MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kyela, imemuhukumu kifungo
cha miaka 30 jela, Mkazi wa Kyela Kati, Malisam Masoud (31), baada yakupatikana
na hatia ya kupora pikipiki kwa kutumia silaha, huku wenzake wawili wakiachiwa
huru.
Adhabu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Rhoda
Ngimilanga,baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na
upande wa mashitaka.
Akitoa hukumu katika shauri hilo namba 166 ya mwaka 2014,
alisema ametoa adhabu hiyo ili kukomesha vitendo hivyo na kuwa onya wenye nia
mbaya ya kutaka kutenda kosa kama hilo waache na wajifunze kuepuka vitendo
hivyo.
Ngimilanga alieleza mahakamani hapo kuwa, kosa hilo nikinyume na
kifungu cha 287 (2) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho
yake mwaka 2012.
Hata hivyo, hakimu huyo alisema baada ya kuchambua kwa kina ushahidi
ulioletwa mahakamani hapo, umeshindwa kuwatia hatiani watuhumiwawengine wawili
katika kosa hilo, Furaha Alex na Iddy Abdalah (wote wakazi wa Mbeya) kutokana
na ushahidi kushindwa kuthibitisha bila kuacha mashaka.
Awali ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wapolisi,
D/CPL Danford, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo, Novemba 11 mwaka 2014 majira
ya saa moja jioni katika kijiji cha Kikusya, Wilayani humo.
Aliongeza kuwa,kwa lengo la kutenda uovu, mshitakiwa
alimkodi mlalamikaji, Bernard Mwaisaka, ambaye ni mwendesha Bodaboda, lakini
kwa lengo la kutimiza nia yake ovu mshitakiwa baada ya kufika eneo la Kikusya
alimgeuka dereva huyo wa bodaboda na kuanza kumshambulia kwa visu sehemu
mbalimbali za mwili wake kabla ya kupora Pikipiki hiyo, yenye usajili wa
T 444 CPB aina ya Bajaji Boxer.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni