Na Moses Ng'wat,
Watu wawili, Geneli Kapwela (65) na Rahab Bungulu (70), wakazi wa kata
ya Matema, Wilayani Kyela, wameuawa kikatili kwa kukatwakatwa sehemu mbalimbali
ya miili yao na kisha kuchomwa moto,wakituhumiwa kuleta ugonjwa wa kipindupindu
kwa njia ya kishirikina kijijini hapo.
Tukio la watu hao kuuawa, ambao ni mume na mke lilitokea usiku wa
Februali mbili, wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao walimokuwa wakiishi katika
kitongoji cha bulinda katika kata ya Matema, Wilayani Kyela.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kwamba jumla ya watu wawili tayari wanashikiliwa na jeshi hilo.
"Katika tukio la kwanza, marehemu Geneli aliuawa kwa kutenganishwa kichwa
chake na kiwiliwili na mkono wa kushoto nao kukatwa na viungo hivyo hadi sasa
havijulikani vilipo" alifafanua Msangi.
Aliongeza kuwa, baada ya watu hao ambao tayari wawili wamekatwa kutekeleza
unyama huo waliamua kuiangusha nyumba ya marehemu hao ambayo ilijengwa kwa
nyasi na makuti na kisha kuiwasha moto huku miliili ya marehemu ikitejetea kwa
moto.
Aliwataja watu wawili wanaoshikiliwa na jeshi hilo kuwa ni Aliko Mwamtibe (47)
na Solomoni Mwamtobe (49) wote wakazi wa kitongoji cha Bulunda.
Akizungumzia tukio hilo wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha
baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika jana, Mkuu wa wilaya ya
Kyela, Dk. Thea Ntala, aliagiaza jeshi la polisi kuwakamata wahusika wote kwani
wapo ambao wamekimbia baada ya kutekeleza unyama huo.
"Hii ni aibu kubwa kwa wilaya yetu kuona kuna watu wanaamini kuwa
kipindupindu kinaambukizwa kwa njia ya kishirikiba, wito wangu kwa jeshi la
polisi kuhakikisha linawakamata wote waliohusika." alisema Dk. Ntala.
Wilaya ya Kyela ni miongoni mwa wilaya nchini ambazo zimekuwa zikikumbwa na
ugonjwa wa kipindupindu mara kwa mara, ambapo tangu ulipuke Disemba mwaka jana
jumla ya watu wawili wamepoteza maisha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni