleta mfadhaiko wa akili na kuharibu ufahamu wa mwanafunzi.

Inatajwa kuwa asilimia 26% ya wanafunzi hukumbwa na hofu pale wanapoambiwa kuwa wanakwenda masomoni mbali na wazazi wao. Kwa maana hivyo ni vema mwanafunzi akafundishwa namna ya kukabili tatizo hili.

MWANAFUNZI SHULE YA MSINGI

Kwa kuwa watoto wengi wanaoanzishwa shule ya msingi huwa na umri mdogo wa kati ya miaka sita na saba, umri ambao ufahamu wao ni mdogo ni wajibu wa mzazi kuhakikisha kuwa anapomwandikisha mwanae kuanza masomo ya darasa la kwanza amfanyie yafuatayo:

KWANZA: Ahakikishe anamwandaa vya kutosha kukabili mazingira mapya ya maisha ya shule, inashauriwa kuwa mtoto anayekaribia kufikia umri wa kwenda shule ni vema akatengwa kimalazi na wazazi wake. Hii itamuongezea ujasiri wa kukabiliana na mambo madogo madogo akiwa peke yake.

PILI: Mtoto anapopelekwa shule asiachwe bila ulinzi wa mtu anayeweza kumtegemea katika matukio ya kumuogopesha. Ni wajibu wa mzazi kumkabidhisha mwanae kwa mwalimu au mwanafunzi mwingine anayemfahamu ili amtie imani wakati anapofadhaishwa na wakati mwingine kumlinda anapoonewa.

TATU: Mzazi amuwezeshe mtoto wake katika mahitaji ya msingi kwa mfano mavazi safi, madaftari, pesa za matumizi, vyote hivi ni kumuondolea hali ya kujiona duni hasa pale anapokutana na wenzake ambao wanamzidi katika hayo niliyotaja na mengineyo.

NNE: Ni wajibu wa mzazi kufuatilia malalamiko ya mwanae atakayoleta pindi atokapo shule na kumuongoza.

Ikiwa anapigwa na wenzake ni vema mzazi akampeleka mwanae shule na kuzungumza na waalimu namna watakavyosaidiana nao kumlea na wakati huo huo kumuonyesha mtoto kimbilio lake pindi atakapokuwa shuleni.

TANO: Lazima mzazi amtie moyo mwanae kwa kumpatia zawadi kila anaporudi kutoka shule na amsifie kwa kazi zake “Kwa sababu leo umeamka mwenyewe nakuzawadia pipi kumi na kesho ukiwahi nitakununulia juisi”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni