Jumatatu, 1 Februari 2016

Samatta aipa neema Club ya Simba






BAADA ya dili la mshambuliaji, Mtanzania, Mbwana Samatta kujiunga na Klabu ya Genk ya Ubelgiji kutimia, habari nzuri kwa klabu yake ya zamani ya Simba ni kuwa inatarajia kuvuna Sh milioni 200 kutokana na kipengele ambacho kiliwekwa na uongozi wa timu hiyo wakati unamuuza kwa Klabu ya TP Mazembe ya DR Congo, miaka mitano iliyopita.

Samatta ambaye anashikilia Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, wiki iliyopita alitua rasmi ndani ya Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa mkataba wa miaka minne akitokea TP Mazembe huku akikabidhiwa jezi namba 77.

Kipengele ambacho uongozi wa Simba wa wakati huo uliokuwa unaongozwa na mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage, kinasema kuwa klabu hiyo itapata asilimia 20 za fedha ambazo mshambuliaji huyo atauzwa kwenda klabu yoyote akitokea Mazembe.

Samatta aliuzwa kutoka Mazembe kwenda Genk kwa euro laki saba (zaidi ya sh bilioni moja za Kitanzania) ambazo kwa kipengele walichokiweka Simba cha asilimia 20, basi watapata milioni 200.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully amesema kuwa wanatambua kuwa wao wanatarajia kupewa fedha hizo kutokana na mkataba ambao waliingia na Mazembe.

“Tunajua kuwa baada ya Samatta kuuzwa kwenda Genk sisi tunapata asilimia 20 za fedha zitakazopatikana kutokana na makubaliano maalumu yaliyowekwa wakati kijana huyo anaingia mkataba na timu ya TP Mazembe.

“Kwa sasa tumeshaanza kufanya mipango kuona kuwa tunafuatilia fedha hizo na kuzipata kwa wakati ambapo zitakuja kuweka sawa mambo mengine,” alisema Tully.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni