Picha hii ikimuonesha mwanamke akiwa katika hali ya ujauzito |
Miaka ya karibuni limekuwapo ongezeko la wanawake kujifungua watoto
kabla ya kufikia wakati wake. Anayezaliwa katika mazingira hayo huitwa mtoto
njiti.
Mtoto anayezaliwa katika
mazingira hayo hutunzwa katika mazingira maalumu hospitalini kwa kuwa wakati
huo mwili wake unakuwa hauna uwezo wa kuhimili kikamilifu maisha nje ya tumbo
la uzazi.
Kwa sababu hiyo, mama hubakia
hospitali kwa muda fulani wakati akiwa anaendelea kupatiwa huduma maalumu
itakayomsaidia aendelee kukua na kuimarika. Hali hii huongeza gharama kwa
familia tofauti na mtoto anayezaliwa akiwa amefikia umri.
Wataalamu wa afya wanasema
mama kujifungua mtoto ambaye hajatimiza miezi tisa ya ujauzito, kunasababishwa
na mambo mengi yanayoweza kuepukika.
Daktari bingwa wa magonjwa ya
wanawake nchini Cuba, Dk Jose Hernandez, anasema asilimia 80 ya sababu hizo
zinaweza kudhibitiwa ikiwa mama atajipanga mapema kushika ujauzito miezi sita
kabla, huku akitunzwa vema kwa kipindi chote mpaka kujifungua.
Dk Jose anasema matumizi
yasiyo sahihi ya dawa ikiwamo dawa za magonjwa mbalimbali, pombe, dawa za
kulevya yameongeza idadi ya wanawake kujifungua watoto njiti duniani.
Anasema matumizi ya Cocain,
Heroin, bangi, mirungi, sigara au kupata moshi kutoka kwa mtu anayevuta ni
sababu tosha zinazosababisha mjamzito kujifungua mtoto njiti.
Anasema wanaume wengi
wamekuwa wakivuta sigara mbele ya wake zao jambo linalohatarisha wajawazito.
Mambo mengine yanayoweza
kusababisha tatizo hilo, anasema ni magonjwa mbalimbali kama shinikizo la damu
na malaria.
“Kuna ugonjwa wa malaria;
ikiwa mama atapata wale wadudu, moja kwa moja wanakwenda kushambulia kwenye
kondo ambalo ni utumbo maalumu unaomlisha mtoto kutoka kwa mama.
Kwa kuwa atakuwa
ameshambuliwa na bakteria, atakuwa dhaifu na hatimaye kusababisha mazingira
yatakayomlazimisha mtoto azaliwe kabla ya wakati.
Anasema tatizo lingine ni
upungufu wa vitamini mwilini, shambulio la bakteria kwenye njia ya mkojo
maarufu kama UTI na upungufu wa damu.
Iwapo damu ya mama ni ndogo
inakuwa haimtoshelezi yeye na mtoto hivyo, mazingira hayo yatalazimisha azaliwe
kabla ya muda wake kufika.
Sababu nyingine ni uwepo wa
magonjwa ya zinaa kama kaswende, kisonono na virusi vya ukimwi (VVU).
Dk Jose anataja mazingira
mengine kuwa ni ya mama kuzaa mfululizo bila kupata muda wa kupumzika.
“Kujifungua mara kwa mara
hasa bila kupitisha miaka miwili, huchangia kwa kiasi kikubwa kujifungua kabla
ya wakati kwa kuwa kizazi chake kinakosa muda wa kupumzika na kujiandaa kwa
ajili ya utungwaji wa mimba nyingine,” anasema.
Kinachoweza pia kusababisha
mama kujifungua mtoto njiti, anasema ni mjamzito ambaye anapendelea kula
vyakula vya vyenye sukari kwa wingi na wakati mwingine chumvi inapozidi.
“Vitu hivyo humsababishia
mama matatizo katika uzazi na wengi hupata kisukari cha mimba ambacho kitabibu
ni hatari,”
Aidha kifafa cha mimba pia kimetajwa kuwa ni sababu kuu kwa kina mama
walio wengi kujifungua kabla ya wakati.
Na kwamba kifafa hicho
kimegawanyika mara mbili ikiwa ni pamoja na shinikizo la moyo kuwa juu zaidi ya
140/90.
“Katika mazingira hayo mama
mjamzito huonyesha dalili za mwili kujaa na ukichunguza katika mkojo wake unakuta
kuna protini nyingi,”
Anafafanua kuwa protini hizi
zinapenya kwenda katika mkojo badala ya kukaa katika damu na kumsaidia yeye
pamoja na kichanga.
Mwenye tatizo kama hilo
inabidi apate msaada wa karibu wa daktari kwa kumchunguza na kushauri hatua
mwafaka za kuchukuliwa ili kulinda uhai wa mama na mtoto.
Suala la utoaji wa mimba wa mara kwa mara ni miongoni
mwa sababu zinazochangia mama kujifungua mtoto njiti.
Anasema kitendo cha utoaji mimba wa mara kwa mara husababisha misuli ya
mlango wa kizazi kulegea na makovu kuwa mengi ndani ya kizazi.
Makovu mengi kwenye kizazi, yanasababisha
kondo kushindwa kujishika kikamilifu kwenye ukuta huo na kuifanya kuwa rahisi
kujiachia.
Hali nyingine ambazo wanawake
hawana budi kuziepuka anazitaja kuwa ni kubeba mimba katika umri mdogo au kuwa
na vioteo ndani ya kizazi kama vile fibroidi.
Kwa mujibu wa taarifa za
kitaalamu za Novemba 2014 inaelezwa kua Nchini Tanzania, kila mwaka, watoto zaidi ya 200,000
huzaliwa mapema sana kabla ya muda wao (watoto njiti) na zaidi ya 9,000
miongoni mwao hufariki kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa mapema
mno.
Kwa mujibu wa ripoti iliyo wahi kutolewa na ya Shirika la
Afya Dunia (WHO) inayoonyesha kuwa watoto wengi hufariki duniani kwa sababu ya
kuzaliwa njiti, ambapo pia shirika hilo lilieleza sababu mbalimbali
zinazosababisha mama mjamzito kujifungua mtoto njiti, ikiwa ni pamoja na kupata
uchungu mapema kabla ya muda unaotakiwa.
WHO lilisema historia inaonyesha
kuwa kinamama wengi hujifungua mapema kutokana na kushika mimba mara kwa mara,
maambukizi ya maradhi na kupatwa magonjwa sugu kama Kisukari na Shinikizo la
damu, kupata uchungu wa muda mrefu. ukosefu wa lishe bora kwa kinamama
wajawazito, wanawake kupata mimba wakiwa na miaka chini ya 18 au zaidi ya miaka
35 na matumizi ya pombe na sigara.
Aina tatu za watoto njiti
Shirika la Afya Duniani linasema
kuna aina tatu za watoto wanaozaliwa njiti; kundi la kwanza ni wale ambao
huzaliwa kabla ya wiki 28 (extreme preterm). Watoto wanaozaliwa katika kipindi
hiki huhifadhiwa katika mashine maalumu (incubator), ambapo asilimia 90 ya
watoto wanaozaliwa katika kundi hilo barani Afrika hufariki dunia.
Kundi la pili la watoto njiti
huzaliwa kati ya wiki 28 na 32, ambapo huhitaji mashine kwa ajili ya
kuwaongezea joto mwilini, ingawa pia husumbuliwa na magonjwa ya mfumo wa hewa kutokana
na matatizo ya mapafu.
Kundi la mwisho la watoto njiti
huzaliwa kati ya wiki 32 na 37, ambapo kati yao asilimia 60 ya vifo vya watoto
hao hutokea barani Afrika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni