Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana msanii wa muziki wa
kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego hadi hapo
litakapojiridhisha kwamba
ametekeleza maagizo yote aliyopewa na Baraza sambamba
na yeye kubadilika katika kubuni kazi zenye maadili na zisizo dhalilisha watu
wa kada mbalimbali.
Maagizo aliyopewa
Msanii Nay ni pamoja na kulipa faini (adhabu) ya kiasi cha Shilingi milioni 1,
kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa ‘Pale Kati’, kufuata sheria,
kanuni na taratibu za urasmishaji sekta ya Sanaa kwa maana ya kusajiliwa na
BASATA na kuhakikisha wimbo wake umefuata taratibu zote.
Aidha, Msanii Nay
ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki yenye kuvunja
maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususani wanawake.
Maamuzi haya
yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria nambari 23 ya mwaka 1984,
ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na waraka wa Wizara ya Habari,
Utamaduni na Michezo wa tarehe 16/7/2009 ambayo kwa sasa inafahamika kama
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Adhabu hizi zimetolewa
kufuatia BASATA kufanya kikao cha pamoja na Msanii huyu jana siku ya Jumanne
tarehe 26/07/2016 kwenye Ukumbi wa Baraza na yeye kukiri makosa na kuahidi
kubadilika.
Makosa aliyosomewa na
yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na; 1. Kujihusisha na shughuli za Sanaa
pasipo kusajiliwa na BASATA. 2. Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia katika
mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake. 3. Maudhui
ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa matumizi ya wazi na ni
kinyume cha sheria za nchi na maadili ya mtanzania.
Ikumbukwe kwamba mnamo
tarehe 16/07/2016 BASATA lilitoa taarifa kwa umma ya kuufungia wimbo wa Pale
Kati kufuatia kubeba maudhui yenye uvunjifu mkubwa wa maadili na kupambwa na
picha dhalilishi kwa wanawake.
Aidha, tarehe
12/02/2016 BASATA liliufungia wimbo wa Shika Adabu Yako wa Msanii huyuhuyu kwa
makosa yanayofanana na haya.
Hivyo adhabu hii
imetolewa ili kumpa muda wa kujifunza, kujitathimi na kujirekebisha kama kweli
ana nia ya kuendelea kufanya kazi ya muziki SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA
KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI,
BASATA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni